Jux: Kwa Priscilla ni kama zali tu

Muktasari:
- Jux mwenye umri wa miaka 35 ameoana na Priscilla (24) aliye muigizaji na filamu na tamthilia za kwenye televisheni pamoja uanamitindo na uwakala wa majumba huko kwao Nigeria, walifunga ndoa Februari 7 mwaka huu kabla ya kufanya sherehe kubwa huko Nigeria hivi karibuni.
MKALI wa muziki wa kizazi kipya nchini, Jux aliyefunga ndoa na Priscilla Ojo iliyogeuka kuwa gumzo nchini na Afrika kwa ujumla, amesema siku ya kwanza alipofanya uamuzi wa kutaka kuoa hakuwa na uhakika na uamuzi huo, kwani alihisi kama mkewe huyo hana mapenzi ya dhati na yeye.
Jux mwenye umri wa miaka 35 ameoana na Priscilla (24) aliye muigizaji na filamu na tamthilia za kwenye televisheni pamoja uanamitindo na uwakala wa majumba huko kwao Nigeria, walifunga ndoa Februari 7 mwaka huu kabla ya kufanya sherehe kubwa huko Nigeria hivi karibuni.
Akizungumza na Mwanaspoti, Jux alisema: “Katika kuoa nilikuwa mguu ndani mguu nje nikijuliza huyu mwanamke ananipenda kweli, hadi kufikia hatua ya kukubali kumuoa? Au ananipenda kwa kutaka kujulikana Tanzania ili aweze kufanya biashara zake kwa urahisi ama kujulikana Tanzania? Ila baada ya kukaa naye ndio nikagundua ananipenda kwa dhati na yuko siriazi nami na sio kitu kingine kama nilivyokuwa nadhani,” alisema Jux.
Aidha, alisema hatarudi nyuma katika sanaa ya uimbaji kama mitazamo ya baadhi kwamba msanii akioa anapotea kwenye game.
“Mimi nadhani nitakuwa tofauti kidogo na wale baadhi ya wasanii pindi wanapooa wanakuwa kimya kwenye kazi zao za sanaa, hivi ninavyokwambia niko mbioni kuachia kazi mpya.”