Kocha Liverpool akanusha ishu ya Nunez

Muktasari:
- Ripoti kutoka Ureno wiki hii zilidai kwamba Benfica itapata mapato ya ziada pale Nunez atakapofikisha idadi ya mechi 60 akiwa ameanza katika EPL na Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa pamoja. Mshambuliaji huyo kutoka Uruguay kwa sasa amefikia mechi 59, hivyo akianza katika mechi moja tu, Liver itabidi ilipe pesa hiyo.
LIVERPOOL, ENGLAND: KOCHA wa Liverpool, Arne Slot amepuuza madai kwamba hajamchezesha Darwin Nunez katika mechi kadhaa kwa sababu ya kifungu kilichomo kwenye mkataba wake ambacho kinaitaka Liverpool kuilipa klabu yake ya zamani, Benfica, Pauni 5 milioni atakapocheza mchezo mwingine.
Ripoti kutoka Ureno wiki hii zilidai kwamba Benfica itapata mapato ya ziada pale Nunez atakapofikisha idadi ya mechi 60 akiwa ameanza katika EPL na Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa pamoja. Mshambuliaji huyo kutoka Uruguay kwa sasa amefikia mechi 59, hivyo akianza katika mechi moja tu, Liver itabidi ilipe pesa hiyo.
Minong’ono hiyo imeibuka baada ya Slot kutomchezesha katika mechi yoyote kati ya mechi mbili zilizopita za ligi..
Alipoulizwa kuhusu kifungu hiki kinachoripotiwa, Slot alisema: “Je, kila mara unawaamini waandishi wa habari wanachosema? Sio kila mara? Mimi pia siamini kila mara. Wakati mwingine unapaswa kuamini, lakini wakati mwingine ni bora usiamini kila kitu kinachoandikwa kuhusu wachezaji.”
“Hii ni jambo jipya kabisa kwangu na nimesema mara nyingi kwamba nafanya kazi katika klabu ambayo inanipa furaha.”
“Sijui kuhusu jambo hili ingawa kama kweli angeniambia(Mkurugenzi wa Michezo) kwamba ‘Kama utamchezesha, itatugharimu hivi’ lakini nafahamu hawezi kufanya hivyo, mimi na yeye hatujawahi kujadili jambo hili. Huenda ni kweli, lakini kama mwandishi wa habari anasema hivyo, tunapaswa... (kuchukulia kwa tahadhari).”
Hatma ya Nunez kuelekea msimu ujao bado haijulikani na anapewa nafasi kubwa ya kuondoka kwenye viunga vya Liverpool huku Al Nassr ya Saudi Arabia ikiwa moja ya timu zinazoweza kumsajili.