Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vita ya usajili 2025/26 inaanzia hapa

USAJILI Pict

Muktasari:

  • Eneo la mkiani, baada ya KenGold kushuka daraja mapema, imeziachia msala Kagera Sugar, Pamba Jiji na Tanzania Prisons zenye pointi zisizozidi 27, lakini hata zilizopo juu yao kama Fountain Gate, KMC, Mashujaa, Namungo, Coastal Union na JKT Tanzania bado hazipo pia salama kwa sasa.

LIGI Kuu Bara ipo ukingoni kwa sasa ikiwa imesaliwa na mechi za raundi tatu kabla ya msimu kufikia tamati Juni 22, huku mbio za ubingwa zikisalia kwa vigogo Simba na Yanga tu, ilihali Azam FC na Singida Black Stars zikichuana kuwania nafasi ya tatu inayotoa tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Eneo la mkiani, baada ya KenGold kushuka daraja mapema, imeziachia msala Kagera Sugar, Pamba Jiji na Tanzania Prisons zenye pointi zisizozidi 27, lakini hata zilizopo juu yao kama Fountain Gate, KMC, Mashujaa, Namungo, Coastal Union na JKT Tanzania bado hazipo pia salama kwa sasa.

Timu hizo zenye pointi kati ya 29 hadi 32 bado zinaweza kuangukia katika play off kama hazitatumia vyema mechi tatu zilizosalia mikononi mwao kujiweka salama, hii ikiwa ni tofauti na Dodoma Jiji, Tabora United, Singida na Azam zilizopo ndani ya Sita Bora kwa pointi zilizonazo hadi sasa.

Hata hivyo, wakati ligi ikiwa inaenda ukingoni, pia kuna baadhi ya mastaa wa timu hizo za Ligi Kuu nao mikataba yao ipo mwishoni, jambo linalotoa nafasi kwa klabu nyingine zenye fedha kujitosa kuwabeba kama zinawahitaji huku zinazowamiliki zikiwa na kazi ya kuwabakisha.

Vigogo Simba, Yanga na Azam wote wana mastaa tegemeo ambao mikataba yao inaisha mwisho wa msimu huu, hivyo kuwapa presha mabosi wanaopambana kuwabakisha kwa kuanza mazungumzo ya kuwaongezea mikataba baadhi yao wakiwa wameanza kufanikisha dili za kubaki nao kwa msimu ujao.

Mwanaspoti linakuletea orodha ya wachezaji ambao mwishoni mwa msimu huu watakuwa sokoni na wenye fedha zao wanaweza kujibebea kiulaini na klabu zitakazotaka kuwabakisha ni lazima zijipange kwa kuvunja benki la sivyo itakula kwao.

USA 01

AISHI MANULA (SIMBA)

Amepoteza namba Simba kwa msimu wa pili sasa tangu alipoumia na hasa baada ya kusajiliwa kwa Ayoub Lakred ambaye pia majeraha yamemuondoa kikosini na nafasi yake ikichukuliwa kikamilifu na Mousa Camara ambaye amekuwa kipa namba moja wa kikosi hicho.

Alikuwa kipa namba moja wa Simba na timu ya Taifa, Taifa Stars. Alijiunga na Simba akitokea Azam FC 2017/18 na katika msimu wa kwanza tu, aliiwezesha timu hiyo kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya kuusotea kwa miaka sita. Ameipa timu hiyo mataji ya ligi mara nne mfululizo huku akiipeleka Simba hatua ya robo fainali mara tano katika misimu sita kwenye michuano ya kimataifa.

Licha ya mkataba wake kwenda ukingoni amepoteza namba kabisa kwenye kikosi cha timu hiyo kiasi cha kukosa nafasi hata ya kukaa benchini. Mwanaspoti limejiridhisha kwamba anatemwa.

USA 02

SHOMARI KAPOMBE (SIMBA)

Panga pangua katika Simba na Taifa Stars, Kapombe hakosekani katika kikosi cha kwanza kutokana na uwezo pamoja na kuwa na akili ya soka. Amekuwa msaada kwa timu yake.

