Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rekodi yamsubiri Mzize Ufaransa

Muktasari:

  • Meneja wa Habari wa Yanga, Ally Kamwe hivi karibuni alinukuliwa akieleza mshambuliaji huyo msimu ujao ataenda kucheza soka la Ufaransa kutokana na kiasi kikubwa cha fedha walichopata, licha ya kutoweka wazi timu gani atakayoenda.

KIWANGO bora kinachoonyeshwa na mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize kimezivutia timu mbalimbali kusaka saini yake, huku ikielezwa nyota huyo anayeongoza kwa mabao ya Ligi Kuu Bara akiwa na 13 anakaribia kujiunga na miamba kutoka Ufaransa.

Meneja wa Habari wa Yanga, Ally Kamwe hivi karibuni alinukuliwa akieleza mshambuliaji huyo msimu ujao ataenda kucheza soka la Ufaransa kutokana na kiasi kikubwa cha fedha walichopata, licha ya kutoweka wazi timu gani atakayoenda.

Mwanaspoti linajua Yanga iko katika hatua nzuri ya mazungumzo na mawakala wa Olympique Lyonnais na AS Saint-Etienne zinazoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1). Na kama dili hilo litatiki Yanga itafanya biashara ya mabilioni ya shilingi na kuweka rekodi ya kuwa klabu ya kwanza Tanzania kuuza mchezaji nje kwa gharama na faida kubwa zaidi.

“Siwezi kuitaja timu lakini kuna mazungumzo na Yanga tunapata Sh5 bilioni, msimu ujao Mzize atacheza Ligi Kuu Ufaransa, kama kuna timu ina kiasi hicho ilete kwa sababu ndiyo mauzo halisi ya mshambuliaji wetu hadi sasa,” alinukuliwa Kamwe.

Mwanaspoti linajua ni uhakika Mzize atauzwa kama ilivyo kwa Aziz Ki atakayeenda FAR ya Morocco.

“Saint-Etienne ni miongoni mwa timu ziliyoonyesha nia ya kumhitaji ila hata Lyonnais imeonyesha uhitaji hivyo, kwa sasa ni ngumu kueleza wazi ni wapi atacheza kwa sababu msimu haujaisha japo mazungumzo yanaendelea,” kilisema chanzo chetu.

Chanzo hicho kilieleza, jambo kubwa ambalo viongozi wanazingatia ni kuhakikisha wanamtafutia nyota huyo timu itakayompa manufaa makubwa katika maisha yake, hasa masilahi yake binafsi na kumfungulia milango ya kuonekana zaidi Ulaya.

Miamba hiyo ya Ufaransa sio ya kwanza kujitokeza kuwania saini ya nyota huyo kwani hivi karibuni, Wydad Casablanca ya Morocco na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini nazo pia zilionyesha nia ya kumhitaji mwanzoni mwa msimu kabla ya kubakia.

Awali ilidaiwa Kaizer Chiefs inayonolewa na aliyekuwa Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi aliyempandisha na kumpa pia nafasi zaidi, iliweka Dola 200,000 sawa na Sh542.3 milioni, ofa ambayo mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu waliitupilia mbali.

Kwa upande wa Wydad Casablanca ambayo awali ilikuwa ikifundishwa na Kocha Rhulani Mokwena wa Afrika Kusini nayo iliweka kitita cha Dola 100,000 (Sh271.1 milioni) huku viongozi wa Yanga wakihitaji Dola 1 milioni sawa na zaidi ya Sh2 bilioni.

REKODI ZAKE

Katika msimu wa kwanza nyota huyo, 2022-2023, alikuwa sehemu ya kikosi kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu na alichangia upatikanaji wa mabao yake sita, akifunga matano na kuasisti moja kati ya 61 ya timu nzima.

Msimu huo, Yanga ilifika hadi fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kukosa ubingwa kwa faida ya bao la ugenini mbele ya USM Alger ya Algeria kufuatia sare ya jumla ya mabao 2-2, ikichapwa nyumbani 2-1, kisha ugenini kushinda 1-0.

Msimu wa pili wa 2023-2024, Mzize alichangia mabao 13, baada ya kufunga sita na kuasisti saba kati ya 71 ya kikosi hicho kizima, kilichotwaa tena ubingwa wa Ligi Kuu Bara ukiwa ni wa tatu mfululizo kufuatia kukusanya pointi zake 80.

Katika misimu mitatu, huenda huu ndio ukawa bora zaidi kwa mshambuliaji huyo kwani hadi sasa amechangia mabao 16 ya Ligi Kuu Bara kati ya 68, yaliyofungwa na kikosi kizima, ambacho kinaongoza kikiwa na pointi 70, baada ya kucheza mechi 26.

Ikiwa Mzize atauzwa, itakuwa kama aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Mkongomani Fiston Mayele aliyeuzwa Julai 30, 2023 kwenda Pyramids ya Misri, baada ya kuonyesha kiwango bora tangu alipojiunga nao akitokea AS Vita Club ya kwao DR Congo.

Mayele msimu wa 2022-2023 katika Ligi Kuu Bara aliibuka mfungaji bora baada ya kutupia mabao 17, akiwa sawa na aliyekuwa nyota wa Geita Gold na Simba, Mrundi Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’, jambo lililoonyesha wazi ni mshambuliaji hatari zaidi.

Kama haitoshi, Mayele msimu huo akaipeleka Yanga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na licha ya kukosa ubingwa mbele ya USM Alger ya Algeria kwa faida ya bao la ugenini, ila alikuwa pia mfungaji bora wa michuano hiyo akifunga mabao saba.

Kutokana na kiwango cha Mzize anachoendelea kukionyesha hadi sasa, ni wazi mshambuliaji huyo huenda akaondoka kwa ajili ya kutafuta changamoto sehemu nyingine, huku ikielezwa miamba wa Ufaransa ni miongoni mwa wanaoihitaji sana saini yake.