Junguni United yafunga mjadala wa iliyowatimua

Muktasari:
- Wachezaji hao saba waliotimuliwa kwa tuhuma hizo ni; Salum Athumani ‘Chubi’, Ramadhan Ally Omar ‘Matuidi’, Abdallah Sebastian, Danford Mosses Kaswa, Bakari Athumani ‘Jomba Jomba’, Rashid Abdalla Njete na Idd Said Karongo, huku kampuni ya uwakili inayowasimamia katika shauri hilo ni The Lord Whiteman & Company Advocates ya jijini Dar es Salaam chini ya wakili Kasigwa Ayoub.
SIKU tatu tu tangu Junguni United iliyopo Ligi Kuu ya Zanzibar kutangaza kuwafukuza wachezaji saba kwa tuhuma za kubeti na wachezaji hao kujibu mapigo kupitia kampuni ya uwakili ilitaka waombwe radhi ndani ya siku 14 na kulipwa fidia ya Sh300 milioni, klabu hiyo imesema imefunga mjadala huo.
Junguni inayoshika nafasi ya 12 katika msimamo wa ZPL ikiwa miongoni mwa timu nne zilizopanda daraja msimu huu sambamba na vinara wa ligi hiyo, Mwembe Makumbi, Telekeza na Inter Zanzibar ilisimamisha wachezaji hao kwa tuhuma za kubeti katika mechi mbili za Ligi Kuu dhidi ya Malindi na New City, lakini wachezaji wakakimbilia kwa mwanasheria kwa madai wamepakaziwa na hawakuitwa kujitetea kabla ya kupewa adhabu hizo zilizowafanya wapoteze haki kama wachezaji wa timu hiyo.
Wachezaji hao saba waliotimuliwa kwa tuhuma hizo ni; Salum Athumani ‘Chubi’, Ramadhan Ally Omar ‘Matuidi’, Abdallah Sebastian, Danford Mosses Kaswa, Bakari Athumani ‘Jomba Jomba’, Rashid Abdalla Njete na Idd Said Karongo, huku kampuni ya uwakili inayowasimamia katika shauri hilo ni The Lord Whiteman & Company Advocates ya jijini Dar es Salaam chini ya wakili Kasigwa Ayoub.
Wachezaji hao kupitia wakili huyo wametoa siku 14 kwa uongozi wa Junguni kuwaomba radhi na kuwalipa Sh300 milioni kwa kuwachafua kwa kitu wanachodai hawajakifanya na pia kutoitwa kusikilizwa kabla ya kutolewa na hukumu hiyo iliyotangazwa hadhani Ijumaa iliyopita.
Hata hivyo, Katibu wa Junguni, Suleiman Mwidani alipotafutwa jana ili kutoa ufafanuzi juu ya madai ya wachezaji hao, aliliambia Mwanaspoti uongozi wa timu hiyo umeshafunga mjadala wa suala hilo na hivyo hawezi kulizungumza katika vyombo vya habari tena.
“Sisi tukiwa uongozi wa Junguni United tumesitisha mawasiliano na chombo chochote cha habari kuzungumzia suala hilo kwa sababu kama barua zilishatoka na hapo tunaona ndio mwisho wetu wa kutoa taarifa ya aina yoyote,” alisema Mwidani kwa kifupi.
Hatua ya klabu hiyo kuwasimamisha na kuwafukuza wachezaji hao, imepokewa kwa hisia tofauti na baadhi ya wadau wa soka visiwani hapa, baadhi wakisema hata kama wachezaji hao wana hatia, bado walipaswa kusikilizwa kabla ya kupewa hukumu, ila ni kama kweli hawakupewa nafasi hiyo.
Mmoja ya wadau hao, Mohammed Said Kabwanga alisema “Huwezi kumhukumu mtu bila kumpa nafasi ya kumsikiliza, kwa tafsiri hii, ndani ya timu hiyo kutakuwa na tatizo, kabla ya kutoa taarifa ilibidi wakae chini na wachezaji wawahoji, wajiridhishe ndipo watoe taarifa kwa umma.”
Mdau mwingine, Ali Ibrahim alisema viongozi wa timu hiyo walipaswa kufikisha shauri lao kwa Mamlaka husika ili Bodi na Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) ili kufanyiwa uchunguzi madai yao na ndio watoe taarifa kwa umma wakiwa na uthibitisho wa tuhuma hizo.
Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Zanzibar, Issa Kassim alisema hadi jana walikuwa bado hawajapokea barua yoyote kutoka Junguni, hivyo hawawezi kufanya chochote kwa sasa hadi watakapoletewa mezani na kuipitia.
“Hadi sasa sisi bado hatujapata barua yoyote kutoka timu ya Junguni na hatuwezi kuchukua hatua bila kupata barua, tunaendelea kusubiri, tutatoa tamko kama bodi vuteni subira,” alisema Kassim alipotafutwa ili kufafanua juu ya hatua ya Junguni kuwafukuza wachezaji hao saba kwa tuhuma hizo.