Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tulimsahau Chuji, tukamuimba Mkude tupo na Morice Abraham


CHEZAJI sio shabiki. Nitakusimulia kitu kuhusu wachezaji wetu. Nitakwambia kitu kuhusu mabadiliko ya vizazi yanavyokwenda kasi. Mfano ni huo hapo ambao nimeutaja hapo juu namna maisha yanavyokwenda kasi kwa mchezaji wa Tanzania.


Ndivyo ilivyo duniani kote. Vizazi vinaenda kasi katika moja kati ya kazi za muda mfupi sana duniani. Kucheza soka. Ndiyo, ni kazi ya muda mfupi ambayo tunalazimika kuwakumbusha vijana wetu kuchukua chao mapema na kufanya kazi kwa nidhamu ya hali ya juu.

Kwa sisi wa ndani ya miaka 20 hii tulimshuhudia Athuman Idd 'Chuji' katika ubora wake. Pasi ndefu na fupi, uwezo wa kuchomoka kwa kasi katika eneo la kiungo. Uwezo wa kukaba. Kwa hapa mjini alianzia kwa Simba kisha akahamia kwa watani Yanga. Zaidi tulimpenda akiwa na timu yetu ya Taifa. Wakati ule akiwa na Marcio Maximo.

Hatujui Chuji alivuna nini katika mpira. Tulikuwa tunasikia tu kwamba anasaini mikataba mipya kwa mamilioni ya pesa. Hatujui aliwekeza au hakuwekeza. Tunachojua ni kwamba kwa sasa Chuji siyo kocha wala sio mchambuzi. Hatumuoni. Tunakutana naye katika mechi za veterans tu. Maisha yameshaenda kasi kwake.

Nani anamkumbuka Chuji Yanga? Nani anamkumbuka Chuji kama alikuwa hodari katika kikosi cha timu ya taifa? Ndio maana wachezaji wa nchi za wenzetu huwa ni wabinafsi linapokuja suala la maslahi. Mchezaji hata kama amekulia katika klabu hiyo hiyo, lakini linapokuja suala la mkataba wake huwa anakuwa makini na yeye na wawakilishi wake wanaweza kuzungumza na klabu hata kwa miezi sita.

Ndivyo kina Bukayo Saka walivyo. Ameingia Arsenal akiwa na miaka sita. Amelelewa na klabu, lakini mazungumzo yake ya mkataba na Arsenal huwa yanachukua miezi mingi. Kila upande unapigania maslahi yake. Mwishowe utasikia ndiye mchezaji anayelipwa zaidi klabuni. Hakuna anayemchukulia mwenzake poa. Sisi huku ingekuwa kesi ndogo kwa mchezaji aliyekulia klabuni kushinikizwa asaini mkataba mpya kwa sababu tu alilelewa na klabu.

Baada ya kizazi cha Chuji kikaja kizazi cha kina Jonas Mkude. Tulimuimba sana. Fundi wa mpira ambaye aliurahisisha mpira katikati ya uwanja. Bahati nzuri kwake alipita katika Simba yenye mafanikio ndani na nje ya uwanja. Ndani ya uwanja Simba walifika robo fainali za michuano ya CAF. Nje ya uwanja mpira wa Tanzania ulizidi kuongezeka pesa.

Muda mwingi alikuwa anahusishwa kwenda kwa watani Yanga. Iliwafanya Simba kuwa makini kumpa mikataba minono. Kuna wakati tukasikia alipewa Sh80 milioni kwa mkataba wa miaka miwili. Sisi wenye kipato cha kawaida tukaguna. Ni pesa nyingi hizo kwetu. Ni pesa nyingi sana kwa Mtanzania wa kawaida.

Mwisho mwisho alihamia Yanga. Baada ya misimu michache Yanga waliachana naye katika dirisha kubwa lililopita la uhamisho. Ni baada ya kushindwa kumpa changamoto timilifu kiungo mkongwe wa Uganda, Khalid Aucho. Kwa mujibu wa Wikipedia Aucho ana miaka 32 wakati Mkude ana miaka 33. Hata hivyo nilianza kumsikia Aucho muda mrefu kabla ya Mkude.

Sasa hivi Jonas simsikii tena. Nadhani hana timu. Msimu huu sijamsikia tena. Hata akirudi uwanjani sidhani kama atakuwa Mkude yule wa Simba. Kitu ambacho hatufahamu ni kitu gani atafanya kama ameamua kutundika daluga. Hatujui kama atakuwa kocha, mfanyabiashara au mchambuzi. Kwa kazi hizi tatu labda kazi ya biashara inaweza kumpatia pesa nzuri. Hizi nyingine hata kina Rio Ferdinand haziwalipi kama wakati ule wanacheza soka.

Mashabiki kama kawaida yao wameachana na Mkude sasa hivi wamehamia kwa viungo wengine wanaotamba sasa. Kwa wachezaji wa ndani nadhani wamehamia katika kizazi cha Morice Abraham. Aliingia Simba kimya kimya kama kivuli, lakini sasa anatamba. Na jinsi mashabiki wetu walivyo wanafiki unaweza kudhani kwamba Morice ni mchezaji mpya kwao.

