Prime
Vigogo Afrika waingilia dili la Sowah Yanga

Muktasari:
- Sowah tangu ajiunge na kikosi hicho dirisha dogo la Januari mwaka huu akitokea Al-Nasr Benghazi FC ya Libya, amefunga mabao 11 ya Ligi Kuu, akizidiwa mawili na kinara mshambuliaji nyota wa Yanga, Clement Mzize anayeongoza akitupia 13.
HAKUNA ubishi, straika wa Singida Black Stars, Jonathan Sowah ni kama ameshindikana kwa moto aliouonyesha kupitia mechi 11 za Ligi Kuu Bara akifunga mabao 11 na kiwango hicho kimezifanya timu mbalimbali kuanza kutunishiana misuli kuisaka saini yake kwa msimu ujao, jambo linaloongeza zaidi thamani aliyonayo.
Sowah tangu ajiunge na kikosi hicho dirisha dogo la Januari mwaka huu akitokea Al-Nasr Benghazi FC ya Libya, amefunga mabao 11 ya Ligi Kuu, akizidiwa mawili na kinara mshambuliaji nyota wa Yanga, Clement Mzize anayeongoza akitupia 13.
Sasa wakati nyota huyo akionyesha kiwango hicho, timu mbalimbali zimeonyesha uhitaji wa kuipata saini yake na mbali na Yanga inayoripotiwa tangu awali kumhitaji, nyingine ni Al-Hilal Omdurman ya Sudan na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza Sowah anahitajika na timu hizo na licha ya Yanga kufanya mazungumzo marakadhaa na wamiliki wake, ila inaelezwa Al Hilal iko tayari kuweka mzigo wa maana kumpata kwa ajili ya kuongeza nguvu yake ya ushambuliaji.
“Mbali na kiasi kikubwa cha fedha ambacho Al Hilal wanataka kuweka ila wanatumia ushirikiano uliopo, kwa sababu hata pia wachezaji kama Ibrahim Imoro na Serge Pokou tulivyowahitaji hawakuweka pingamizi,” kilisema chanzo kutoka kikosi hicho.
Hata hivyo, hivi karibuni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Singida Black Stars (CEO), Jonathan Kassano katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti mjini Singida, alinukuliwa akiweka wazi timu yoyote inayomhitaji mchezaji huyo iweke kiasi cha Sh5 bilioni. Thamani ambayo wachambuzi kadhaa wa soka wameipinga wakidai umri wa mchezaji huyo hauendani na thamani hiyo.
Sowah alijiunga na Al-Nasr Benghazi Januari 27, 2024, akitokea Medeama ya kwao Ghana, pia alionyesha kiwango bora na kuzivutia klabu mbalimbali ikiwemo Yanga baada ya kuwasumbua kwenye Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya makundi.
Akiwa na Medeama aliyojiunga nayo Januari 11, 2023, akitokea Danbort FC, alicheza michezo 20 ya Ligi Kuu ya Ghana na alifunga mabao 16, huku katika Ligi ya Mabingwa Afrika, alifunga matatu kwenye mechi zake saba alizochezea kikosi hicho.
Katika michuano ya FA ya Ghana alifunga mabao matatu katika michezo saba na Medeama na kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka, huku akijumuishwa kikosi cha mwisho cha Ghana kwenye fainali za Mataifa Afrika (AFCON) 2023, zilizofanyika Ivory Coast.