Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mapinduzi afichua aliyoyapitia Yanga, ataja majeraha

Muktasari:

  • Mwezi mmoja baadaye, Mapinduzi alishtua umma kufuatia taarifa za kuumia kwake vibaya akiwa mazoezini tena akiumia mwenyewe, bila kuumizwa na mtu. Jeraha ambalo lilikuwa ndio ufunguo wa kufifisha maisha yake ya soka.

Ilikuwa Januari 4, 2020 mchezo mkubwa Tanzania Simba na Yanga zipo Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, wekundu hao wakitangulia kwa mabao 2- 0 ya mshambuliaji Meddie Kagere na winga Deo Kanda.

Simba walikuwa wanaona kama ni siku yao lakini kumbe haikuwa hivyo, akatoka kijana mmoja mfupi wa kimo mwenye utundu wa miguu kutoka Yanga, Mapinduzi Balama akifunga bao la kikatili dakika ya 50 kwa shuti kali lililojaa moja kwa moja wavuni. Kisha dakika tatu baadaye beki wa wekundu hao Mohammed Hussein 'Tshabalala' akajifunga kisha mchezo kumalizika kwa mabao 2-2.

Mechi hiyo ilipoisha staa aliyeimbwa kuliko wote alikuwa mmoja tu, Mapinduzi maarufu kwa jina la Kipenseli, kikubwa lilikuwa bao lake la kikatili lililobadilisha mchezo mzima, Yanga wakimbeba na kumuona kama mkombozi.

Mwezi mmoja baadaye, Mapinduzi alishtua umma kufuatia taarifa za kuumia kwake vibaya akiwa mazoezini tena akiumia mwenyewe, bila kuumizwa na mtu. Jeraha ambalo lilikuwa ndio ufunguo wa kufifisha maisha yake ya soka.

Ingawa Mapinduzi amefanikiwa kurudi uwanjani, lakini bado sio yule aliyekuwa kabambe kabla ya kuumia, akiendelea kupambana kujirudisha kwenye ubora wake akiwa na Kikosi cha Jeshi Mashujaa FC.

Jeraha lile lilimsumbua Mapinduzi na kukaa nje takribani misimu miwili, akipambana na hatua mbalimbali za kupigania kipaji chake. Hatua iliyolifanya Mwananchi kumtafuta na kutaka kujua kwa undani hatua ya jeraha lile, mpaka kupona kwake. Hapa anasimulia;

"Nakumbuka nilikuwa Yanga, majeraha nilipata wakati tunajiandaa na mchezo dhidi ya Ndanda wakati wa mazoezi kutokana na ubovu wa viwanja vyetu hivi.

“Ilitokea tu nataka kuzuia mpira, nikaacha mguu ikasababisha kupata ufa kwenye mfupa na ilinifanya kukaa nje ya uwanja kwa takribani miaka miwili hivi,” anasema.

Mapinduzi anasema hali hiyo ilisababisha yeye kupoteza matumaini ya kurudi tena kwenye mpira, ila watu waliomzunguka, wamshauri aendelee na matibabu yake huku akiishukuru Yanga kwa kumsaidia.

Anasema kuwa alitumia fedha nyingi kwenye matibabu, ikifikia hadi Sh20 milioni, “Kama mimi nilitumia pesa hiyo, sijui kwa upande wa Yanga ilitumia gharama gani, maana walinisafirisha mpaka Afrika Kusini nilikaa takribani miezi miwili.”

“Kwa sababu jeraha langu lilikaa muda mrefu bila matibabu muhimu na ilitokana na kutokutilia maanani ukubwa wa tatizo, yaani tulikuwa tunaona ni kitu cha kawaida, kwa hiyo tulipofika Sauzi (Afrika Kusini) kule ikabidi tuanze upya kwa sababu nilichelewa, ilinichukua muda mrefu kurudi maana kule nilienda baada ya kukaa miezi saba au nane hivi.”

Anasema aliishi na maumivu miezi hiyo yote, kwa sababu alikuwa bado hajatibiwa. Hivyo alivyofika Afrika Kusini alianza upya matibabu.

Alipofika Afrika Kusini

Mapinduzi anasema alivyofika Afrika Kusini walimwambia kuwa ameumia katika kifundo cha mguu na amepata mpasuko kidogo kwenye mfupa.

Hivyo ilibidi afanyiwe upasuaji na kukaa tena miezi sita na baada ya hapo alitakiwa kuanza kutafuta unafuu kwa miezi karibu minne, mpaka akae sawa kabisa kiafya ndipo ilipotimia miaka miwili bila kucheza mpira.

Anasema haikuwa rahisi, ni jambo ambalo linahitaji mhusika awe na washauri wanaomkuzunguka, bila hivyo mchezaji unaweza kukata tamaa.

"Yanga ni timu ambayo ilionyesha kujali, kama isingekuwa hivyo sidhani kama leo ningekuwa na uwezo wa kucheza tena mpira. Kwa hiyo naishukuru Yanga pia ilinisaidia kwa hilo tena kwa asilimia kubwa sana."


Changamoto ilipoanzia

Hata hivyo Mapinduzi anasema alivyopata majeraha hayo aliona ni kawaida, hata madaktari wa kipindi hicho cha mwanzo walichukulia suala hilo ni kawaida, hivyo naye alichukulia kawaida kwa kuwa walimtaarifu kuwa baada ya miezi mitatu angepona.

