Harmonize anatekeleza kuzifufua ndoto zake

Muktasari:
- Hatua hii mpya inaonekana kama mkakati wa Harmonize kuzifikia ndoto zake chini ya Konde Music ambayo nguvu yake ilishashuka licha ya hapo awali mashabiki wengi kuamini ingeleta mapinduzi katika tasnia ya muziki Bongo kwa kuibua vipaji vingi.
MWIMBAJI wa Bongo Fleva, Harmonize ameimarisha rekodi lebo yake yake ya Konde Music Worldwide kwa kuongeza watendaji kadhaa akiwemo Sandra Brown ambaye aliwahi kuwa meneja wa Mbosso pindi tu aliposainiwa WCB Wasafi.
Hatua hii mpya inaonekana kama mkakati wa Harmonize kuzifikia ndoto zake chini ya Konde Music ambayo nguvu yake ilishashuka licha ya hapo awali mashabiki wengi kuamini ingeleta mapinduzi katika tasnia ya muziki Bongo kwa kuibua vipaji vingi.
Novemba 2023 Harmonize alisema Konde Music itasaini wasanii wapya kuziba nafasi za waliondoka pamoja na kumtambulisha meneja wake mpya, hilo moja ametimiza bado hilo la kusaini wasanii wapya maana lebo kwa sasa ina mwanamuziki mmoja pekee.
Harmonize alitangaza kufungua Konde Music hapo Oktoba 10, 2019 ikiwa ni muda mfupi tangu kuachana na WCB Wasafi, lebo yake Diamond Platnumz ambayo ndio ilimtoa kimuziki mwaka 2015.

Mnamo Aprili 11, 2020 ndipo Konde Music walitangaza kumsaini msanii wa kwanza ambaye ni Ibraah aliyekuja na EP yake, Steps (2020) ikiwa na nyimbo tano, huku akiwashirikisha Joeboy, Skibii na Harmonize.
Ndani ya miaka mitano, Konde imeweza kusimamia wasanii sita ukimtoa Harmonize ambaye ndiye mmiliki, wasanii hao ni Ibraah, Country Boy, Anjella, Cheed, Killy na Young Skales kutokea nchini Nigeria.
Hata hivyo, lebo hiyo kwa sasa imesalia na msanii mmoja tu ambaye ni Ibraah baada ya mwaka 2023 wasanii wote kuondoka kwa sababu mbalimbali, wapo walioomba kuondoka na wengine walipewa mkono wa kwaheri.
Kipindi Konde Music inaanza ilionekana inakuja kuleta ushindani mkubwa kwa WCB Wasafi ila sasa mambo yamebadilika, Diamond aliwahi kukiri kuwa Harmonize alimpa changamoto kwa kuwatambulisha wasanii wapya wawili, Anjella na Ibraah.

Kufanya kwao vizuri kulipelekea Ibraah kupewa tuzo na kipindi cha Empire cha E FM Radio kama Msanii Bora Chipukizi kwa mwaka 2020 ingawa msanii huyu hajawahi kushinda tuzo yoyote kubwa ya muziki Tanzania.
Diamond alitoa kauli hiyo wakati Anjella ameshaondoka Konde Music na kubaki Ibraah pekee yake, huku lebo hiyo ikiwa imehama katika jengo walilopanga kama ofisi hapo awali huku kukiwa na maneno mengi.
Harmonize alisema baada ya yeye na Ibraah kusalia utakuwa ni mwendo wa kazi mfululilizo, na ndivyo ilivyokuwa hasa mwaka uliopita ambapo Ibraah alitoa kazi nyingi ikiwepo EP yake ya pili, Air Piano (2024), pamoja na kufanya kolabo nyingi.
Ila bado sio kama mwanzo, wakati Ibraah anaanza alikuwa ni msanii wa kutoa kazi kila wakati, hakuwahi kukaa kimya muda mrefu, Konde Music nayo ilionekana kudhamiria kufanya jambo kwa msanii huyo na tasnia kwa ujumla.
Utakumbuka awali wasanii wa Konde Music walitoa albamu na EP pamoja na kupewa magari, sasa mashabiki wanajiuliza ile nguvu ya Harmonize kuwekeza katika muziki mbona imepungua kwa kiasi kabla ya kufikia mafanikio makubwa kama WCB Wasafi?.
Country Wizzy aliachia EP yake, The Father (2020) yenye nyimbo saba, huku Seyi Shay, Snymaan, Skales na Harmonize wakishirikishwa.

Ibraah alitoa albamu moja, The King of New School (2022) yenye nyimbo 17 na kuwashirikisha Maud Elka, Christian Bella, L.A.X, Waje, AV, Roberto na Bracket.
Na kwa upande wa Cheed na Killy waliojiunga Konde Music hapo Septemba 2020 wakitokea King’s Music ya Alikiba nao kila mmoja alitoa EP yake na Harmonize kushirikishwa zote, Cheed alitoa, Endless Love (2022) na Killy, The Green Light (2022).
Vilevile Konde Music waliwapatia magari wasanii wake, Julai 2021 Harmonize alimpatia gari Angella aina ya Crown, hiyo ni baada ya Ibraah na Country Wizzy kupatiwa magari aina hiyo, pia Meneja wa Ibraah, Jose wa Mipango naye alipatiwa gari lake.
Hata hivyo, kipindi Country Wizzy anaachana lebo hiyo Januari 2022 alirudisha gari hilo, Harmonize alisema ilikuwa ni sawa maana kuna wasanii wengine wanauhitaji wa gari hilo ila baadaye hata kina Angella nao walirudisha gari waliyopewa.

Licha ya juhudi zote hizo, bado Konde Music na wasanii wake hawakuwa tishio kama ilivyotarajiwa, ndipo Harmonize akapunguza kikosi kazi na sasa anataka kurudi upya kwa lengo la kuziishi ndoto zake.
Ikumbukwe Harmonize ni msanii wa pili kuachana na WCB Wasafi na kuanzisha lebo yake baada ya Rich Mavoko aliyekuja na Bilionea Kid, kisha Rayvanny akaibuka na Next Level Music (NLM) yenye msaanii mmoja, Mac Voice ila anatajwa kuikimbia NLM kimyakimya.