Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MINZIRO: Hiki ndicho kinaua timu ndogo

Muktasari:

  • Hata hivyo, usajili mbovu iwe ni kwa kuchukua wachezaji wasiokidhi viwango, gharama kubwa au kutokuwa na mipango ya muda mrefu huwa na athari kubwa kwa timu ndogo.

KATIKA ulimwengu wa soka usajili wa wachezaji ni miongoni mwa vipengele muhimu vinavyoamua mafanikio ya timu au kufeli.

Hata hivyo, usajili mbovu iwe ni kwa kuchukua wachezaji wasiokidhi viwango, gharama kubwa au kutokuwa na mipango ya muda mrefu huwa na athari kubwa kwa timu ndogo.

Timu kubwa mara nyingi huwa na uwezo wa kifedha na rasilimali nyingi za kusajili wachezaji bora, huku zile ndogo zikitegemea usajili wa busara na kiuchumi ili kuhimili ushindani.

Usajili wa aina hiyo mara nyingi huzipa mzigo wa kifedha, huathiri morali ya kikosi na mara nyingine husababisha kushuka daraja. Ungana na Mwanaspoti katika mahojiano na kocha wa Pamba, Fredy Felix ‘Minziro’ aliyewahi kuifundisha Geita Gold na kuweka rekodi ya kutinga michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mbali na hayo, Minziro anagusia mambo mbalimbali akieleza chimbuko la jina lake hilo maarufu tangu alipokuwa kijana akizichezea timu za Yanga na Pan African, huku akigusia sababu zinazowafanya makocha wasipate muda wa kupumzika akitaja matokeo, mazoezi, mikakati, vyombo vya habari pamoja na kusimamia tabia na maendeleo ya wachezaji kwamba vinachangia.

Hilo ni shinikizo ambalo huambatana na ratiba ngumu zisizo na nafasi ya mapumziko, hali inayowafanya makocha wengi kukosa muda wa kupumzika au kujitunza kiafya na kiakili.


PAMBA ILICHELEWA HAPA

Minziro, kocha wa pili Pamba msimu huu aliyerithi mikoba ya Goran Kopunovi aliyetimuliwa siku chache baada ya Ligi Kuu Bara kuanza anasema moja kati ya kosa kubwa ambalo Pamba Jiji ililifanya tangu awali ni usajili ambao uliifanya timu iyumbe katika mzunguko wa kwanza.

“Kuchelewa kwa Pamba kumesababishwa na jinsi ambavyo walifanya usajili ambao baadaye ulifeli maana hii kazi inahitaji wachezaji na ukishakosea hapo basi lazima upoteze. Nilipokuja niliagiza baadhi ya wachezaji ambao walitubusti sana mpaka kufikia hatua hii ambayo tupo na naamini tutamaliza vizuri,” anasema.

Pamba ambayo ilipanda Ligi Kuu msimu huu kocha huyo anasema suala la kusalia ana uhakika nalo zaidi kwani anaamini kupitia kikosi alicho nacho wanatafanikiwa.

“Nafasi ya kusalia ni kubwa kwa sababu tumepiga hatua. Tulikuwa sehemu hatari tukapigana kuisukuma timu kufanikiwa.

Tukatoka chini mpaka hapa tulipo na tunapigana na timu ambazo zilikuwa juu yetu na zingine tumeziacha. Kwa hiyo kikubwa nafasi yetu ya kusalia bado ipo,” anasema.

Kocha huyo anaweka wazi kuwa mkataba wake na Pamba Jiji kwamba uko ukingoni, lakini kama viongozi watamuongeza ataendelea na kazi.

“Mimi niko kwenye timu kwanza kuhakikisha haishuki daraja na kazi yangu kubwa ni kuishauri timu kuhakikisha kwamba tunapambana. Kwa asilimia kubwa tunaenda vizuri na ninaamini tutafanikiwa tu. Baada ya hapo tutakaa mezani kufanya mazungumzo mengine.”