Anasema alifungwa mguu, baada ya miezi mitatu alipofunguliwa akaona hali iko vile vile, ndipo wakaanza kutafiti ili kujua ni nini shida?

“Ndipo tukaanza kwenda hospitali zingine hapa nchini, wakatuambia tukanunue kiatu fulani cha kuvaa nikanunua na kukivaa kwa miezi, lakini gharama yake siifahamu kwa sababu ilininunulia Yanga.

"Lakini hali haikubadilika na sikuwa naweza kufanya hata mazoezi wala kukimbia kwa miezi kama sita napata shida tu, ndipo wakafanya maamuzi ya kunipeleka Afrika Kusini.”

Mapinduzi anasema baada ya madaktari kumpima, ilikuwa ni tofauti kwa asilimia 100 na sehemu walizokuwa wanapita huku Tanzania, kwa sababu walimweleza kuwa anatakiwa kufanyiwa upasuaji, kitu ambacho mwanzo hakukifikiria. 

"Waliniambia nitafanyiwa upasuaji mkubwa, hivyo itabidi nikae miezi sita. Wakati huo natamani kucheza, niliombe muda wa kulifikiria hilo kwamba inakuaje hii miezi yote wakati nimeshakaa kipindi kama hicho nyuma, yote hiyo ni kutibu tu jeraha, hapo sijaanza kufanya mazoezi,” anasimulia.

Anasema kabla hajafanya maamuzi, kwa kuwa alishasema maisha yake ni mpira na amepata fursa Yanga wamejitolea kumtibu, kwa nini akatae.

“Nilitafakari nikaamua kukubali kwa sababu nilisitisha programu za matibabu, lakini nilikuwa naona Dah! Hii imekuaje tena kukaa mwaka mzima nje, huku mkataba wangu ulikuwa unaenda mwishoni, Yanga mkataba uliisha nikiwa mzima," anasema.


Familia

Mapinduzi anasema yupo karibu na familia yake hasa wazazi na mke wake, hivyo kwa pamoja waliungana kumtia moyo na kumsihi asikate tamaa.

Anasema alipoambiwa atafanyiwa upasuaji, watu wa kwanza kuwaambia ilikuwa wao kwanza.

"Wamekuwa watu wanaonisapoti mpaka sasa, kwa hiyo nikiwa nao karibu wananipa moyo. Mpaka sasa hivi wananiona nacheza, kwa hivyo kuna wakati ukiwa unaongea nao wanakwambia unaona ungekata tamaa ingekuaje, wakati sasa hivi umerudi na unacheza mpira," amesema.


Nilikuwa nalia mwenyewe

Akisimulia wakati wa majereha yake, Mapinduzi anasema alipata maumivu makali sana alipokuwa anaonekana jukwaani lakini hachezi hali iliyomfanya awe analia mwenyewe.

"Ni kweli nilikuwa nalia mwenyewe kwa sababu kuna hali hata wewe mtu wa kawaida, lazima unapitia mpaka wewe mwenyewe unakuwa na uchungu kwa sababu kuna kipindi niliumia pale Yanga, msimu wa kwanza ulivyokwisha halafu msimu wa pili ile Yanga Day nimekula suti na niko jukwaani.

"Ikatokea siku uwanjani kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, pale wenzangu wanabadilisha wanavaa jezi, mimi niko na suti napanda jukwaani, kwa hiyo iliniumiza kwamba msimu wa pili huu mashabiki wananiona nimevaa suti tu.

“Wakati wenzangu wako uwanjani wanacheza, iliniumiza sana hadi wenzangu walijihisi vibaya kwamba inakuaje hii, haiwezekani misimu miwili yote niko juu.”


Ukaribu na Injinia

Mapinduzi anasimulia kuwa kutoka katika Klabu ya Yanga aliyekuwa karibu naye kwa wakati ule alikuwa Enjinia Hersi Said, kwa sababu alikuwa amesimmamia sambamba na kiongozi mmoja aliyekuwa akiitwa Kaligo.

Pia alipewa kipaumbele sana kumsimamia na Bosi mwenyewe 'GSM' kwa sababu hata nilivyoenda Afrika Kusini, alifikia kwake usiku ule hivyo kutoa shukrani kwa viongozi wote waliokuwa pamoja naye kwani hakuna aliyekuwa mbali naye.

"Kwa hiyo viongozi wote walikuwa karibu yangu, nawashkuru sana na wakati wote mshahara wangu ulikuwa unaingia kama kawaida mpaka naondoka nilikuwa napata stahiki yangu vizuri tu,” anasema.

Mapinduzi anatoa wito juu ya ubora wa viwanja huku akiomba timu nyingi ziboreshe viwanja vya mazoezi kwa sababu sehemu ya mazoezi ndipo muda mwingi mchezaji anakua huko, kuliko hata katika siku za mechi ambazo ni chache.

"Mechi inaweza kuwa kwa wiki mara moja, lakini kiwanja cha mazoezi kila siku mchezaji anakuwepo na haipewi kipaumbele lakini ndio sehemu muhimu zaidi.”

Mapinduzi anahitimisha kwa kusema kuwa kwa timu za hapa nchini kutengeneza sehemu ya mazoezi zikawa bora ni suala la msingi, lakini pia TFF inatakiwa isimamie utekelezaji wa ujenzi wa viwanja vya mazoezi kuliko hata vya mechi.

Makala hii imeandikwa kwa msaada wa Taasisi ya Gates Foundation.