Mara kadhaa ameichezea Taifa Stars mbele ya macho yao lakini walikuwa hawamzingatii kwa sababu alikuwa hachezi Simba na Yanga. Morice ni yule yule tu. Kipaji maridhawa. Pasi nzuri. Umiliki na utulivu mkubwa wa mpira miguuni. Ufupi wake unampa mnyumbuliko mzuri katikati ya uwanjani. Sasa hivi watu wanamzingatia kwa sababu anacheza Simba.

Februari mwaka jana nilienda naye Indonesia akiwa katika kikosi cha timu ya taifa ambacho kilienda kucheza mechi ya kirafiki na timu ya taifa ya Indonesia. Aling'ara sana kiasi kwamba mawakala walimfukuzia kwa karibu. Nilipoandika habari ile katika mitandao ya kijamii hakuna aliyejali kwa sababu wakati ule alikuwa hachezi Simba wala Yanga. Leo ukiandika vile kila mtu atajali.

Kama kuna wachezaji ambao Morice anapaswa kuomba ushauri kwao basi ni hawa hawa Chuji na Mkude. Watamwambia majuto yao au mafanikio yao. Hukumu zipo hapa hapa duniani. Wao wanaweza kuwa mwalimu mzuri kwa Maurice kuhusu kipaji chake, suala la nidhamu na suala la kipato.

Lakini kwa sasa ninachoweza kuwausia wachezaji wengi wa Kitanzania ni mambo mawili. Kwanza kabisa ni nidhamu ya kazi yao. Wengi hawana nidhamu na huwa wanajifanya wasela wakati wakiwa katika ubora wao. Mashabiki wetu pamoja na mabosi wa mpira ni wazuri sana katika kumdekeza mchezaji muhimu uwanjani. Hata kama kocha anajaribu kurekebisha nidhamu kwa mchezaji bado mashabiki na viongozi watamdekeza wakitaka lazima apangwe.

Lakini jambo la pili ni kwa wachezaji kutokuwa mashabiki katika timu wanazochezea. Wanapaswa kuwa wachezaji wa kulipwa hasa ambao wana menejimenti zinazoangalia maslahi yao na pia kuangalia fursa zinazojitokeza kama vile kuhamia katika timu yenye maslahi zaidi au kucheza soka katika klabu ya nje yenye maslahi zaidi. Tatizo wachezaji wetu huwa wanajifanya mashabiki wa timu zao.

Wengi wamepotea kwa kucheza kinazi zaidi badala ya kuzingatia weledi katika kazi zao. Matokeo yake kuna wachezaji wa zamani ambao hadi leo wanazidai klabu zao baada ya wakati ule kuingia katika uongo wa kudanganywa kusaini bila ya mikataba. Mpira unapoisha hakuna anayekupa thamani. Wachezaji wetu wa sasa wajifunze makosa ya wachezaji wa zamani. Hakuna anayekupa thamani kama haujithamini.

Wakati mwingine unashangaa kuona wachezaji wetu wa zamani wanahitaji huruma kutoka kwa viongozi wa klabu zao au mashabiki kama vile wakati wanacheza mpira walikuwa hawalipwi. Wasichojua ni kwamba uhusiano baina ya wao na klabu ulikuwa katika mkataba tu na si vinginevyo. Kwamba mchezaji alikuwa klabuni kama mfanyakazi mwingine tu. Kama dereva au mpishi wa timu.

Mpira unapoisha unahitaji kuwa na kipato kizuri kwa ajili ya kumudu kununua hata tiketi ya kuingia uwanjani. Kama wachezaji wote wa zamani watataka kuingia uwanjani bure nadhani klabu zitakuwa zinapata hasara. Kama wachezaji wote wa zamani watahitaji jezi za bure pindi zinapotolewa klabuni biashara itakwendaje?

Kitu kingine cha msingi zaidi kwa wachezaji wetu ni kupima mambo ambayo wanaweza kuyafanya kwa ufasaha pindi mpira utakapoondoka mguuni. Wengi wanafurahia wakati uliopo na hawaangalii wakati ujao. Kitu kibaya zaidi ni kwamba walitumia muda wao mwingi kucheza soka badala ya kwenda shule. Hauwezi kuwalaumu kwa sababu wasingeweza kufanya mambo mawili kwa wakati mmoja.

Hata kina Lionel Messi hawakwenda shule, lakini wakajikita katika kuifanya kazi yao kwa ufasaha zaidi kwa sababu hawakuwa na namna nyingine. Sisi unakuta mchezaji hana shule, lakini wala haithamini kazi yake. Wenzetu wanaithamini kwa sababu wanatafuta uwekezaji ambao utalipia fidia ya wao kutokwenda shule. Sisi mchezaji ambaye hakwenda shule ndio huyo huyo anaongoza kwa utovu wa nidhamu ndani na nje ya uwanja.