Kapombe alijiunga na Simba akitokea Azam ambako aliondoka akiwa ameifungia mabao manane katika msimu wake wa mwisho kwa Wanalambalamba. Licha ya kuwa miongoni mwa wachezaji waliocheza kwa dakika nyingi Msimbazi, mkataba alionao upo ukingoni na ana uhuru wa kuzungumza na timu yoyote inayomtaka.

Ni msimu wa pili mfululizo sasa beki huyo amekuwa akiongezewa mkataba katika dakika za jioni, ilitokea hivyo pia msimu uliopita akiongezwa mkataba wa mwaka mmoja sasa anawarudisha tena mezani mabosi wa timu hiyo kwaajili ya mazungumzo mapya.

Beki huyo ni miongoni mwa wachezaji walioipa Simba mafanikio misimu minne mfululizo wakitwaa taji la ligi, kuifikisha robo fainali sita za CAF katika miaka saba ikiwamo na fainali ya Kombe la Shirikisho 2024-25, ambapo Simba itacheza dhidi ya RS Berkane ya Morocco. Katika ligi msimu huu, amefunga mabao matatu na asisti tatu.

USA 03

MOHAMMED HUSSEIN 'TSHABALALA' (SIMBA)

Ufundi wake haupishani na Kapombe, ni beki mwenye kasi ya kushambulia na ana jicho la kuona lango, akiwa amejiunga na Wekundu hao wa Msimbazi akitokea Kagera Sugar. Ndiye mchezaji aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi bila kutoka ndani ya timu hiyo kwa sasa, huu ukiwa ni msimu wake wa 10 sasa Msimbazi.

Tshabalala ndiye nahodha wa timu hiyo akipokea kitambaa kutoka kwa mkongwe John Bocco ambaye ametimka ndani ya kikosi hicho akicheza JKT Tanzania. Beki huyu ni panga pangua wa kikosi cha Simba na katika timu ya taifa, Taifa Stars.

Beki huyo ambaye amecheza kwa ubora misimu yote 10 tangu amejiunga na Simba amewaweka matajiri wa timu hiyo kwenye nyakati ngumu kumuongeza mkataba mpya kutokana na ofa nyingi zilizo mbele yake ndani na nje kinachosubiriwa sasa ni uamuzi wake wa mwisho wa msimu ataendelea kubaki Simba au ataenda kujaribu maisha mengine nje ya timu hiyo.

Tshabalala licha ya kuongezewa nguvu Simba wakinasa saini ya Valentin Nouma bado ameendelea kucheza kikosi cha kwanza akimuachia dakika chache beki mpya huyo. Tshabalala ana mabao mawili na asisti nne kwenye ligi msimu huu.

USA 04

FABRICE NGOMA (SIMBA)

N muhimu kwenye kikosi cha kwanza cha Simba eneo la kiungo cha ulinzi amekuwa imara eneo hilo tangu ajiunge na Simba msimu uliopita akichukua nafasi ya Sadio Kanoute ambaye aliachana na Simba baada ya mkataba wake kuisha.

Anatajwa kama moja ya viungo bora wa ukabaji, kazi yake uwanjani inambeba na ni miongoni mwa wachezaji ambao mkataba wake unaelekea ukingoni hivyo kama kuna mtu mwenye fedha zake anaweza kumnasa kiulaini.

Ngoma tangu amejiunga na Simba msimu ulioisha ameliongoza eneo hilo la kiungo cha ulinzi akianza kucheza na mzawa Mzamiru Yassin, Debora Fernandes na sasa ametengeneza pacha nzuri na Yusuf Kagoma, msimu huu ameifungia timu hiyo mabao mawili.

USA 05

MAXI NZENGELI (YANGA)

Kiraka ni mchezaji ambaye anaweza kucheza namba nyingi uwanjani na akaweza kuzitendea haki, pia ni mchezaji anayecheza mara nyingi zaidi winga zote mbili na ni tegemeo kikosini mwa timu hiyo ameweza kupenya mbele ya makocha watatu walioinoa Yanga kwa misimu miwili tofauti.

