Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Siri ya Sekunde 5,400 za sapraizi Ligi Kuu Bara

SAPRAIZI Pict


LIGI Kuu Bara msimu huu imefika kwenye hatua moja kabla ya ile ya mwisho zote zikiwa zenye presha kubwa zaidi katika maeneo tofauti.


Mechi nane zitachezwa kesho na kila moja itakuwa na dakika 90 zenye sekunde 5,400 za sapraizi ambazo zinaweza kubadili historia ya klabu, wachezaji na makocha.


Kuanzia kileleni kwenye mbio za ubingwa, katikati ya msimamo ambako baadhi ya timu zinapigania kumaliza katika nafasi nzuri hadi chini kwenye vita vya kujiokoa dhidi ya kushuka daraja hakuna timu ambayo inaweza kuingia uwanjani ikiwa haina jambo la kupigania.

Raundi ya 29 inayochezwa leo, Jumamosi, imebeba uzito mkubwa kwa sababu inaweza kuamua hatima ya ubingwa, kutoa picha ya mwisho ya timu zitakazoshuka daraja pamoja na kuongeza ushindani katika tuzo binafsi za ufungaji bora, asisti nyingi na 'clean sheet' nyingi.


SAPRA 03

YANGA BADO KIDOGO

Kwa mara nyingine tena, ubingwa wa Ligi Kuu umebaki kuwa mapambano kati ya watani wa jadi, Yanga na Simba.

Yanga ndiyo inayoongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 69 baada ya kucheza mechi 28, huku Simba ikifuatia kwa pointi 67. Tofauti ya pointi mbili pekee imeifanya raundi ya 29 kuwa ya muhimu zaidi kwa timu zote mbili.

Kwa hesabu zilizopo, Yanga inahitaji kukusanya pointi nne katika mechi mbili zilizobaki, dhidi ya TRA United na JKT Tanzania ili kutwaa ubingwa bila kutegemea matokeo ya Simba.

Hilo linaifanya mechi ya leo Jumamosi dhidi ya TRA United katika Uwanja wa KMC Complex, Dar kuwa kama fainali nyingine kwa kikosi cha Jangwani.

Ushindi katika mchezo huo utawapeleka hatua moja tu kuelekea kutwaa ubingwa wao wa tano mfululizo, mafanikio ambayo yataendelea kuthibitisha ubabe wao katika soka la Tanzania.

Yanga imeonyesha uthabiti mkubwa msimu huu. Mbali na kuwa na safu imara ya ulinzi ikiruhusu mabao tisa ambayo ni machache zaidi, pia imekuwa ikipata ushindi katika mechi ambazo zimeonekana kuwa ngumu, jambo ambalo limeifanya ibaki kileleni kwa kipindi kirefu cha msimu.


SAPRA 06

SIMBA HAINA NAFASI YA KUKOSEA

Kwa upande wa Simba, hesabu ni nyepesi kuzisema lakini ni ngumu kuzitimiza.

Wekundu wa Msimbazi hawana nafasi ya kupoteza hata pointi moja katika mechi mbili zilizobaki. Wanalazimika kuifunga Singida Black Stars katika raundi ya 29 na kushinda pia mchezo wao wa mwisho wa msimu dhidi ya KMC.

Lakini hata ikifanya hivyo, bado hawatakuwa na uhakika wa ubingwa isipokuwa Yanga ipoteze pointi katika moja ya michezo yake miwili iliyobaki.

Hii ndiyo hali inayowafanya Simba kuingia katika raundi hii wakibeba presha kubwa. Baada ya kuukosa ubingwa kwa misimu minne mfululizo, mashabiki wao wanaamini huu ndiyo wakati wa kurejesha heshima ya klabu.

Tatizo kubwa kwa Simba ni mpinzani wao, Singida Black Stars, si timu ya kubeza. Tayari Singida imejihakikishia nafasi ya nne kwenye msimamo ikiwa na pointi 50 na imekata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

Kutokana na kutokuwa na presha ya matokeo, Singida inaweza kucheza kwa uhuru zaidi, jambo linaloweza kuifanya kuwa mpinzani mgumu kwa Simba.


SAPRA 04

CHINI KUNAWAKA MOTO

Wakati macho mengi yakiwa kwenye mbio za ubingwa, vita ya kusalia Ligi Kuu nayo imefikia hatua ya mwisho.