Akizungumzia ukaribu wake na msaidizi wake, Mathias Wandiba, Minziro anasema ni kutokana na kuzoweana kikazi na kupata mafanikio kwa pamoja.

“Sisi ni ‘wanyama wa mbugani’ huwa tunafanya kazi kila wakati ambayo hakuna asiyeiona kwa sababu inakwenda vizuri. Tulikuwa Singida pamoja, Alliance na Geita ambako tuliipeleka timu kimataifa baada ya kushika nafasi ya nne (katika Ligi Kuu).

“Bado tukaendelea na ligi yetu hii, tukaondoka pale Geita tukiwa nafasi ya tano, lakini tukawaachia timu yao. Siri kubwa ni kwamba unapofanya kazi inakuwa na mafanikio kutokana na umoja. Sifa yake (Wandiba) kubwa ni kijana ambaye anajituma na kuwajibika na msikivu. Kwa hiyo ni rahisi kufanya naye kazi kwa sababu mnaelewana.”


UBORA WA LIGI, WAAMUZI

Minziro aliyewahi kukipiga Yanga na Pan African enzi hizo, anasema kuna mahala Ligi Kuu Bara imefika na hayo ni mafanikio ya pamoja.

“Nikiambiwa niieleze kwa ujumla nitasema ligi yetu iko kwenye ubora mkubwa na ni jambo la kuwashukuru watu wa Azam, NBC na hawa ndio wameifanya ifikie hivi ilivyo. Hizi kampuni mbili zimewajibika na kugharamika sana kuhakikisha inakuwa  bora unaona wachezaji sio kama zamani mishahara ilikuwa hakuna mpaka wanagoma,” anasema.

“Wachezaji wa kigeni pia wengi wameongezeka wanaendelea kuja. Zamani wengi walikuwa wanakimbilia Sauzi, lakini sasa kila mtu anatamani kucheza Bongo, huu ni ukuaji.”

Akizungumzia uchezeshaji wa waamuzi wengi, kocha huyo anasema: “Kuhusu suala la waamuzi tunaweza kulizungumzia, lakini pia wanazidiwa japokuwa muda mwingine wanasemwa hawatendi haki, ila wanahitaji kuadhibiwa kwani hakuna mwamuzi ambaye ataadhibiwa akajisikia furaha. Kwa hiyo na wao pia waendelee kujifunza ili wasirudie makosa.

“Sipendi kubishana na waamuzi wala kuwapinga kwa sababu nawaachia kwa sasa hivi, mbali na kuwa na vyombo vya waamuzi ila mechi ziko mbashara wachambuzi wanaona na wanasema ukweli na uongo. Kwa hiyo kuna vitu ambavyo ukiviona unaweza kusema umeonewa, lakini ukiangalia marudio utagundua kuwa waamuzi walikuwa sahihi.

“Wapunguze makosa sasa ligi yetu inatazamwa dunia nzima. Kama tunasema sisi ni bora basi tuendelee kuwa vizuri zaidi.”


MRITHI WAKE

Beki huyo wa zamani wa Yanga anasema wapo mastaa wengi ambao akiwaangalia anaona wamefuata nyendo zake japokuwa kuna tofauti flani hivi ya uchezaji na ule aliokuwa nao enzi zake.

“Unajua sasa mpira umebadilika ni tofauti na sisi zamani tulikuwa tunawajibika binafsi bila kocha kukufundisha. Vingine vya ziada unaongeza mwenyewe. Wapo baadhi yao unawaona wanafanya kazi nzuri, wengine bado kwa sababu ya uvivu na kutojitambua kwa sababu mwingine unamkuta yuko vizuri ana uwezo.