Nzengeli msimu huu hajacheza mechi nyingi kama ilivyokuwa msimu uliopita chini ya Miguel Gamondi akiwa ndiye mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi, msimu huu ameanza vibaya baada ya kupata majeraha amerejea na kuendelea alipoishia hadi sasa ameifungia Yanga mabao matano huku akitoa pasi za mwisho zilizozaa mabao 'Asisti' saba.

Kiungo huyo mshambuliaji licha ya kuto kuzungumzwa sana kwa ubora kama ilivyo kwa wachezaji wengine amekuwa msaada mkubwa ndani ya kikosi cha Yanga akiwanyima nafasi ya kucheza wazawa Farid Mussa, Denis Nkane ambao wanacheza eneo hilo. Hata hivyo inaelezwa Yanga imemalizana naye mapema ili kuhakikisha mwamba huyo anasalia kikosini.

USA 06

KHALID AUCHO (YANGA)

Sio Yanga tu ni kiungo tishio katika kikosi chake cha timu ya taifa Uganda akivaa kitambaa cha unahodha, Aucho ni kiungo bora wa ukabaji ndani ya Yanga kwa sasa kutokana na umiliki wake wa mpira awapo uwanjani na namna ya utoaji pasi amekuwa na uchezaji mzuri na ni kipenzi cha mashabiki.

Tangu amejiunga na Yanga ukiwa ni msimu wake wa tatu amekuwa kiungo namba moja na mchezaji wa kutumainiwa eneo hilo ambalo amekuwa akicheza na Mudathir Yahya na Duke Abuya wote wamekuwa wakipeana nafasi.

Hata hivyo, nyota huyu wa kimataifa wa Uganda, ufundi bado upo na ubongo wake amekuwa mhimili mkubwa katika kikosi cha Yanga tangu alipojiunga na timu hiyo msimu wa 2021/22 akitokea Misr Lel Makkasa SC ya Misri, licha ya kuonekana umri unasonga.

USA 07

PACOME ZOUZOUA (YANGA)

Kiungo fundi hivyo ndio anavyoitwa na mashabiki wa timu yake kutokana na ufundi alionao na ndio kipenzi cha mashabiki wa Jangwani naye mkataba wake unaelekea mwishoni, timu yoyote ikimtaka inamnasa kiulaini kwa sasa.

Ni msimu wake wa pili ndani ya kikosi cha Yanga alijiunga na timu hiyo msimu uliopita hadi sasa amepachika mabao saba kambani sawa na msimu uliopita ambapo pia aliingia kambani mara saba amebakiza mechi saba kuvuka rekodi yake mwenyewe na kumaliza mkataba wa kuendelea kuiitumikia timu hiyo.

Ukiondoa idadi hiyo ya mabao aliyoyafunga Zouzoua ndiye kinara wa kutoa pasi za mwisho zilizozaa mabao hadi sasa kwenye mechi 24 walizocheza amechangia mabao nane na kinara Feisal Salum 'Fei Toto' ambaye ametoa asisti 12. Inaelezwa huyu naye ameshamalizana na mabosi wa Yanga na huenda akasaini muda wowote.

USA 08

DICKSON JOB (YANGA)

Ndiye nahodha msaidizi wa Yanga akichukua kitambaa kutoka kwa Bakari Mwamnyeto ambaye amekuwa akikalia mbao tangu waongezwe kikosini Job na Ibrahim Abdallah 'Bacca' ambao wametengeneza pacha nzuri kikosini humo lakini pia timu ya taifa, Taifa Stars.

Ligi Kuu Bara ikimalizika msimu huu utakuwa msimu wa nne wa Job kukipiga Yanga na kutokana na mchango wake kwenye timu, imeelezwa anahitaji kuboreshewa maslahi yake yatakayofanya apotezee ofa ya Simba ambao wanaelezwa kuwa wapo siriazi sana na beki huyo wa Taifa Stars, akiwa chaguo la kwanza la kocha chini ya makocha wanne waliopita Yanga akianza na Nasreddine Nabi, Miguel Gamondi, Sead na sasa Miloud Hamdi.

Mchezaji huyo aliyejiunga na Yanga 2021 akitokea Mtibwa Sugar anamalizia msimu wa nne baada ya mitatu kucheza kwa mafanikio akitwaa mataji ya Ligi Kuu, Ngao ya Jamii na Kombe la Shirikisho na kuvaa medali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya timu hiyo kucheza fainali.

