Prime
Moallin afichua jambo, Ibenge amtaja Arajiga, aigusia Simba
KAIMU Kocha Mkuu wa Yanga, Abdihamid Moallin, akifichua siri ya ushindi wake kuelekea kutimiza ndoto ya kutetea ubingwa wao, huku kocha wa Azam,Florent Ibenge akilia na mwamuzi Ahmed Arajiga.
Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 69 mbili zaidi ya Simba (67) inayoshika nafasi ya pili huku kila timu ikiwa na mechi mbili mkononi.
Kocha Moallin alisema ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Azam ulikuwa muhimu kwa sababu ulipatikana dhidi ya timu bora katika kipindi ambacho Yanga imekuwa ikikabiliwa na michezo migumu mfululizo, ikiwamo kucheza na wapinzani hao mara mbili ndani ya siku chache baada ya pambano la nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB lililodumu dakika 120.
Alisema licha ya uchovu uliokuwepo kwa pande zote mbili, wachezaji wa kikosi chake walionyesha kiwango cha juu cha kujituma na kutekeleza kwa usahihi kile walichokipanga kabla ya mchezo.
“Si rahisi kufunga mabao matatu dhidi ya Azam na wakati huo huo kutoruhusu bao. Tulijua tunakutana na moja ya timu bora nchini yenye wachezaji wazuri, kocha mzuri na mfumo mzuri wa mchezo, hivyo tulipaswa kuwa katika kiwango chetu bora kabisa,” alisema Moallin.
Kocha huyo alisema siri kubwa ya ushindi huo ilikuwa kudhibiti eneo la kiungo, sehemu ambayo waliamini ndiyo nguvu kubwa ya Azam katika kujenga mashambulizi.
Kumbuka eneo la kiungo la Azam pale kati katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Juni 24, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, walianza Himid Maona Sadio Kanoute, dakika ya 71 wakafanyiwa mabadiliko wakaingia Yahya Zayd na James Akaminko huku Feisal Salum 'Fei Toto'alicheza dakika zote.
“Tulitaka kudhibiti safu ya kiungo na kuwanyima nafasi wanazopenda kuzitumia zaidi. Wachezaji walitekeleza hilo kwa kiwango cha juu sana na ndiyo maana tuliweza kuudhibiti mchezo,” alisema.
Katika kudhibiti hilo, Moallin katikati alianza na Duke Abuya na Maxi Nzengeli, huku mfumo wa uchezaji wa Yanga ulikuwa wakienda kushambulia Allan Okello na Pacome Zouzoua wanaongezeka kati na kufanya kuwa viungo wanne, kisha Laurindo Aurelio 'Depu' akitanua kushoto akicheza kama winga, huku Prince Dube akibaki kati kama mshambuliaji wa mwisho na beki wa kulia, Yao Kouassi, anapanda akiwa kama winga wa kulia. Katika kuzuia, wote hao walikuwa wakirudi nyuma wakimuacha Dube na Depu mbele.
Katika hatua nyingine, Moallin alisema ratiba ngumu waliyoipitia tangu kumalizika kwa kalenda ya FIFA ilikuwa imeonekana ngumu kwa wengi, lakini walichokifanya ni kujikita kwenye maandalizi ya kila mchezo mmoja baada ya mwingine.
Sasa baada ya ushindi huo, Yanga imebakiwa na michezo miwili dhidi ya TRA United (Juni 27) na JKT Tanzania (Juni 30), mechi ambazo zinashikilia hatma ya kutetea ubingwa wao wa ligi.
Moallin alisema hakuna kitakachobadilika katika mtazamo wao kuelekea mechi hizo mbili za mwisho kwani lengo linaendelea kuwa moja tu, kukusanya pointi zote zinazowezekana.
“Leo (Jumatano) tumemaliza Azam, kesho (Alhamisi) tunaanza kufikiria mchezo unaofuata. Tuna wachezaji wenye ubora mkubwa na akili ya ushindani. Kila mechi iliyobaki ni muhimu na tunahitaji pointi tatu,” alisema.
Yanga inapambana kutetea ubingwa wa ligi iliouchukua kwa misimu minne mfululizo, huku ikilitolea macho taji hilo baada ya kuvuliwa lile la CRDB ikiolondoshwa nusu fainali kwa kufungwa 3-2 na Azam.
MSIKIE IBENGE
Kwa upande wa Azam, Kocha Mkuu Florent Ibenge, alisema uchovu uliotokana na mchezo wa nusu fainali dhidi ya Yanga uliwaathiri kwa kiasi kikubwa na kuchangia kupoteza mchezo huo.
Ibenge alisema kikosi chake kilianza mchezo ikiwa imepungukiwa nguvu baada ya kucheza sehemu kubwa ya mechi iliyopita ikiwa na wachezaji 10, jambo lililofanya waonekane dhaifu katika kipindi cha kwanza walichoruhusu bao.
“Mwanzoni tulionekana kuchoka. Tulicheza mechi iliyopita tukiwa pungufu ya mchezaji mmoja kwa muda mrefu na hilo lilitugharimu. Kipindi cha kwanza tulikuwa nyuma kwa bao moja,” alisema Ibenge.
Hata hivyo, alisema Azam ilirejea vizuri kipindi cha pili na kuanza kuutawala mchezo kwa kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga kabla ya mwelekeo wa mchezo kubadilishwa na bao la pili la Yanga lililotokana na penalti iliyotolewa na mwamuzi Ahmed Arajiga.
“Niliona tulikuwa bora zaidi kipindi cha pili. Tulimiliki mpira na kutengeneza nafasi za kufunga, lakini mambo yalibadilika baada ya penalti. Sijui kama kweli ilikuwa penalti, lakini mwamuzi (Arajiga) ndiye mwenye uamuzi ya mwisho. Bao hilo la pili lilibadilisha kabisa mchezo,” alisema.
Penalti hiyo ilitokana na beki wa Azam, Twalibu Nuru katika harakati za kumzuia Depu asifunge bao akiwa ndani ya boksi, akaonekana kumuangusha kwa tafsiri ya Arajiga, ni faulo hivyo Yanga ikanufaika licha ya kwamba marejeo ya video ilionekana beki aliugusa mpira.
Pamoja na kipigo hicho, Ibenge aliendelea kuisifu Yanga akisema imeendelea kuwa timu bora nchini kwa miaka ya hivi karibuni kutokana na uthabiti wake wa kiushindani.
“Nimesema mara nyingi kuwa Yanga ndiyo timu bora Tanzania kwa miaka mitano iliyopita. Ukicheza dhidi ya timu kama hiyo ukiwa umetoka kwenye mazingira magumu, si jambo rahisi,” alisema.
Kocha huyo hakusita pia kuzipongeza Yanga na Simba kwa mchango wao mkubwa katika kuifanya ligi ya Tanzania kuwa na ushindani mkubwa zaidi barani Afrika.
Alisema mafanikio ya timu hizo mbili katika mashindano ya CAF yamechangia Tanzania kupata nafasi ya kuwakilishwa na timu nne katika michuano ya Afrika.
“Tunajua Yanga na Simba ni timu kubwa. Wamefanya mambo makubwa katika soka la Afrika na mafanikio yao ndiyo yameifanya Tanzania kupata nafasi ya kupeleka timu nne kwenye mashindano ya CAF. Nawapongeza kwa mchango wao,” alisema.
Ibenge alisisitiza kuwa licha ya kupoteza mchezo huo, Azam itaendelea kujijenga na kupambana ili kufikia kiwango cha kushindana kwa karibu zaidi na vigogo hao wa soka la Tanzania katika misimu ijayo.