“(Lakini) anashindwa kuelewa kuwa huu mguu wake ni pesa yaani kama wangekuwa wanajitambua thamani walionayo... zamani wakati mimi nacheza nilikuwa beki ambaye najua thamani ya mguu wangu, sikutaka adui auchezee. Kwa hiyo bado hawajajitambua ingawa najua kwamba wanalipwa. Kwa kazi yao ya mpira bado wengine mpaka uwasukume sana na hiyo ndio shida ya kizazi hiki,” anasema Minziro.

UGUMU KUFANYA KAZI NA WAGENI

“Ugumu ni mdogo sana, kwa sababu lugha ya mpira huwa inaeleweka duniani kote ndio maana mchezaji anaweza kutoka Brazil na akaja hapa akacheza bila shida.

“Kwa sababu lugha ya kocha inaeleweka, iwe raia au wageni hakuna shida yoyote katika ufanyaji wa kazi ni kawaida tu.

“Napenda kufanya kazi na wageni ijapokuwa sio wote nataka mwenye uwezo ili tusije kupoteza pesa bure kama inavyotokea kwa timu nyingi,unamsajili na kumlipa hela na wakati wazawa wako wengi.”


TOFAUTI TIMU KUBWA NA NDOGO

Minziro ambaye pia aliwahi kuifundisha Yanga kipindi cha nyuma anasema tofauti ya timu kubwa na ndogo ipo na ni kubwa.

“Kwanza kufundisha timu kubwa muda mwingi unakuwa salama sana, kwani unakuwa huna presha kubwa kama utakavyokuwa kwa hizi. Presha yake ni pale ambako mnakuwa hampati matokeo unaipata kwa wanachama na mashabiki, lakini vinginevyo ukishapata kile unachokitaka kocha unakuwa umetulia kwa sababu uko na watu ambao wako tayari.

“Ila kwa timu ndogo lazima upambane kuhakikisha mchezaji yuko tayari na kupata wenye uwezo huwa ni wachache sana. Kazi inakuwa kubwa kumfanya huyu mdogo aendane na wakubwa.”


SAA ZA KUPUMZIKA

Kutokana na majukumu makubwa aliyonayo kama kocha, Minziro anasema hapati muda mwingi wa kupumzika labda wakati wa likizo.

“Siwezi kusema ni saa ngapi kwa sababu muda mwingi niko kwenye presha tu kwa sababu kama wakati huu unafikiria timu haijawa salama. Sidhani kama napata muda nikilala saa moja au mawili nafikiria mechi tu. Ukipata matokeo mazuri afadhali unapata muda wa kupumzika, hasa kwa timu zetu hizi (ndogo) ukipata pointi kichwa kinatulia na ninalala kwa muda sasa.”


KUHUSU KUBETI

Wachezaji wengi sasa wameingia kwenye wimbi la mchezo wa kamari na kocha Minziro anasema kuwa suala hilo ni kweli.

“Mwanzo nilikuwa siamini, ila sasa naanza kuyaona kwa sababu kuna baadhi ya timu wanasema wameondoa wachezaji kwa mambo kama hayo,” anasema.

“Kwa hiyo yapo lakini sio mazuri kwa sababu mchezaji anapoingia kwenye masuala hayo hata huko duniani kwenye mambo ya mpira wanasema mchezaji kama huyo akijulikana anafungiwa maisha kabisa hata kama ni kocha au kiongozi.”

Miziro amedumu katika soka kwa miaka mingi, kwanza akiwa mchezaji na pili kocha wa timu mbalimbali kwenye Ligi Kuu Bara na Ligi Daraja la Kwanza, hivyo kwa wengi ni miongoni mwa wakongwe ambao pengine kwa sasa wangekuwa wameshastaafu masuala ya soka.

Hata hivyo, mwenyewe ukimuuliza kwanini bado yupo katika mikikimikiki hiyo anasema: “Nilishawahi kufikiria kuhusu (kupumzika) ndio maana nikapumzika ila kwa sasa najiona bado niko fiti na nitaendelea kuwepo katika mpira.