USA 09

JONAS MKUDE

Mkude aliyesajiliwa Yanga msimu uliopita baada ya kumaliza mkataba Simba aliyoitumikia kwa mafanikio, akiwa Yanga ametwaa taji moja na yupo pamoja na timu hiyo kusaka taji la pili kwake lakini ni la nne kwa timu hiyo mfululizo japo hana uhakika wa namba.

Katika msimu wa kwanza, Mkude aliitumikia Yanga mechi 10 tu akicheza jumla ya dakika 300, tofauti na hali ilivyo msimu huu ambapo amechezeshwa mechi mbili akitumia dakika 26 katika Ligi Kuu na kuzua maneno kwamba huenda asiwe sehemu ya kikosi msimu ujao kwani anaoshindana nao katika eneo la kiungo wamemzidi kiasi cha kumnyima nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Kwa msimu huu Khalid Aucho ndiye mwenye namba ya uhakika kikosini kacheza mechi 20, dakika 1548, amefunga bao moja katika ushindi wa Yanga wa 5-0 dhidi ya Mashujaa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma wakati Duke Abuya kacheza mechi 22, dakika 1184, kafunga mabao mawili na asisti mbili, jambo linaloendelea kufinya nafasi ya Mkude kupata namba.

Kiungo huyo ni msimu wake wa mwiosho ndani ya kikosi cha timu hiyo mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu nini kitamfanya abaki ndani ya timu hiyo ambayo pia inamalizana na Aucho ambaye mkataba wake pia upo ukingoni.

USA 10

CLATOUS CHAMA

Licha ya kutabiriwa makubwa mwanzoni mwa msimu huu akijiunga na Yanga akitokea Simba, Chama hana maisha mazuri ndani ya timu hiyo kutokana na kukosa namba kikosi cha kwanza ameitumikia Yanga kwa dakika 727 akicheza mechi 24 kati ya 26 za ligi walizocheza.

Chama ambaye anacheza namba moja sambamba na Pacome, Stephane Aziz Ki ameshindwa kupenya kikosi cha kwanza kwenye michezo 31 ya mashindano yote aliyocheza amefunga mabao sita na kutoa asisti tisa hivyo amehusika kwenye mabao 16 kati ya 68 yaliyofungwa na timu hiyo.

Kiungo huyo anasaka taji la nne msimu huu baada ya kubeba matatu akiwa Simba ndiye mwenye rekodi ya kutengeneza mabao mengi zaidi msimu mmoja ndani ya misimu kumi ya hivi karibuni akifanya hivyo msimu wa 2021/22 alipotoa asisti 15.

USA 12

MUDATHIR YAHYA

Wakati akisajiliwa Yanga katika dirisha dogo la usajili, Mudathir Yahya hakuonekana kama angeweza kupenya ndani ya kikosi cha kwanza cha timu hiyo.Kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu baada ya kuachana na Azam FC ilikuwa ilitajwa kuwa sababu.

Uwepo wa nyota wa safu ya kiungo ambao walikuwa wanafanya vizuri katika kikosi cha Yanga wakati Mudathir anasajiliwa kina Khalid Aucho, Stephane Aziz Ki, Yannick Bangala na Salum Abubakar 'Sure Boy' ulionekana ungekuwa kikwazo kwa kiungo huyo wa Taifa Stars kupata nafasi kikosi cha kwanza.

Hata hivyo, mambo yamekuwa tofauti na Mudathir ndio ameonekana kujihakikishia nafasi kikosi cha Yanga akianza chini ya kocha Nasreddine Nabi ambaye alimtumia kikosi cha kwanza hadi alipoondoka chini ya Miguel Gamondi mambo yaliendelea kuwa mazuri kwake hadi sasa wakipita makocha wanne ameweza kuimiri ushindani.

Ni msimu wake wa mwisho ndani ya kikosi hicho tayari ametwaa mataji ya ligi, kombe la Shirikisho FA na kuvaa medari ya CAF akiisaidia timu hiyo kucheza fainali Kombe la Shirikisho Afrika. Kwa sasa inatajwa kunyemelewa na Azam, huku mabosi wa Yanga wakianzisha mazungumzo naye kumbakisha.