KMC tayari imeshuka daraja baada ya kukusanya pointi tisa pekee katika michezo 28.

Timu hiyo imeshuka daraja moja kwa moja baada ya kuwa na msimu mbaya ulioshuhudia ikipoteza michezo 23.

Lakini pambano kubwa zaidi sasa liko kati ya Tanzania Prisons, Mtibwa Sugar, Mbeya City, Fountain Gate, Namungo na Mashujaa.

Kila timu kati ya hizo bado ina nafasi ya kujikuta katika eneo la kushuka daraja au kujinusuru kulingana na matokeo ya raundi mbili zilizobaki.


TANZANIA PRISONS VS MTIBWA KUNA KAZI

Mchezo unaosubiriwa kwa hamu zaidi katika vita vya kushuka daraja ni ule wa Tanzania Prisons dhidi ya Mtibwa Sugar utakaochezwa Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Prisons ipo nafasi ya 15 ikiwa na pointi 26, nafasi ambayo ina maana ya kushuka daraja moja kwa moja.

Mtibwa Sugar ipo nafasi ya 14 ikiwa na pointi 27, nafasi ya kucheza play-off.

Tofauti ya pointi moja pekee imeufanya mchezo huu kuwa kama fainali.

Iwapo Prisons itashinda, itapanda juu ya Mtibwa na kuwaweka Wakata Miwa hao katika hatari kubwa ya kushuka daraja.

Kwa upande wa Mtibwa, kupoteza kutamaanisha kwamba italazimika kushinda mchezo wake wa mwisho dhidi ya Namungo huku ikiomba Prisons ishindwe kupata matokeo mbele ya Mashujaa.

Kwa kifupi, timu itakayofanya kosa katika mchezo huu inaweza kujikuta ikilipa gharama kubwa mwisho wa msimu.


MBEYA CITY ITATOBOA?

Mbeya City nayo imefufua matumaini ya kubaki ligi kuu baada ya ushindi muhimu dhidi ya Pamba Jiji uliowafanya kufikisha pointi 28.

Katika raundi ya 29 watacheza dhidi ya Dodoma Jiji, ambayo tayari imejihakikishia kubaki ligi kuu ikiwa na pointi 34.

Kwa Mbeya City, ushindi utaongeza nafasi kubwa ya kuendelea kubaki ligi kuu na kupunguza presha kuelekea mchezo wa mwisho.


SAPRA 05

NAMUNGO, FOUNTAIN GATE, MASHUJAA FC

Katika Uwanja wa Majaliwa kutakuwa na mchezo mwingine wenye uzito mkubwa kati ya Namungo na Fountain Gate.

Namungo ina pointi 30 huku Fountain Gate ikiwa na pointi 29.

Matokeo ya mchezo huo yanaweza kuamua timu ipi itaingia raundi ya mwisho ikiwa katika mazingira salama na ipi itaendelea kuwa kwenye presha ya kushuka daraja.

Mashujaa, ambao pia wana pointi 30, wana nafasi nzuri ya kujinusuru endapo wataifunga KMC ambayo tayari imeshathibitisha kushuka daraja. Kwa jumla, vita vya kushuka daraja vinaonekana kuwa na ushindani mkali sawa na ule wa kuwania ubingwa.


SAPRA 01

HUKU NAKO SIO POA

Mbali na ushindani wa timu, vita ya tuzo ya mfungaji bora wa ligi nayo imezidi kuwa tamu.

Kwa sasa Mossi Ndumumwe wa Singida Black Stars na Feisal Salum 'Fei Toto' wa Azam wanaongoza kwa kufunga mabao 14 kila mmoja.

Wote wawili bado wana michezo miwili ya kuongeza idadi yao ya mabao, jambo linalomaanisha ushindi wa tuzo hiyo bado uko wazi.

Nyuma yao kuna Mathew Tegisi wa Pamba Jiji, Allan Okello wa Yanga na Fabrice Ngoy wa Namungo ambao kila mmoja amefunga mabao 11.

Tofauti ya mabao matatu pekee ina maana lolote linaweza kutokea katika raundi mbili zilizobaki.

