Prime
Hatumtendei haki Mbwana Ally Samatta, ni huzuni
WAPI heshima kwa Mbwana Samatta? Siioni. Napita mitandaoni na napita katika vijiwe, lakini siioni heshima ambayo anastahili kupewa. Michuano ya Afcon inaendelea kule Morocco na maelfu ya Watanzania wanaongea vibaya kuhusu Samatta.
Desemba, mwaka huu alitimiza miaka 33. Yupo katika siku za mwisho za kucheza katika ubora wake. Samatta hayupo katika ubora wake, lakini hata Cristiano Ronaldo hayupo katika ubora wake. Lionel Messi hayupo katika ubora wake.
Mambo hufika mwisho. Yanapofika mwisho huwa tunajadili walichowahi kufanya katika mpira na tunakiheshimu kuliko viwango vyao. Kwa hiyo tunajaribu kusamehe kinachoendelea na kujaribu kukumbuka kikubwa walichotufanyia. Na Samatta ndivyo alivyopaswa kujadiliwa.
Ukienda mitandaoni kwa sasa ni zile kauli zinazoudhi na kulenga kumdhalilisha Mtanzania wa kwanza kucheza katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu England. Mtanzania wa kwanza kufunga bao Wembley.
Mtanzania wa kwanza kuifunga Manchester City. Mtanzania wa kwanza kuifunga Liverpool. Mtanzania wa kwanza kucheza soka la kiushindani la kiwango cha juu kabisa.
Baada ya mechi dhidi ya Nigeria kauli ni zilezile chafu ‘hana lolote’. ‘Huyu naye wa nini?’. ‘Huyu naye angetupisha tu’. Kauli zinazoudhi. Mbwana hayupo katika ubora wake, lakini sio mchezaji mbinafsi.
Kuna wakati alikuwa anataka kustaafu katika timu ya taifa, rais Wallace Karia na watu wa TFF wakamwambia wanamhitaji sana. Kuna wakati anajipumzisha kwa ajili ya kupisha nguvu mpya katika kikosi cha timu ya taifa ikiwemo katika zile mechi za kirafiki.
Huyu sio mchezaji mbinafsi. Hata Morocco hajajipeleka mwenyewe na wala hajipangi mwenyewe. Na hata alipowekwa benchi katika pambano dhidi ya Uganda hakuchukia. Nafasi yake ilikwenda kwa Kevin John ambaye alimpokea na kujaribu kumtunza kule Genk.
Hata hivyo, pambano hilo hilo lilitukumbusha kwamba mambo sio rahisi mle uwanjani kama watu wanavyoamini. Kuna wale ambao wanadhani Samatta hajitumi katika timu ya taifa, lakini Kevin aliingia uwanjani na alipata wakati mgumu kama anavyopata Samatta.
Ilipofika mapumziko watu walewale ambao walisema Samatta atupishe katika mechi ya kwanza ndio walewale waliotaka Kevin atoke ili Samatta aingie.
Hii ni kuthibitisha kwamba wakati huu kuna watu wanaomsakama Samatta lazima wakumbuke kwamba kwanza anastahili heshima kwa aliyoyafanya, lakini pia bado hatujatengeneza kina Samatta wengine kama tunavyofikiria.
Katika kiwango chake hiki hiki cha sasa, Samatta bado anapambana na kina Clement Mzize, Kevin John, Suleiman Mwalimu na wengineo. Ni vile tu watu wamemchoka. Ni vile tu kuna watu wengine wanaamini kwamba yeye ni kila kitu katika kikosi chetu.
Maisha sio rahisi sana kama watu wanavyodhani. Maisha sio rahisi sana unapozaliwa katika taifa kama la Tanzania. Hauwezi kuibeba timu mgongoni peke yako. Sio Tanzania tu. Ryan Giggs hajawahi kucheza Kombe la Dunia. Alizaliwa Wales, taifa ambalo halina mastaa wengine wa kumsaidia kazi.
George Weah hajawahi kuipeleka Liberia Kombe la Dunia licha ya yeye kuwahi kuwa mwanasoka bora wa dunia. Maisha sio rahisi unapotokea katika taifa ambalo halina vipaji vikubwa. Zambia ina wachezaji wazuri, lakini Kalusha Bwalya hakuwahi kuipeleka Kombe la Dunia.
Katika dunia ya leo ni bahati kwamba tulimpata Samatta na akawaonyesha watoto wetu nini maana ya mafanikio. Zamani mafanikio tulikuwa tunayapima kwa kina Boniface Pawassa. Tulikuwa tunayapima kupitia wachezaji wa ndani. Samatta ametuonyesha nini maana ya mafanikio halisi.
Ni kweli kwamba kwa sasa amepungukiwa na uwezo wake. Hata yeye mwenyewe haamini katika nguvu zake na alisema wazi baada ya pambano dhidi ya Uganda. Tunachopaswa kukilinda kwa sasa ni heshima yake. Wazungu huwa wanaita legacy.
Sisi hatumdai sana ila yeye anatudai sisi kuitukuza heshima yake. Ni jambo ambalo hatulifanyi pale tunapohisi amekuwa na mechi mbovu uwanjani. Ni kitu ambacho wenzetu huwa wanakiweza na wanakifanya. Watanzania tunaishi kwa ajili ya leo tu na hatuiheshimu jana yetu.
Najua unafiki wa Watanzania. Muda si mrefu Samatta hatakuwepo tena katika jezi ya Taifa Stars na tutaanza kumkumbuka. Ndani ya mwaka huu huu tuliwahi kuwakumbuka Samatta na Simon Msuva wakati walipokosekana katika jezi ya taifa Stars. Leo tumegeuka tena.
Kwa sababu hatuzalishi kina Samatta wengine hatuna muda mrefu tutaendelea kumkumbuka Samatta huyu ambaye watu wanamzodoa mitandaoni. Kama kungekuwa na watu wetu wanacheza Stuttgart, Torino, PSV na timu za madaraja haya labda tungeweza kudai aondoke mapema sana. Lakini kwa kuwategemea washambuliaji wetu wengine hawa hawa nadhani muda si mrefu Samatta atastaafu na tutaleta unafiki wa kumkumbuka.
Binafsi namheshimu Samatta kwa legacy ambayo anatuachia. Baada ya kila kitu alichotufanyia katika mpira wetu siwezi kuandika neno la kumdhalilisha kwa sababu tu ameshindwa kumiliki mpira vizuri katika pambano moja la Taifa Stars pale Rabat. Utakuwa ujinga.
Hata kina Kalusha Bwalya na George Weah katika siku zao za mwisho za usakataji wa soka walionekana wazi kwamba walikuwa wameishiwa lakini watu walikuwa wanashughulika zaidi na kuheshimu walichofanya kuliko kujadili zaidi viwango vyao uwanjani.
Wachezaji ambao wanaweza kusemwa vibaya ni wale ambao wanang’ang’ania kuitwa au kuchezea timu zao za taifa angali wakiwa wamechoka. Samatta haonekani kuwa mbinafsi na mwenye tabia hizo. Kwanini tunamsema? Huwa anajiita katika kikosi? Huwa analazimisha kupangwa? Huwa ni mjivuni nje ya uwanja? Hapana. Kwanini tunamsema vibaya staa wetu? Ni huzuni.
Kule kwenye muziki inaonekana wanatushinda. Mbona hawawasemi vibaya kina Profesa Jay na wanaendelea kusifia nyimbo zao za zamani ingawa wanajua kwamba kwa sasa hawawezi kushindana na kina Diamond Platnumz katika muziki wa sasa? Ni huzuni.