Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kisa Yanga, Simba yaweka mzigo mezani

Muktasari:

  • Simba ambayo leo, Jumapili inakabiliana na KMC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara, tayari imeshuka dimbani mara 25, ikishinda 23, sare tatu na kupoteza mechi moja ikiachwa pointi nne na Yanga inayoongoza msimamo.

VITA iliyopo hivi sasa kati ya Simba na Yanga katika Ligi Kuu Bara imemfanya kigogo mmoja wa Wekundu wa Msimbazi kuweka mzigo mezani kuhakikisha timu yao inafikia malengo.

Simba ambayo leo, Jumapili inakabiliana na KMC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara, tayari imeshuka dimbani mara 25, ikishinda 23, sare tatu na kupoteza mechi moja ikiachwa pointi nne na Yanga inayoongoza msimamo.

Katika ligi hiyo, mbali na kuwania ubingwa, pia kuna vita ya kusaka tuzo ya Ufungaji Bora inayowahusu Jean Charles Ahoua na Leonel Ateba wa Simba wanaoshindana na nyota wa Yanga, Clement Mzize na Prince Dube, pia kuna ile ya Clean Sheet, Moussa Camara wa Simba na Djigui Diarra wa Yanga.

Simba ambayo katika mechi 25 imefunga mabao 60 ikizidiwa na Yanga manane pekee, imekuja na mpango wa kununua kila bao litakalofungwa kuanzia sasa.

Mchakato huo wa kununua mabao ulikuwa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na Simba imetinga fainali, lakini sasa hadi Ligi Kuu kuna mzigo umewekwa.

Akizungumza na Mwanaspoti, bosi wa zamani wa Simba, Azim Dewji alisema ishu ya kununua mabao kwa sasa siyo kwenye mechi za kimataifa pekee, bali wamehamishia pia nguvu Ligi Kuu lengo likiwa ni kuongeza morali ya kupambania mafanikio ya timu.

Bosi huyo alisema motisha hiyo itawafanya nyota wa kikosi hicho akiwemo Jean Cherles Ahoua na Leonel Ateba kuiongoza vizuri safu ya ushambuliaji kupambana ili kuipiku Yanga.

“Kila bao nalinunua Sh500,000. Nimeamua kufanya hivi ili timu ifunge mabao mengi kupunguza tofauti yetu na Yanga. Pia washambuliaji wapambane katika kuwania Tuzo ya Ufungaji Bora dhidi ya kina Mzize (Clement) na Dube (Prince). Kiukweli nafurahia sana ninapoona tunafunga mabao mengi,” alisema Dewji na kuongeza:

“Ligi hivi sasa ina ushindani na Simba ni timu kubwa yenye wachezaji wenye ubora, hivyo uongozi na mashabiki hawapendelei kuona tunapata matokeo yasiyoridhisha. Nafurahia kuona mabao mengi yanafungwa na sina shida. Ninachotaka wafunge hata mabao 10 kwani pesa zipo, ni wao tu kujituma.”

VITA IKO HAPA

Kwa sasa Ahoua anaongoza kwa ufungaji akiwa na mabao 15 akifuatiwa Clement Mzize (13), huku Prince Dube na Leonel Ateba waliofunga 12 kila mmoja wakishika nafasi ya tatu.

Nyota hao kwa mechi zilizobaki zinaongeza ushindani katika kuwania Tuzo ya Ufungaji Bora inayoshikiliwa na kiungo wa Yanga, Stephane Aziz Ki ambaye alimaliza msimu uliopita akiwa na mabao 21.

Wakati mastaa hao wakipambania tuzo hiyo, pia wana jukumu la kuzisaidia timu wanazozitumikia kuwania taji la Ligi Kuu Bara ambalo Yanga inalitetea ikilichukua kwa misimu mitatu mfululizo, huku Simba ikilifukuzia tangu mara ya mwisho ilipolibeba 2020-2021.

Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, Yanga inaongoza ikiwa na pointi 70 ikishinda mechi 23 kati ya 26, sare moja na kupoteza mbili, ikifunga mabao 68 na kuruhusu 10. Simba katika mechi 25 imeshinda 21, sare tatu na kupoteza moja ikikusanya pointi 66, ikifunga mabao 60 na kuruhusu 10.


SIMBA REKODI MPYA

Achana na rekodi ya Fadlu Davids aliyoiandika hivi karibuni kwa kuifikisha Simba fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya takriban miaka 32, ishu mpya ni kwamba kikosi hicho kimecheza mechi 19 mfululizo za ligi bila kupoteza.

Wakati Fadlu anaweka rekodi hiyo, tayari Yanga imeongozwa na makocha wanne ambao ni Miguel Gamondi, Sead Ramovic, Abdihamid Moallin na Miloud Hamdi, na imeshuhudiwa timu hiyo ikicheza mechi 16 mfululizo za ligi bila kupoteza. Imeshinda 15 na sare moja, wakati Simba ikishinda 17 na sare mbili.

Tangu mara ya mwisho Yanga ifungwe 3-1 na Tabora United, Novemba 7, 2024, ikiwa ndiyo mechi ya mwisho kwa Gamondi kikosini hapo, timu hiyo mechi sita zilizofuatia ilifundishwa na Ramovic ikishinda zote, kisha Hamdi ameiongoza mechi tisa ikishinda nane na sare moja. Mechi moja iliongozwa kwa muda na Moallin ambayo timu hiyo ilishinda pia.

Mara ya mwisho Simba kupoteza ilikuwa Oktoba 19, 2024 kwa bao 1-0 dhidi ya Yanga, lakini baada ya hapo Fadlu amekuwa akiendeleza furaha kwa mashabiki wa timu hiyo.

Simba katika mechi 19, 10 ni za ugenini na imeshinda nane na sare moja wakati za nyumbani ikishinda nane na sare moja. Fadlu hadi sasa ameiongoza Simba kwenye mechi 25 za ligi, ikishinda 21, sare tatu na kupoteza moja.

Akizungumzia hilo, Fadlu alisema rekodi zipo ili kuwekwa na kuvunjwa na kwa upande wake anapambana Simba ifikie malengo kwa kutwaa taji la Kombe la Shirikisho Afrika.

“Ni mafanikio, lakini bado sijafikia malengo. Natamani kuwa na rekodi ya peke yangu kwa kutwaa taji la Afrika na siyo kufikia rekodi ya mtu mwingine. Nina nafasi ya kufanya hivyo na naamini itakuwa bora zaidi kwangu,” alisema Fadlu ambaye ameifikisha Simba fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.Pia hivi karibuni ameshinda Kombe la Muungano baada ya kuifunga JKU bao 1-0, huku akiifikisha Yanga nusu fainali ya Kombe la FA.