Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Prisons yainyuka Coastal, yaiweka pabaya Kagera 

PRISONS Pict

Muktasari:

  • Ushindi kwa Prisons unaipa presha kubwa Kagera Sugar katika vita ya kujinasua na aibu ya kushuka daraja, ambapo kwa sasa Maafande hao wanazo dakika 180 za kujiuliza dhidi ya Yanga na Singida BS kumaliza msimu.

Ushindi wa mabao 2-1 iliyopata Tanzania Prisons dhidi ya Coastal Union unaiweka katika presha kubwa Kagera Sugar ambayo baadaye itakuwa kibaruani mbele ya Mashujaa.

Hii ni kutokana na vita ya kukwepa kushuka daraja baada ya KenGold kutangulia mapema na kuziachia msala timu zilizopo juu yake katika msimamo kila mmoja kujipambania kivyake kubaki salama Ligi Kuu msimu ujao.

Prisons ambayo haikuwa na mwanzo mzuri msimu huu, ushindi wa leo dhidi ya Wagosi wa Kaya unaiweka nafasi ya 11 ikifikisha pointi 30 na sasa watasubiri mechi mbili zilizobaki dhidi ya Yanga na Singida Black Stars kujua hatma yao.

Timu hiyo inaendeleza ushindi katika mchezo wa nne mfululizo ikianza dhidi ya Kagera Sugar 1-0, KenGold 3-1, ikashinda 3-2 dhidi ya JKT Tanzania na leo imetakata kwa ushindi huo.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Maafande hao walianza kucheka na nyavu dakika ya 28 kupitia kwa Ezekiel Mwashilindi aliyefunga kwa mpira wa friikikii na kudumu hadi mapumziko.

Coastal ilionyesha uimara na kutengeneza mashambulizi kadhaa lakini beki ya Prisons chini ya nahodha, Jumanne Elfadhir ilikuwa imara kudhibiti hatari, huku kipa  Sebusebu Samson akifanya kazi ya ziada.

Beno Ngassa hakuwa nyuma kuwainua tena mashabiki wa Prisons kwa kuiandikia bao la pili dakika ya 74 na kuihakikishia timu hiyo pointi tatu ikifufua zaidi matumaini ya kubaki salama Ligi Kuu.

Dakika ya 90, Coastal Union ilipata bao kupitia kwa Bakari Suleiman na kuibakiza timu hiyo nafasi ya nane kwa pointi 31 ikisaliwa na mechi mbili kuhitimisha msimu.

Hata hivyo, matokeo ya Wajelajela hao yanaiweka mtegoni Kagera ambao saa 1:30 usiku itakuwa kazini Kaitaba, mjini Bukoba kuikaribisha Mashujaa ambapo matokeo ya sare au kupoteza yataishusha rasmi daraja.

Kagera iliyodumu Ligi Kuu kwa miaka 21 tangu walipopanda 2004, wapo nafasi ya 15 kwa pointi 22 ambapo kocha Juma Kaseja atakuwa na dakika 90 za presha kuivusha au kuiangusha timu hiyo.

Kocha wa Coastal, Joseph Lazaro amesema pamoja na kupoteza mechi hiyo, lakini hawajapoteza muelekeo akikiri hadi sasa timu nyingi hazijawa salama sana kujihakikishia kubaki Ligi Kuu.

"Tunaenda kusahihisha makosa mechi zijazo kuhakikisha tunakuwa salama hadi mwisho wa msimu, lakini kwa ujumla Ligi ni ngumu tangu mwanzo hadi sasa," amesema Lazaro.

Kocha wa Prisons, Aman Josiah amesema hadi sasa ushindi huo wamejihakikishia kucheza play off, lakini kwa mechi mbili zilizobaki ni kufa na kupona kutafuta pointi sita ili kujiondoa kwenye mchujo.

"Kama tumeshinda mechi nne mfululizo itakuwaje kushindwa pointi sita zilizobaki, kimsingi nimepunguza presha kwa wachezaji na matokeo haya ni mafanikio ya mazoezi yetu,"  amesema Josiah.