Senegal walipigaje pale? Cheki namba zinavyoongea
Muktasari:
- Lakini, ile ‘come back’ ya mabao 5-0 dhidi ya Irak, jana, imebadili fikra na mawazo waliobeza mwanzo na sasa kila kitu kipo hadharani wakisikilizia tu nini kitafuata baada ya kila timu katika kila kundi walipomaliza mechi zao usiku wa kuamkia leo.
TORONTO, CANADA: SENEGAL ni wa ajabu sana! Walibezwa mechi mbili za mwanzo ambazo waliambulia matokeo ya fedheha katika Kombe la Dunia 2026, baada ya kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Ufaransa kisha kunyukwa nyundo 3-2 na Norway katika kundi I, jambo ambalo lilionyesha kana kwamba mabingwa hao wa Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 wangemaliza na vichapo.
Lakini, ile ‘come back’ ya mabao 5-0 dhidi ya Irak, jana, imebadili fikra na mawazo waliobeza mwanzo na sasa kila kitu kipo hadharani wakisikilizia tu nini kitafuata baada ya kila timu katika kila kundi walipomaliza mechi zao usiku wa kuamkia leo.
Kabla ya mechi dhidi ya Irak, Senegal walijua kuwa walihitaji ushindi mkubwa, na waliufanikisha kwa kuichakaza mabao 5-0 na kukisogeza karibu zaidi na kikapu cha hatua ya 32 bora kupitia kundi la washindi wa nafasi ya tatu wenye matokeo bora wanane.
Mabao ya Pape Gueye katika Uwanja wa Toronto yaliyokuwa ya kuvutia kipindi cha pili yalifuata ya Habib Diarra na Ismaïla Sarr, huku Iliman Ndiaye naye akifunga bao zuri dakika nane kabla ya mwisho wa mchezo. Hadi jana walikuwa nafasi ya tano katika jedwali la timu bora za washindi wa tatu, na kwa hali ilivyo, huenda wakakutana na England tena katika hatua inayofuata itakayochezwa Atlanta, Marekani, Julai Mosi.
Senegal walistahili ushindi huo kwa sababu walimaliza mchezo wakiwa na mashuti 28 na mategemeo ya kufunga bao ya 3.03, dhidi ya Irak waliokuwa na 0.18 kutokana na mashuti sita pekee waliyopiga.
NAMBA BAADA YA MCHEZO
Senegal imekuwa taifa la kwanza la Afrika katika historia kufunga mabao matano katika mchezo mmoja wa Kombe la Dunia. Mabao hayo yalifungwa na Habib Diarra dakika ya nne, Ismaila Sarr (56), Pape Gueye (59 na 71) na Iliman-Cheikh Ndiaye (82).
Timu hiyo pia imeandika ushindi mkubwa zaidi kuwahi kupatikana kwa taifa la Afrika katika Kombe la Dunia, na kwa ujumla ushindi wake mkubwa zaidi katika mashindano makubwa (Afcon au Kombe la Dunia).
Irak kwa upande wake sasa imepoteza mechi zote sita ilizocheza katika Kombe la Dunia, ikiwa ni moja ya mataifa yenye rekodi mbaya zaidi ya asilimia 100 ya kupoteza pamoja na El Salvador na Haiti. Kwa upande wa Senegal imepata clean sheet ya kwanza katika Kombe la Dunia tangu mchezo wao wa kwanza dhidi ya Ufaransa 2002 walioshinda bao 1-0, na hivyo kukata mfululizo wa mechi 13 bila kutopata clean sheet.
Nyota wa nchi hiyo, Ismaila Sarr, Pape Gueye na Iliman Ndiaye wote walifunga na pia kutoa pasi za mabao katika mchezo dhidi ya Irak ikiwa ni mara ya kwanza kwa timu kuwa na wachezaji watatu waliofanya hivyo katika mchezo mmoja wa Kombe la Dunia tangu Ujerumani ilipofanya hivyo dhidi ya Brazil 2014 katika ushindi wa mabao 7-1.
Si hivyo tu, Sarr sasa ndiye mfungaji bora wa Senegal kwenye Kombe la Dunia akiwa na mabao manne na ana jumla ya mchango wa mabao matano (kafunga manne, asisti moja). Pia amekuwa mchezaji wa pili wa Senegal kufunga mabao matatu katika shindano moja la Kombe la Dunia baada ya Papa Bouba Diop 2002.
Gueye kwa upande wake amekuwa mchezaji wa pili kutoka Afrika kufunga mabao mawili kama mchezaji wa akiba katika mchezo wa Kombe la Dunia, baada ya Roger Milla wa Cameroon aliyefanya hivyo mara mbili 1990 (dhidi ya Romania na Colombia).
