Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mechi nne za uamuzi mgumu Yanga

Muktasari:

  • Uamuzi huo ni wa kufanya mabadiliko ya benchi linaloongozwa na Kocha Miloud Hamdi.

YANGA inasikilizia mechi nne zilizobaki za Ligi Kuu Bara kufanya uamuzi mgumu ndani ya benchi lake la ufundi.

Uamuzi huo ni wa kufanya mabadiliko ya benchi linaloongozwa na Kocha Miloud Hamdi.

Licha ya kuiongoza Yanga kwenye mechi tisa za Ligi Kuu Bara akishinda nane na sare moja, lakini kwa hali ilivyo Hamdi ni kama anahesabu siku za kubaki kikosini.

Mbali na ligi, pia Hamdi ameifikisha Yanga nusu fainali ya Kombe la FA, ambapo ipo katika njia nzuri ya kutetea mataji mawili iliyobeba msimu uliopita.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga kimeliambia Mwanaspoti kuwa, licha ya matokeo mazuri inayoyapata lakini hairidhishwi na mbinu za kocha huyo, hivyo imefanya makubaliano ya kuanza mchakato wa kumtafuta mbadala wake.

“Makubaliano ya pande zote mbili yamefanyika kilichobaki ni msimu kukamilika ili kuangalia namna ya kumpata kocha mwingine ambaye ataendana na kasi ya kikosi chetu,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:

“Hamdi si kocha mbaya, lakini uongozi unaona msimu ujao tuwe na kocha mwingine ambaye ataibadilisha zaidi timu kiuchezaji na kufanya makubwa kimataifa. Kile alichokifanya Hamdi hadi sasa ndani ya timu kitabaki kama kumbukumbu na tunatambua mchango wake.”

Kuhusu mikakati ya kocha mpya, chanzo hicho kilisema mchakato unaendelea huku mabosi wakipambana kuona wanaumaliza msimu vizuri kwa kutetea mataji.

“Mchakato wa mbadala wa Hamdi upo kwenye mikakati, kilichopo sasa ni kupambania mataji yote yaliyo mbele yetu na tunaamini hilo linawezekana kutokana na aina ya kikosi tulichonacho,” kilisema chanzo.

Hamdi aliyechukua mikoba ya Sead Ramovic, ameiongoza Yanga kwenye mechi tisa za Ligi Kuu Bara - timu hiyo ikishinda nane na sare moja, ikifunga mabao 26 na kuruhusu matatu, huku ikiambulia ‘clean sheet’ sita.

Hamdi ameiwezesha Yanga kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kufikisha pointi 70, timu hiyo ikicheza mechi 26, bado nne kumaliza msimu ambapo inapambana kutetea ubingwa.

Yanga ndiyo mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara ikichukua ubingwa huo mara tatu mfululizo, hivyo msimu huu inalisaka taji la nne mfululizo ambalo litakuwa la 31.

Mechi nne za ligi zilizobaki kwa Yanga ni dhidi ya Namungo (nyumbani), Tanzania Prisons (ugenini), Dodoma Jiji (nyumbani) na Simba (nyumbani).

Hivi karibuni, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, alisema wameanza kufanya maboresho ya timu kwa ajili ya msimu ujao baada ya kujihakikishia mapema nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Tumeanza kuboresha timu yetu kwa ajili ya msimu ujao, maboresho ya kwanza ni kubakisha nyota tulionao kwa mujibu wa ripoti ya mwalimu, wale ambao watataka kuondoka, tutaangalia kwa maslahi ya klabu nani tumuondoe, lakini malengo makubwa ni kutengeneza timu ya msimu ujao kwa sababu tayari tuna tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa,” alisema Kamwe.