Maswali mazito yenye majibu magumu
Muktasari:
- Kutokana na mfumo mpya wa mashindano uliopanuliwa, timu 16 zinaondolewa baada ya mechi hizi za mwisho. Pamoja na kwamba timu nyingi tayari zimefuzu hatua ya mtoano, ni muhimu kuzingatia kwamba kulihitajika majibu katika maswali mazito. Haya ndiyo maswali makubwa yaliyojibiwa katika mechi zilizopigwa.
MIAMI, MAREKANI: HATUA ya makundi ya Kombe la Dunia ambalo ndilo kubwa zaidi kuwahi kufanyika inafikia tamati. Hata hivyo, bado kulikuwa na maswali mengi muhimu yaliyohitaji majibu katika mechi za mwisho za makundi.
Kutokana na mfumo mpya wa mashindano uliopanuliwa, timu 16 zinaondolewa baada ya mechi hizi za mwisho. Pamoja na kwamba timu nyingi tayari zimefuzu hatua ya mtoano, ni muhimu kuzingatia kwamba kulihitajika majibu katika maswali mazito. Haya ndiyo maswali makubwa yaliyojibiwa katika mechi zilizopigwa.
WAANDAAJI KUFUZU 32 BORA BILA KUFUNGWA
Kwa kawaida, Kombe la Dunia limekuwa likiandaliwa na nchi moja, na mara nyingi mwenyeji hunufaika kwa kucheza mbele ya mashabiki wake.
Lakini, safari hii, Canada, Marekani na Mexico zimemaliza hatua ya makundi huku Marekani na Canada zikimaliza kwa vipigo.
Canada, chini ya Jesse Marsch ilicheza dhidi ya Uswisi katika pambano la kuamua mshindi wa Kundi B baada ya timu zote mbili tayari kufuzu, lakini ikaishia kufungwa mabao 2-1, huku Marekani iliyomaliza hatua ya makundi kwa kucheza dhidi ya Uturuki ambao wamekuwa miongoni mwa timu zilizokatisha tamaa zaidi katika mashindano hayo ikiwachapa wenyeji hao kwa mabao 3-2.
Ni Mexico pekee ambayo bado haijafungwa wala kuruhusu bao.
HISPANIA WAMERUDI KWENYE UBORA?
Katika mshangao mkubwa wa mashindano, Hispania walishindwa kuifunga Cape Verde katika mechi ya kwanza Licha ya kumiliki mpira kwa asilimia 74.3 wakishindwa kutengeneza nafasi nyingi za wazi, huku kukosekana kwa Lamine Yamal katika kikosi cha kwanza kukionekana wazi.
Lakini, dhidi ya Saudi Arabia, Yamal alirejea na Hispania walionekana tofauti kabisa ambapo alifunga bao, huku Mikel Oyarzabal akifunga mawili. Ndani ya dakika 25 tayari walikuwa wanaongoza 3-0. Swali lililokuwapo kabla ya mechi iliyopigwa usiku wa kuamkia leo dhidi ya Uruguay ni kama kiwango hicho kilitokana na ubora wa Hispania au udhaifu wa Saudi Arabia.
Jibu inawezekana tayari umelipata.
UBELGIJI WATAENDELEA KUKATISHA TAMAA?
Enzi za “kizazi cha dhahabu” cha Ubelgiji zimekwisha. Baada ya sare dhidi ya Misri na Iran, kikosi hicho Rudi Garcia kabla ya mechi ya leo alfajiri dhidi ya New Zealand kilikuwa bado hakijapata ushindi wowote. Cha kushangaza zaidi ni kwamba hakijafunga bao lolote kupitia wachezaji wao; bao lao pekee limetokana na mchezaji wa timu pinzani kujifunga.
Dhidi ya Iran walipiga mashuti 23 bila kufunga, idadi kubwa zaidi kwa timu iliyoshindwa kupata bao katika Kombe la Dunia tangu 1994. Jibu la swali hili pengine unalo baada ya mechi iliyochezwa alfajiri hii.
VITA YA HAALAND DHIDI YA MBAPPE
Katika ngazi ya wachezaji binafsi, mashindano hayo yamekuwa yakiwazungumzia zaidi Lionel Messi na Kylian Mbappe katika mbio za kuvunja rekodi za mabao. Lakini, Erling Haaland pia amekuwa na mwanzo wa kuvutia akiwa amefunga mabao mawili katika kila moja ya mechi zake mbili za kwanza za Kombe la Dunia.
Na akifanya hivyo tena dhidi ya Ufaransa atakuwa mchezaji wa kwanza tangu 1954 kufunga mabao mawili au zaidi katika kila moja ya mechi zake tatu za kwanza za Kombe la Dunia. Kwa sasa Haaland na Mbappe wote wana mabao manne wakimfuatia Messi mwenye mabao matano.
Mbappe pia ameendelea kuandika historia, ambapo mabao mawili katika mechi iliyopita yamemfikisha kwenye jumla ya 16 katika mechi 16 za Kombe la Dunia, huku manne aliyofunga katika mashindano hayo yakimfanya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Ufaransa.
Ingawa Norway na Ufaransa tayari zimefuzu hatua ya mtoano, pambano kati ya Haaland na Mbappe linatarajiwa kuwa moja ya mechi zinazovutia , huku kila mmoja akitaka kuthibitisha kuwa ndiye nyota mkubwa zaidi wa kizazi chake.