Baada ya tizi la siku mbili, Simba yaifuata Berkane kimkakati

Muktasari:
- Msafara huo utaondoka hapa Casablanca kuanzia saa 11 jioni kwenda Berkane ambako mechi ya kwanza ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika itapigwa Mei 17, 2025.
KIKOSI cha Simba kilichokuwa kimejichimbia na kupiga tizi la siku mbili jijini Casablanca, Morocco, inajiandaa kuondoka ikiongoza msafara wa wachezaji, viongozi na watu wengine walio, katika msafara wa timu hiyo kwenda Berkane saa chache zijazo.
Msafara huo utaondoka hapa Casablanca kuanzia saa 11 jioni kwenda Berkane ambako mechi ya kwanza ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika itapigwa Mei 17, 2025.
Kabla ya safari hiyo nyota wa Simba, Shomari Kapombe, Che Fondoh Malone na Kibu Denis wameelezea maandalizi yao na kuwataka mashabiki wa Simba kutokuwa na hofu, kwani wana matumaini ya kufanya vizuri.
Wachezaji hao wamesema maandalizi yao yamekuwa ni mazuri na wana imani watatwaa ubingwa wa michuano hiyo ya Kombe la Afrika.
Meneja Habari na Mahusiano wa Simba, Ahmed Ally amesema kila kitu kimeenda vizuri jijini Casablanca na sasa wanaenda Berkane ambako mechi hiyo itachezwa.
Kocha Fadlu na benchi nzima limekuwa makini katika mazoezi ya timu hiyo yaliyoanza jana na kuendelea leo, ikiwamo kuwapa mbinu mastaa hususani makipa kaa lengo la kuepuka mtego wa Berkane iliyocheza mechi sita za Caf msimu huu, ikishinda zote na kufunga mabao 18 bila kuruhusu bao.