Simba ubingwa Shirikisho Afrika unawezekana

Muktasari:
- Mchezo huo utafanyika katika Uwanja wa Manispaa jijini Berkane, Morocco ambao Simba watakutana na wenyeji wao RS Berkane.
Jumamosi wiki hii, Mei 17, wawakilishi wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika, Simba wanatupa karata katika mechi ya kwanza ya hatua ya fainali ya mashindano hayo msimu huu.
Mchezo huo utafanyika katika Uwanja wa Manispaa jijini Berkane, Morocco ambao Simba watakutana na wenyeji wao RS Berkane.
Baada ya hapo timu hizo zitarudiana hapa Tanzania katika Uwanja wa Benjamin Mkapa siku ya Jumapili, Mei 25 ambapo mshindi qa mechi mbili baina yao ndio atatwaa ubingwa wa mashindano hayo yanayoshika nafasi ya pili kwa thamani kwenye mashindano ya klabu Afrika.
Ni jambo lililo wazi kwamba mechi hizo mbili za fainali dhidi ya RS Berkane sio nyepesi kwa Simba kutokana na ubora wa kitimu ambao wapinzani wao hao wamekuwa nao.
Unaweza kupima ubora wa Berkane katika mashindano hayo kwa kuangalia ufanisi wa kitimu au mchezaji mmoja mmoja kwa takwimu ambazo wanazo hadi wanatinga hatua ya fainali.
Berkane inashika nafasi ya pili kwa kuwa na wastani wa kufunga mabao mengi kwa mechi ambapo ina wastani wa bao 1.8 kwa mchezo huku ikiongoza kwa kuruhusu mabao machache ambapo ina wastani wa kuruhusu bao 0.2 kwa mechi.
Ndio timu inayoongoza kwa kucheza mechi nyingi kweye mashindano hayo bila kuruhusu bao (clean sheets) ambapo imefanya hivyo mara nane na inaongoza kwa kuondosha hatari nyingi kulinganisha na nyingine.
Ni timu ambayo ina uzoefu mkubwa wa mashindano hayo tena wa mechi za hatua za juu za Kombe la Shirikisho Afrika kwa vile imeshiriki mara nyingi na katika hizo, imetwaa taji mara mbili na mara mbili ilimaliza katika nafasi ya pili.
Hata hivyo pamoja na ubora na uzoefu wa RS Berkane, Simba haipaswi kuzicheza mechi hizo mbili kinyonge bali inatakiwa kuingia na imani ya kwamba inaweza kupata matokeo mazuri kwenye mechi hizo mbili za fainali na ikatwaa ubingwa.
Wahenga walisema hakuna linaloshindikana chini ya jua hivyo Simba inatakiwa kuzicheza mechi zake dhidi ya RS Berkane ikiamini inao uwezo na sababu ya kufanya vyema na kuleta heshima ya taji hapa nyumbani Tanzania.
Na watu wa kwanza ambao wanapaswa kutimiza hilo kwa Simba ni wachezaji ambao wanatakiwa kufanyia kazi vyema maelekezo ya benchi lao la ufundi katika dakika 180 watakazopambana na Berkane.
Wachezaji wa Simba wanapaswa kufanya hilo kwa kucheza kwa kujituma na kujitolea kuanzia filimbi ya kuanza mchezo hadi ya kumalizia itakapopulizwa.
Wanapaswa kuhakikisha wanakimbia kilomita nyingi ndani ya uwanja zaidi ya zile ambazo wachezaji wa Berkane watakimbia lakini pia wanapaswa kucheza kwa nidhamu kubwa ili wajiepushe na adhabu za kadi ambazo zitanufaisha wapinzani wao kwa kuwapa mapigo ya adhabu kubwa au ndogo au wachezaji wa Simba kuonyeshwa kadi zinazoweza kuwagharimu.
Muda wote ndani ya uwanja wanatakiwa kufuata vyema na kwa usahihi wa hali ya juu, maelekezo ya kimbinu ambayo watapatiwa na benchi lao la ufundi kwa kuzingatia tathmini ya ubora na udhaifu wa wapinzani wao.
Kunaweza kufanyika maandalizi makubwa nje ya uwanja kwa maana ya hamasa ya fedha na mashabiki kujaa uwanjani lakini kama wachezaji wakishindwa kutimiza vyema kile wanachohitajika kukifanya ndani ya kiwanja, itakuwa ni kazi bure.
Hatua ya fainali sio rahisi kufika na inawezekana kikosi cha sasa cha Simba kikashindwa kutinga tena kwa miaka ya hivi karibuni hivyo wachezaji wanatakiwa kuitumia vyema fursa iliyopo mkononi mwao kutwaa taji ili waingie katika vitabu vya kihistoria ndani na nje ya klabu hiyo.
Kwa upande wa benchi la ufundi, linapaswa kuandaa mbinu na mipango bora kwa ajili ya mchezo huo na kuwaelekeza wachezaji namna bora ya kufanyia kazi ndani ya uwanja ili waweze kuzalisha kilicho bora kwenye hatua ya fainali.
Pamoja na kwamba RS Berkane inapewa nafasi kubwa kwenye makaratasi kutwaa taji hilo msimu huu, Simba inayo nafasi tena kubwa ya kuishangaza timu hiyo ya Morocco na soka la Afrika kiujumla kwa kupata ushindi na kuchukua ubingwa wa kombe hilo.
Iko mifano mingi ya timu ambazo ziliingia fainali zikiwa hazipewi nafasi kubwa ya kuchukua Kombe lakini mwisho wa siku zilifanikiwa kuondoka na taji na kuziacha kwenye mshangao zile ambazo zilionekana kama zingetwaa kiurahisi.
Mfano ni Ugiriki ambayo ilitwaa taji la mashindano ya Mafaifa y Ulaya mwaka 2004 ikiwa haina kikosi chenye mastaa kulinganisha na kile cha Ureno ambayo kilicheza nacho fainali.