Ukiachana na hayo, timu ya Sunderland sasa ina wachezaji watano tofauti waliofunga mabao katika Kombe la Dunia 2026 ambao ni Habib Diarra, Brian Brobbey, Granit Xhaka, Wilson Isidor na Nilson Angulo, na ni Tottenham Hotspur (2018) na Manchester United (2014) pekee ziliowahi kuwa na wachezaji wengi zaidi (sita kila moja).
MISRI VS IRAN
Mbali na mechi ya Senegal dhidi ya Irak iliyopigwa Canada, wawakilishi wengine wa Afrika walikuwa uwanjani Seattle, Marekani ambako Misri iliyomaliza nafasi ya pili katika kundi G ilikipiga na Iran zikamalizana kwa kugawana alama mojamoja baada ya kufungana bao 1-1.
Lakini, katika mchezo huo pia kulikuwa na namba fulani ambazo zimeingia katika rekodi ingawa Misri ilihakikisha nafasi yake ya kufuzu hatua ya mtoano kutokana na matokeo yaliyokuwa yamekamilika kabla ya mechi hiyo.
Lakini, kwa ujumla hii ni mara ya kwanza kwa Misri kufuzu hatua ya mtoano baada ya kucheza hatua ya makundi katika historia ya Kombe la Dunia, ilhali Iran ni taifa la tatu kutoka Asia kumaliza hatua ya makundi bila kupoteza, likiungana na Japan (2002 na 2026) na Korea Kusini (2002).
Misri (dakika 4:26) na Iran (13:13) kila moja ilifunga bao la mapema zaidi kuwahi kufungwa katika historia ya Kombe la Dunia kwa mataifa yao, huku beki wa Iran, Ramin Rezaeian sasa ana mabao matatu, akimpita Mehdi Taremi (2) kuwa mfungaji bora wa nchi hiyo kwenye Kombe la Dunia. Nyota huyo pia ana jumla ya mchango wa mabao manne (kafunga matatu, asisti moja), rekodi ya juu zaidi kwa Iran.
Ukiachana na hilo, straika wa Misri, Mahmoud Hassan (Trezeguet) alihusika katika bao (asisti), ukiwa ni mchango wake wa pili katika mechi mbili za Kombe la Dunia 2026 (kafunga bao moja na asisti moja, tofauti na 2018 ambapo hakuwa na mchango wowote katika mechi tatu. Naye Mostafa Shobeir amekuwa kipa wa pili wa Misri kuokoa penalti katika Kombe la Dunia, baada ya Essam El Hadary 2018 dhidi ya Saudi Arabia.
Kwa upande mwingine, Iran ilimaliza mchezo na matarajio ya bao ya 1.94, ikiwa ni ya juu zaidi katika historia yao ya Kombe la Dunia, huku mechi hiyo katia ya nchi hizo mbili za Kiarabu ikiwa na kadi nyingi za njano (nne) katika kipindi cha kwanza, tukio la kwanza kwa Kombe la Dunia 2026.
CAPE VERDE VS SAUDI ARABIA
Gemu nyingine ya moto iliyokuwa na wawakilishi wa Afrika ni ile ya Cape Verde dhidi ya Saudi Arabia, ambapo pia Waafrika hao walifuzu barua ya 32 bora wakishika nafasi ya pili katika kundi H licha ya suluhu waliyoipata.
Lakini, wakati unashangazwa na Cape Verde taarifa ikufikie kuwa ni taifa la kwanza jipya katika mashindano hayo kufuzu kutoka hatua ya makundi tangu Slovakia 2010, na la kwanza kutoka Afrika tangu Ghana 2006. Pia Cape Verde kumiliki sare tatu inakuwa timu ya kwanza mpya kwenda mtoano bila kupoteza mechi zake tatu za makundi tangu Senegal ilipofanya hivyo 2002.
Kwa upande wake, Saudi Arabia imefeli kufuzu hatua ya mtoano katika mashindano sita kati ya saba ya mwisho ya Kombe la Dunia, lakini pia imemaliza na rekodi ya chini ya mashuti (17) na matarajio ya kufunga bao (1.2) katika historia yao ya mashindano.
Huku nyuma kipa Vozinha wa cape Verde ni miongoni mwa makipa wachache zaidi wenye miaka 40 waliowahi kuwa na clean sheet zaidi ya moja kwenye Kombe la Dunia, akiungana na Peter Shilton (England) na Dino Zoff (Italia).
Lakini, kiungo wa Cape Verde, Laros Duarte alitengeneza nafasi tatu katika mechi dhidi ya Saudi Arabia akitokea benchi, mmoja wa wachezaji walio na ubunifu mkubwa kutoka benchi katika mashindano hayo. Naye kiungo Mohamed Kanno wa Saudi Arabia aliibuka na mshindi mipambano 12 ya kugombea mpira hewani, moja ya idadi kubwa zaidi kwa mchezaji wa nchi hiyo katika Kombe la Dunia tangu 2006.