Chipo na hesabu kali Ligi Kuu bara
Muktasari:
- Mtibwa ipo katika mtego mgumu na inakutana na timu zinazojikwamua kushuka daraja, ikiwemo Tanzania Prisons iliyopo nafasi ya pili kutoka mwisho na Namungo FC iliyopo nafasi ya 10, huku michezo yote miwili ikichezwa ugenini.
KOCHA Mkuu wa Mtibwa Sugar, Yusuf Chipo ana hesabu kali za mechi mbili zilizosalia kumaliza msimu huu, akisisitiza timu hiyo inahitaji kushinda zote ili kukusanya pointi sita zitakazoamua kama itacheza mtoano au kubaki salama.
Mtibwa ipo katika mtego mgumu na inakutana na timu zinazojikwamua kushuka daraja, ikiwemo Tanzania Prisons iliyopo nafasi ya pili kutoka mwisho na Namungo FC iliyopo nafasi ya 10, huku michezo yote miwili ikichezwa ugenini.
Endapo Mtibwa itashinda mechi hizo mbili, itafikisha jumla ya pointi 33, hali itakayoiweka katika nafasi ya kutegemea matokeo ya timu nyingine zilizo nafasi za chini katika msimamo wa Ligi Kuu.
Akizungumza kuhusu hali hiyo, Kocha Chipo amesema: “Plani A ni timu ishinde mechi zote ili tusiipe Prisons nafasi ya kutushusha chini, kusema ukweli ni mtihani mgumu unaohitaji hesabu kali.”
Ameongeza “Ninachowasisitiza wachezaji wapambane bila kukata tamaa. Jambo la msingi ni timu iendelee kusalia Ligi Kuu iwe kwa kucheza mtoano au la.”