Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Gakpo apata pigo kambini Uholanzi ikiisubiri Morocco 32 Bora

Muktasari:

  • Mei mwaka huu, Gakpo na mpenzi wake Noa van der Bij, walitangaza kwamba walikuwa wanatarajia kupata mtoto wao wa pili wa kiume.

Mshambuliaji wa Liverpool, Cody Gakpo, amepata pigo akiwa kambini na kikosi cha Uholanzi baada ya kupokea taarifa za mtoto wake wa kiume aliyetarajiwa kuzaliwa Oktoba mwaka huu, kufia tumboni.

Mei mwaka huu, Gakpo na mpenzi wake Noa van der Bij, walitangaza kwamba walikuwa wanatarajia kupata mtoto wao wa pili wa kiume.

Hata hivyo, Noa amethibitisha kuwa mtoto wao huyo wa kiume aliyetarajiwa kuitwa Elijah, amefariki dunia akiwa bado tumboni.

Gakpo mwenye umri wa miaka 27, kwa sasa yupo kwenye majukumu ya kimataifa akiwa na timu ya taifa ya Uholanzi katika Fainali za Kombe la Dunia zinazofanyika Marekani, Canada na Mexico, huku Noa akiwa nchini Marekani kwa ajili ya kumsapoti mshambuliaji huyo wa Liverpool.

Mwezi Mei, wawili hao walichapisha ujumbe wa furaha kupitia Instagram wakitangaza kwamba walikuwa wanatarajia kumpata mtoto wao wa pili mwezi Oktoba mwaka huu, baada ya kupata mtoto wao wa kwanza, Samuel, kumpata mwaka 2024.

Lakini leo Jumamosi Juni 27, 2026, Noa ameweka ujumbe wa kusikitisha kupitia Instagram Stories akifichua kuwa ujauzito umeharibika.

Katika chapisho hilo, ameambatanisha picha yao wakishikana mikono juu ya blanketi na kofia ndogo ya mtoto, akiandika: "Kwa mioyo iliyovunjika, tunashiriki habari ya kusikitisha kwamba mtoto wetu wa kiume amefariki akiwa tumboni. Asanteni kwa upendo na msaada wenu. Elijah Raphael Gakpo. Atapendwa milele. Atabaki kuwa mwana wetu milele."

Katika ujumbe mwingine, Noa alichapisha picha ya mshumaa uliowashwa kanisani na kueleza: "Tulikwenda kanisani kuwasha mshumaa. Baadaye tulitembea hadi sehemu ya watoto kuchezea karibu na kanisa pamoja na mtoto wetu Samuel. Kulikuwa na mtoto mmoja tu pale, na jina lake lilikuwa Elijah.

"Hakungekuwa na ishara nzuri zaidi kutoka kwa Mungu. Alitukumbusha kwamba mtoto wetu mdogo hayuko mbali nasi kamwe."

Haijafahamika ni lini hasa ujauzito huo uliharibika, kwani hapo kabla Noa aliendelea kuchapisha picha mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii kwa muda mrefu.

Mwanzoni mwa Juni, alichapisha picha akiwa ameshika kinywaji juu ya tumbo lake la ujauzito, kabla ya kushiriki picha nyingine akiwa Texas na pia wakati wa mchezo wa kwanza wa Uholanzi dhidi ya Japan kwenye Kombe la Dunia.

Gazeti la Uholanzi la De Telegraaf liliripoti kuwa siku nne zilizopita Gakpo hakushuka kwenye basi la timu kuelekea mazoezini, bali baadaye alifika kwa gari tofauti. Shirikisho la Soka la Uholanzi (KNVB) lilieleza hakukuwa na kuchelewa bali kulikuwa na sababu muhimu iliyomfanya afike kwa njia hiyo.

Baada ya habari hizo kusambaa, mashabiki wa Liverpool walimiminika kwenye mitandao ya kijamii kumtumia Gakpo na familia yake salamu za pole.

Mmoja ameandika: "Tunatuma mawazo yetu, upendo na salamu za rambirambi kwa Cody Gakpo na familia yake kufuatia habari ya kusikitisha ya kumpoteza mtoto wao wa kiume. You'll Never Walk Alone."

Ujumbe huo ulitazamwa zaidi ya mara 213,000 kwenye mtandao wa X, huku ukijaa salamu za pole na ujumbe wa kuwafariji.

Shabiki mwingine ameandika: "Hakuna maneno ya kuelezea. Pole sana kwa Cody na familia yake. Huu ni maumivu yanayofanya kila jambo lingine lionekane dogo. Tuko pamoja nawe, Cody. Tunakutumia upendo wote duniani. Chukua muda wote unaouhitaji. You'll Never Walk Alone."

Uholanzi itashuka tena dimbani Juni 30 katika Kombe la Dunia dhidi ya Morocco kwenye Uwanja wa Monterrey nchini Mexico ikiwa hatua ya 32 bora. Mshindi wa mchezo huo atakutana na mshindi kati ya Afrika Kusini na wenyeji wenza Canada katika mchezo utakaochezwa Julai 4 huko Houston, Texas.

Gakpo tayari amefunga mabao mawili kwenye mashindano hayo mwaka huu, akiendelea kuonyesha kiwango bora akiwa chini ya kocha Ronald Koeman. Pia aling'ara kwenye Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar, kiwango kilichomsaidia kupata uhamisho wa kujiunga na Liverpool.