JKT Queens v Yanga Princess, mechi ya ubingwa

Muktasari:
- JKT ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) ikiwa na pointi 38 na Yanga ikiwa nafasi ya pili na pointi 33.
BAADA ya kupoteza mchezo dhidi ya Simba Queens wikiendi iliyopita, JKT Queens itashuka tena Uwanja wa Mej Gen Isamuhyo ikiikaribisha Yanga Princess.
JKT ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) ikiwa na pointi 38 na Yanga ikiwa nafasi ya pili na pointi 33.
Msimu huu timu hizo zinakutana mara nne kwenye mashindano tofauti na JKT ikishinda mara mbili na kupoteza mechi moja.
Timu hizo zilianza kukutana mwanzoni mwa msimu Oktoba 05, mwaka jana kwenye fainali ya ngao ya jamii ambayo JKT ilibeba ubingwa kwa kuitandika Yanga bao 1-0 la Donisia Minja.
Desemba 17 zilipokutana tena kwenye Ligi, JKT iliondoka na ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa tena na Minja.
Kwenye mashindano ya Samia Cup zilizoshirikisha timu nne, Yanga ilitandika JKT mabao 3-0.
Ni mechi ya maamuzi endapo JKT itapoteza basi itakuwa imejitoa kwenye mbio za ubingwa zinazowaniwa na Simba iliyopo kileleni na pointi 40 tofauti ya pointi mbili na wanajeshi hao.
Licha ya rekodi nzuri ilizonazo JKT kila wanapokutana lakini ni mechi ngumu kwa timu zote mbili kutokana na ubora wa Yanga waliouonyesha hivi karibuni.
Miongoni mwa nyota wa Yanga wa kuchungwa kwenye mechi hiyo ni mshambuliaji, Jeaninne Mukandayisenga ambaye kwenye mechi sita amefunga mabao nane.
Kwa JKT ukiachana na Stumai Abdallah kinara wa ufungaji akiwa na mabao 26, Winifrida Gerald ni miongoni mwa nyota ambao kama safu ya ulinzi ya Yanga haitakuwa makini kumkaba.