USA 13

YAO KOUASSI

Msimu wa kwanza ndani ya Yanga alivunja ufalme wa Kibwana Shomari akimuweka nje ya uwanja licha ya kuwa nyota wa kikosi cha kwanza akitwaa mataji mawili mfululizo ujio wake ulikuwa mwiba kutokana na ubora aliouonyesha.

Lakini majeraha aliyoyapata mwanzoni mwa msimu huu yamefuta ubora wak na kusahaulika kabisa huku yanga ikiongeza nguvu eneo hilo kwa kumsajili Israel Mwenda ambaye tayari ameanza kuonyesha makali yake akifunga mabao mawili msimu huu baada ya kuingia dirisha dogo.

Yao inaelezwa hatakuwa sehemu ya kikosi hadi mwisho wa msimu na mkataba wake unamaliza msimu huu swali ni je? uongozi wa timum hiyo utamuongeza mkataba au itamuacha akajaribu maisha nje ya timu yao.

Yao aliyekuwa nje ya uwanja kwa miezi mitatu kutokana na kuumia nyama za paja, alianza mazoezi na wenzake, lakiniamejitonesha na kumfanya aendelee kukosekana uwanjani, huku ikielezwa kwa mechi zilizosalia za kufungia msimu sio rahisi kuziwahi tena, hivyo ni hadi msimu ujao.

Beki huyo raia wa Ivory Coast amekuwa akiandamwa na majeraha tangu kuanza kwa msimu huu na kumfanya atumike katika mechi saba kati ya 26 za Ligi Kuu ilizocheza timu hiyo inayoongoza msimamo, ambapo pengo lake limezibwa na Mwenda aliyeingia dirisha dogo na wakati mwingine Kibwana Shomari.

Kibwana hadi sasa ametumika katika mechi saba kati ya 25 akitumia dakika 533 akiwa na asisti moja, wakati Mwenda amecheza mechi nane akitumia dakika 675 na kufunga mabao mawili bila ya kuwa na asisti yoyote.


AZAM FC

Matajiri hao wa Chamazi, waliokuwa na msimu mbaya kwa kung'olewa mapema katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho (FA), kwa sasa inawania kumaliza nafasi ya tatu ijihakikishe tiketi ya CAF kwa msimu ujao, wachezaji walio mbioni kumaliza mkataba ni pamoja na kiungo mshambuliaji kutoka Gambia, Gibril Sillah, washambuliaji Adam Adam anayecheza kwa mkopo Tanzania Prisons na Alassane Diao, sambamba na  Idd Seleman 'Nado'.


TABORA UNITED

Nyuki hawa wa Tabora ambao msimu huu walianza na moto kabla ya kuyumba hivi karibuni kwa kupoteza mechi mfululizo, ina orodha ndefu ya mastaa wanaomaliza mikataba akiwamo washambuliaji waliotengeneza pacha ya hatari, waliowahi kukipiga pia Yanga, Yacoub Songne na Heritier Makambo.

Pia wamo Andy Bikoko, Kelvin Pemba, Ibrahim Hamad 'Hilika', Yassin Mustafa, Banele Sikhondze, Shedrack Asiegbu, Emmanuel Chigozie, Moses Msukanywele, Abdallah Seseme, Shafii Maulid, Omary Yusuf na Nelson Munganga.


KENGOLD

Kikosi hiki kilichopanda daraja msimu huu kisha kushuka kwa kuvuna pointi chache kuliko zote hadi sasa katika Ligi Kuu, asilimia kubwa ya nyota walioingia dirisha dogo na wengine walioanza msimu na timu hiyo wanamaliza mikataba yao na timu yoyote inayowahitaji wanaweza kuwavizia tu.

Wachezaji hao wa KenGold wanaomaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu huu ni, Sadala Lipangile, Abdallah Nassir, Mathias Juviliani, Bernard Morrison, Kelvin Yondani, Lassa Gradi Kiala, Erick Kabamba, Stephen Duah, Nassir Bofu, Abdullah Abdul, Fredrick Kalabunga, Selemani Bwenzi, Masoud Abdallah 'Cabaye', Joshua Ibrahim.