Pia Mudathir Yahya (Yanga), Pacome Zouzoua (Yanga), Selemani Mwalimu (Simba) na Prince Dube (Yanga), ambao kila mmoja ana mabao tisa, bado wana nafasi ya kujisogeza juu iwapo watafunga katika michezo iliyobaki.


DIARRA ASHINDWE YEYE

Katika upande wa makipa, Djigui Diarra wa Yanga anaendelea kuthibitisha ubora wake.

Mpaka sasa amekusanya clean sheets 16, idadi inayomweka kileleni mwa orodha ya makipa waliocheza mechi nyingi bila ya kuruhusu bao.

Anamfuatia Mahamadou Kassali wa Simba mwenye clean sheets 14.

Diarra anahitaji clean sheet moja pekee katika michezo miwili iliyobaki ili kujihakikishia kumaliza msimu akiwa kinara wa kipengele hicho.

Hata kama Kassali atafanikiwa kupata clean sheets mbili katika mechi zilizobaki, bado hataweza kumpita Diarra endapo kipa huyo wa Yanga ataongeza clean sheet moja zaidi.


MPANZU ACHOMOZA

Katika utengenezaji wa mabao, Elie Mpanzu wa Simba ndiye anaongoza akiwa ametoa asisti tisa.

Kiungo huyo amekuwa mhimili muhimu katika safu ya ushambuliaji ya Simba kutokana na uwezo wake wa kutengeneza nafasi za kufunga.

Feisal Salum anaendelea kuwa katika msimu bora zaidi wa maisha yake baada ya kuwa nafasi ya pili kwa asisti akiwa nazo nane, huku pia akiongoza kwa pamoja katika ufungaji bora.

Okello, Iddi Selemani, Clatous Chama na Zabona Mayombya wote wana asisti saba kila mmoja, wakati Duke Abuya na Maxi Nzengeli wakifuatia kwa asisti sita.

Ushindani huu unaonyesha namna ambavyo ubora wa mchezaji haupimwi kwa kufunga mabao pekee, bali pia kwa uwezo wa kuwasaidia wenzake kufunga.


SAPRA 02

DAKIKA 180 HISTORIA KUANDIKWA

Kwa kifupi, raundi mbili zilizobaki za Ligi Kuu Bara sawa na dakika 180 kwa kila timu, zinatarajiwa kuwa miongoni mwa raundi zenye ushindani mkubwa zaidi katika miaka ya hivi karibuni.

Yanga inapigania kutetea ubingwa wake kwa mara nyingine, Simba inapambana kurejesha taji Msimbazi, huku vita vya kushuka daraja ikifanya timu zipambanie uhai wao.

Wakati huo huo, vita vya mfungaji bora, mtoa asisti bora na kipa mwenye clean sheets nyingi inaendelea kuongeza ladha ya mwisho wa msimu.

Hakuna shaka kuwa kila filimbi itakayopulizwa katika viwanja mbalimbali nchini itakuwa na maana kubwa ikizingatiwa kwamba mechi hizi zote zitaanza muda mmoja. Kwa baadhi ya timu itakuwa mwanzo wa shangwe za ubingwa na mafanikio, lakini kwa nyingine inaweza kuwa mwanzo wa machozi ya kushuka daraja. Hivyo, macho yote sasa yanaelekezwa kwenye raundi ya 29, ambayo inaweza kuamua kwa kiasi kikubwa sura ya mwisho ya msimu wa Ligi Kuu msimu huu wa 2025-2026.


RATIBA RAUNDI YA 29 NA 30

Juni 27, 2026 (zote saa 10:00 jioni)

Dodoma Jiji vs Mbeya City

Tanzania Prisons vs Mtibwa Sugar     

Yanga vs TRA United

Mashujaa vs KMC

Pamba Jiji vs JKT Tanzania

Simba vs Singida Black Stars

Coastal Union vs Azam

Namungo vs Fountain Gate


Juni 30, 2026 (zote saa 10:00 jioni)

JKT Tanzania vs Yanga

Simba vs KMC

Coastal Union vs Pamba Jiji

Fountain Gate vs Singida Black Stars

Mbeya City vs TRA United

Mashujaa vs Tanzania Prisons

Azam vs Dodoma Jiji

Namungo vs Mtibwa Sugar