“Ila ninapopata matokeo mabovu hapo natamani kuacha (mpira) nikafanye mambo ya kufanya, ila bado najiona nina nguvu za kufanya japokuwa mpira una matokeo matatu.”


KAZI NA MAKOCHA WAGENI

Minziro ambaye aliwahi kufanya kazi na makocha wa kigeni anasema ni faida kufanya nao kazi, lakini maslahi ndio yanayowakwamisha (wazawa) wengi kutofundisha nje.

“Ukifanya kazi na hizi ngozi nyeupe unavuna mambo mengi, mbali na hizi kozi tunazokwenda na unakaa na makocha kama wale unapata faida kubwa sana. Kwa kocha yeyote hata pale Simba naamini Selemani Matola anapata mambo mengi kwa sababu yuko pale kwa muda mrefu japokuwa wakiondoka mnapoteana,” anasema kocha huyo.

“Matamanio ya kufundisha nje yalikuwepo ila inategemea ni nchi gani. Hizi za ukanda wetu ulipaji ni wa shida, hivyo hakuna maslahi.”


MATUKIO ENZI ZAKE

Mpira wa miguu una matukio mengi na Minziro kama mchezaji wa zamani anataja mambo ambayo hataweza kuyasahau.

“Mambo mengi ya mpira ambayo ni ya hovyo yalikuwepo toka zamani ila inategemea na jinsi mchezaji unavyokuwa na akili na utulivu. Mtu anaweza akakufuata kukuyumbisha na mambo ya rushwa labda, ila unamuangalia tu na kuachana naye kutokana na ukubwa wa akili yangu, au unaambiwa uifungishe timu ili upate nafasi ya kucheza timu nyingine ni mambo ya ajabu tu.”


KUNG’OLEWA JINO

Minziro anatoa stori jinsi alivyong’olewa jino na mchezaji mwenzake, Hussein Masha na kisha akachangiwa pesa.

“Nilipewa elfu saba tu ... ule mkasa ulikuwa hivi Masha alichezewa rafu na mchezaji wetu wa Yanga na kwa bahati mbaya alikuwa amekasirika sana. Wakati mwamuzi keshatoa uamuzi wake tunarudi uwanjani baada ya kugombana, nashangaa tu nimepigwa na kiwiko cha mdomo,” anasema Minziro.

“Basi jino likawa limetoka, lakini niliendelea na mechi mpaka mwisho. Nilizozana naye kidogo na mashabiki wakachangia, basi nikapata elfu saba miaka hiyo ni nyingi na nikaweka jino bandia. Ule mchango wa mashabiki ulinipa faraja nikaona kweli wananipenda na kunithamini kama mchezaji wao pendwa.”

MAWINGA HATARI

Mchezaji huyo wa zamani pia awaelezea nyota waliokuwa wakikipiga kama mawinga enzi hizo ambao kutokana na nafasi yake kama beki alilazimika kukabiliana nao.

“Ninapokutana na wachezaji kama Sunday Juma alikuwa Simba, wengine kama Beya Simba wa Pamba hao ni wachezaji ambao (walikuwa) wana kasi sana. Mtu kama Ali Nassoro wa Malindi, Amir Aziz kwa kweli nimekutana na mawinga wengi ambao walikuwa ni hatari. Ukiwa beki ni lazima uwe na makali ya kupambana na mtu kama Justine Simfukwe.”

Nyota huyo aliyekipiga pia timu ya taifa (Taifa Stars) anasema zipo mechi ambazo hatazisahau enzi hizo.

“Wakati huo nilikuwa bado chipukizi nikiwa na Pan Afrika nilicheza mechi dhidi ya Simba ikiwa imetoka Brazil wakija na mtindo wa Samba beki alikuwa (Ahmed) Amasha na hapo nimepewa nafasi ya kucheza kwa mara ya kwanza.

