Senegal yaifumua Iraq 5-0, yafufua matumaini ya kutinga mtoano
Muktasari:
- Licha ya ushindi huo mkubwa, Senegal italazimika kusubiri matokeo ya makundi mengine ili kujua kama itafanikiwa kuingia hatua ya mtoano kama moja ya timu bora zilizomaliza nafasi ya tatu.
TIMU ya taifa ya Senegal imefufua matumaini ya kutinga hatua ya 32 Bora ya Kombe la Dunia 2026 baada ya kuichapa Iraq mabao 5-0 katika mchezo wa mwisho wa Kundi I uliochezwa Uwanja wa Boston, Jimbo la Massachusetts, Marekani.
Licha ya ushindi huo mkubwa, Senegal italazimika kusubiri matokeo ya makundi mengine ili kujua kama itafanikiwa kuingia hatua ya mtoano kama moja ya timu bora zilizomaliza nafasi ya tatu.
Senegal ilianza mchezo kwa kasi kubwa na kufungua ukurasa wa mabao dakika ya nne kupitia Habib Diarra aliyemalizia mpira uliotokana na kona ya Lamine Camara, huku beki Abdoulaye Seck akihusika katika kuanzisha shambulizi hilo.
Mambo yalizidi kuwa mabaya kwa Iraq dakika ya 13 baadaye baada ya nahodha wao, Rebin Sulaka, kumuangusha Sadio Mane akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga.
Mwamuzi Anthony Taylor hakusita kumuonyesha kadi nyekundu ya moja kwa moja na kuwaacha Iraq wakicheza pungufu kwa zaidi ya dakika 80.
Hata hivyo, kipa Ahmed Basil aliokoa faulo ya Mane, jambo lililoifanya Iraq kuwa bado mchezoni licha ya kucheza wakiwa 10.
Kipindi cha pili kilikuwa cha upande mmoja baada ya Senegal kuongeza kasi. Ismaila Sarr alifunga bao la pili dakika ya 56 akimalizia pasi safi ya Lamine Camara, kabla ya kiungo Pape Gueye kupachika bao la tatu dakika ya 59.
Gueye, ambaye alitokea benchi na kuingia dakika ya 57, hakutosheka na bao moja kwani aliongeza la nne kwa shuti lingine kali dakika ya 71, baada ya kupokea pasi kutoka kwa Iliman Ndiaye.
Dakika ya 82, Ndiaye naye aliandika jina lake kwenye orodha ya wafungaji kwa shuti lililomshinda kipa Jalal Hassan aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Basil, na kuhitimisha ushindi mnono wa mabao 5-0.
Pape Gueye alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mechi baada ya kufunga mabao mawili na kuwa mhimili mkubwa wa ushindi huo.
Ushindi huo umeingia kwenye historia ya soka la Afrika kwani ni mkubwa zaidi kuwahi kupatikana na timu ya Afrika katika fainali za Kombe la Dunia.
Senegal yenye pointi tatu, inasikilizia matokeo ya timu zingine katika kuwania kufuzu mtoano kupitia timu nane zitakazomaliza nafasi ya tatu bora kwenye kila kundi ambapo sasa ni ya tano kwenye msimamo huo.
Kwa upande wa Iraq, ilikuwa ni mwisho mbaya wa kampeni yao ya pili katika historia ya Kombe la Dunia.
Timu hiyo chini ya kocha Graham Arnold ilimaliza hatua ya makundi bila hata pointi moja, ikiendeleza rekodi ya kutoshinda wala kupata sare katika mechi zote sita ilizowahi kucheza kwenye fainali za Kombe la Dunia.