NAMUNGO

Wachezaji wanaomaliza mikataba ndani ya klabu ya Namungo inayojiandaa kutua Dar es Salaam ili kukabiliana na Yanga katika mechi ya Ligi Kuu Bara, ni pamoja na wakongwe Meddie Kagere na Erasto Nyoni waliotua klabuni hapo misimu miwili iliyopita wakitokea Simba.

Wengine ni Khamis Halifa 'Nyenye', Hashim Manyanya, Lucas Chalambwiga, Hamis Mgunya, Hassan Kibailo, Eric Kapaita, Eric Molongi, Jonathan Nahimana, Derick Mukombozi na Hassan Kabunda.


KMC FC

Kwa kikosi cha KMC hadi sasa orodha ambayo Mwanaspoti imepenyezewa ni beki Rahim Shomary, kiungo mshambuliaji Ibrahim Elias 'Mao', makipa Wilbol Maseke na Ismail Mpank pamoja na Ally Shabani Valentine.


FOUNTAIN GATE FC

Kwa upande wa Fountain Gate inayoshika nafasi ya 12 katika msimamo wa Ligi Kuu nyota wanaomaliza mikataba ni John Noble, Kassim Haruna 'Tiote', Edgar William, Olawale Oremade, Lawrence Luvanda, Said Mbatty.


PAMBA JIJI FC

Wababe hao wa zamani wa soka la Tanzania, waliorejea katika Ligi Kuu msimu huu baada ya msoto wa miaka 23, Pamba Jiji wachezaji wanaomaliza mikataba ni; Frank Ng'amba, Ben Nakibinge, Eric Okutu, Yunus Lema, Ally Ramadhan 'Oviedo', Samson Madeleke, James Mwashinga, Deus Kaseke, Abalkassim Suleiman na Habib Kyombo.


COASTAL UNION

Wagosi wa Kaya na Mabingwa wa Ligi Kuu Bara 1988, wachezaji wanaomaliza mikataba ni Salum Aiyee, Aaron Kalambo, Mbaraka Yusuph, Lameck Lawi na Mgaya Ally, huku ikielezwa baadhi yao akiwamo Lawi wameanza kuzungumza ili kuwaongezea.


MASHUJAA FC

Maafande hao wanaoshiriki Ligi Kuu kwa msimu wa pili sasa, wachezaji wanaomaliza mikataba ni pamoja na Ally Nassoro 'Ufudu', Yusuph Dunia, Jaffary Kibaya, Abdulmalik Zakaria, Crispin Ngushi, Seif Karihe.


KAGERA SUGAR

Wana Nkurukumbi wanaopambana kujiokoa wasishuke daraja, Kagera Sugar inayonolewa na kiap wa zamani wa kimataifa, Juma Kaseja, baadhi ya wachezaji wanaomaliza mikataba ni pamoja na Nassoro Kapama, Samwel Onditi, Omary Chibada. Tariq Seif,  na Abdallah Mfuko.


SINGIDA BS

Kwa upande wa Singida Black Stars inayopambana kumaliza nafasi ya tatu ikichuana na Azam n ikiwa pia ipo nusu fainali ya Kombe la FA wachezaji wanaomaliza mikataba ni pamoja na Metacha Mnata, Morice Chukwu, Farie Ondongo na Marouf Tchakei,


TZ PRISONS

Kwa maafande hao w Magereza wanaopambana kujiokoa wasishuke daraja baadhi ya mastaa ambao mikataba yao ipo ukingoni ni Bebno Ngassa, Samsom Mwaituka, Marco Mhilu na Mussa Haji.


JKT TANZANIA

Maafande hao wa JKT Tanzania iliyopo nafasi ya saba katika Ligi Kuu wachezaji wanaomaliza mikataba ni John Bocco, Matheo Antony na Ally Msengi anayecheza kwa mkopo kutoka Tanzania Prisons.


DODOMA JIJI

Walima zabibu wa Dodoma Jiji, wenyewe wamekuwa na usiri wa nyota wanaomaliza miakataba, lakini jina pekee lililotua mezani mwa Mwanaspoti ni beki Jerom Mgeveke.