“Hapo wametoka Brazil wanapiga Samba ya ukweli, pale mimi nakuwa beki wa kushoto. Baada ya mechi hiyo tulitoka sare wakati huo Yusuf Ambwene anakaa benchi alikuwa na adhabu. Baada ya hapo nikaanza kuaminika na kucheza na Simba, Yanga kwani kocha alikuwa tayari ameshaniamini kuwa nina uwezo.”


KIMATAIFA, HESHIMA

Wakati akiwa kocha wa Geita Gold misimu michache iliyopita, Minziro alifanikiwa kuipeleka timu hiyo katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na hapa anautaja uzoefu alioupata.

“Kwa kweli nilipata uzoefu mkubwa kwani kwa vijana wale wengine ndio ilikuwa mara yao ya kwanza kucheza kimataifa na kusafiri pia. Lakini ilikuwa faraja kwani hata Geita hawakutegemea. Yote kwa yote vijana walifunga mkanda na kufanya yale ambayo waliyaweza na mwisho tukaweka rekodi hiyo nzuri. Kama Geita ingeendelea kuwepo, basi tungeshindana na timu kubwa.”

“Mimi naiona heshima kwa makocha wazawa. Sasa timu kama Geita ilivyoamua kusitisha mkataba wangu leo wako wapi? Kwa sababu unajifunza kutokana na makosa... unapofanya kazi kuna mwingine anaona kama unapiga kelele tu. Anadhani kocha yeyote akija anaweza kufanya, kumbe anakosea.

“Nadhani hata wao Geita wanajuta, mimi heshima yangu iko palepale ukiniletea dharau basi nakuachia kazi yako,” anasema.

Minziro ni miongoni mwa wachezaji ambao ni zao la Zanzibar kwani alikulia huko, na hapa anataja tofauti kati ya soka la Bara na Zanzibar.

“Zanzibar wanalipa, lakini sio kama huku Bara, ila kule wanakazania sana vijana na kazi yao ilikuwa kuwapandisha wachezaji timu za juu. Wanatoa vipaji vingi kwa sababu vijana wengi ni kucheza Bara, na walionyesha ubora kwenye mechi za Muungano.

“Wanapokutana na timu za huku (Bara) basi wanapambana kuonyesha vipaji na wanafanikisha hilo. ZFF waiboreshe ligi hasa kwa wadhamini.”


MAJINA MINZIRO, BABA ISAYA

Mchezaji huyo wa zamani kila mmoja anamjua kwa majina matatu, yaani Fredy Felix Minziro, lakini hilo la Minziro lina siri yake.

“Jina langu halisi ni Fred Felix Yesaya Kataraiya. Hii Minziro ni la utani lilitokana na vita vya Uganda na Tanzania wakati ule unajua mazoezi tunapiga pale Kaunda - Jangwani (Dar). Wakati huo wa vita (mashabiki) wanakaa hapo na redio zao wanaangalia mazoezi, basi wakasikia jina la Minziro, basi mtu akaanza kuniita hivyo watu wakaanza kulitumia hadi leo,” anasema.

“Minziro ni kijiji kimoja kipo huko Kagera. Mwaka Jana nilitamani kwenda wanione maana nimelipaisha sana jina lao, ila sikupata muda. Jina la Majeshi nilipewa kutokana na aina yangu ya uchezaji wa morali, nacheza huku naongea, lakini Baba Isaya pia nilipewa ila sina mtoto anayeitwa hivyo.”

Minziro pia anatoa siri ya kwa nini timu nyingi zikikutana naye zinajipanga akisema sababu ni moja tu - mbinu.

“Watu wanajua kuwa unapokutana na mimi ukilegalega nakufunga hata mabao matano. Wote makocha wanajua ndio maana wanapocheza na mimi wanakaza. Mechi zangu zote ambazo tumecheza na kushinda hazikuwa rahisi. Tumekutana na Dodoma (Jiji) tukawafunga ilikuwa vita, Azam - Mwanza. Mchezaji mvivu simtaki hawezi kuwa rafiki yangu kwa sababu anaharibu kazi.”