Ubora utaamua nani kuibuka kidedea fainali UEFA CL
Muktasari:
- Hata hivyo, Arsenal waliochukua ubingwa wa England wiki mbili zilizopita, huenda wakawa na faida ya kuwa katika fomu zaidi leo au wakaathiriwa na uchovu. Ni namna tu kila timu itakavyochanga karata zake.
BUDAPEST, HUNGARY: LEO inapigwa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya PSG na Arsenal, lakini ukifuatilia utagundua kwamba PSG ambao ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo walikuwa na muda mrefu wa kupumzika kuliko Arsenal hasa ikizingatiwa kwamba walibeba ubingwa wa Ufaransa (Ligue 1), takribani mwezi mmoja uliopita.
Hata hivyo, Arsenal waliochukua ubingwa wa England wiki mbili zilizopita, huenda wakawa na faida ya kuwa katika fomu zaidi leo au wakaathiriwa na uchovu. Ni namna tu kila timu itakavyochanga karata zake.
Ukiangalia takwimu za msingi pekee unaweza kudhani timu hizo mbili zilizofika fainali zimekuwa na misimu yenye ugumu sawa. Wakati Arsenal walipata mapumziko mazuri katika kipindi cha kiangazi kilichopita, PSG walikuwa Marekani wakicheza hadi fainali ya Kombe la Dunia la Klabu, mashindano yaliyoanza siku 14 tu baada ya wao kushinda Ligi ya Mabingwa Ulaya 2025.
Wachezaji wa timu hiyo hawakupata muda wa kutosha wa kupumzika baada ya mashindano hayo, kwa sababu msimu wa 2025-26 ulianza mwezi mmoja tu baada ya fainali hizo kumalizika kupitia mchezo wa UEFA Super Cup. Na utetezi wao wa taji la Ligue 1 ukaanza siku chache baadaye.
Toleo jipya la Kombe la Dunia la Klabu halikupokewa vizuri na mashabiki wengi, ambao nao walionekana kuchoshwa na soka kupita kiasi. Wengi walipenda kuona mapumziko ya kawaida ya kiangazi.
Mashindano hayo pia yaliweka mazingira magumu kwa timu zilizoshiriki, ambapo wachezaji walilazimika kucheza bila kupata muda wa kutosha wa kupumzika na kurejea katika hali bora ukilinganisha na wapinzani wao.
Hakuna njia ya kuthibitisha moja kwa moja kwamba wachezaji wa Chelsea waliathirika na ushindi wa Kombe la Dunia la Klabu na ndio maana msimu huu ulikuwa mgumu kwao Ligi Kuu England, lakini huenda si bahati mbaya kwamba walishinda mechi mbili tu kati ya sita za kwanza za ligi na baadaye kumaliza nafasi ya 10.
Kwa mfano, Cole Palmer alikuwa na msimu mbaya kiasi kwamba hata hakuitwa katika kikosi cha Kombe la Dunia cha mwaka huu.
Lakini tangu msimu mpya uanze kupitia Super Cup ya Agosti, hakuna kulinganisha mzigo waliobeba wachezaji wa PSG dhidi ya wale wa Arsenal.
Tangu mwanzo wa msimu wa 2025-26, Arsenal wamecheza mechi nyingi zaidi kuliko timu yoyote katika ligi tano kubwa za Ulaya kutokana pia na safari yao ndefu kwenye Carabao na FA. Na muhimu zaidi, tofauti na PSG, nafasi za kufanya mzunguko wa kikosi zimekuwa chache sana.
Kwa mfano, wakati PSG walipoanza msimu wa ndani dhidi ya Nantes, kikosi chao cha kwanza kilikuwa na wachezaji wawili tu walioanza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya miezi michache kabla.
Kuondoka kwa kipa Gianluigi Donnarumma kwenda Manchester City kulimaanisha mabadiliko yalikuwa lazima, lakini saba kati ya mabadiliko mengine manane ulikuwa uamuzi wa kocha Luis Enrique, huku jingine likisababishwa na adhabu ya Joao Neves.
Katika mchezo huo dhidi ya Nantes, huku matokeo yakiwa 0-0, Nuno Mendes, Achraf Hakimi, Ousmane Dembele, Desire Doue na Khvicha Kvaratskhelia waliingia kutokea benchi na kusaidia ushindi wa 1-0. Lakini kiwango hicho cha kuhitaji mastaa kutoka benchi hakijawa cha kila wiki.
Enrique amewapumzisha kabisa wachezaji wake muhimu katika mechi nyingi za Ligue 1. Hilo limeifanya PSG, licha ya kucheza mechi nyingi, kuingia fainali ya wiki hii ikiwa na wachezaji wake muhimu wakiwa fiti na wenye nguvu.
Baadhi ya mastaa wa PSG wamecheza dakika chache sana za ligi msimu huu. Mshindi wa Ballon d’Or Dembele alianza mechi 11 kati ya 34 za Ligue 1; Joao Neves, Mendes na Fabian Ruiz walianza mechi 13 kila mmoja; Kvaratskhelia 18; Doue na Hakimi 16, huku Marquinhos akianza 11.
Na si kwamba walikuwa wanaingia sana kutoka benchi pia hakuna hata mmoja aliyefikisha nusu ya dakika zote Ligue 1 msimu huu. Wengi wao waliwekwa tayari kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, mashindano ambayo Enrique anaonekana kuyapa umuhimu zaidi.
Kwa mfano, Mendes na Marquinhos wamecheza dakika nyingi zaidi Ligi ya Mabingwa Ulaya kuliko Ligue 1, licha ya PSG kucheza mechi 18 chache zaidi Ulaya.
Ingawa PSG wamekuwa na majeraha kadhaa, sababu kubwa ya hali hiyo ni mzunguko wa kikosi. Kvaratskhelia amekosa mechi tatu za ligi kutokana na majeraha, Marquinhos mbili, Mendes nane, Neves tisa na Dembele 10. Mara nyingi wamepewa mapumziko kwa makusudi.
Aidha, kikosi kikubwa cha PSG kinaundwa na wachezaji vijana au waliopo katika umri bora wa kucheza soka, ambao wana uwezo mkubwa wa kuhimili ratiba ngumu. Kuwapumzisha mara kwa mara mastaa kama Marquinhos kulikuwa muhimu, lakini wengine wengi waliachwa ili wawe tayari kwa kipindi hiki muhimu cha msimu.
Ubora wa PSG ndani ya Ligue 1 umemruhusu Enrique kudhibiti majeraha na kuzuia uchovu akipanga kwa umakini mzigo wa kazi kwa wachezaji kupitia mapumziko ya mara kwa mara. PSG walitwaa Ligue 1 kwa msimu wa tano mfululizo mwaka huu.
Kwa upande mwingine, kila anayefuatilia Ligi Kuu England anajua jinsi Arsenal walivyolazimika kufanya kazi kubwa ili kushinda ubingwa. Sehemu ya hali hiyo ilitokana na maumivu ya kushindwa kwao miaka iliyopita.
Baada ya kumaliza nafasi ya pili mara tatu mfululizo, Arsenal walikuwa na kiu kubwa ya kutwaa taji safari hii na waliogopa kulipoteza tena mbele ya Manchester City.
Lakini, pia walionekana kuchoka katika hatua za mwisho za msimu, na sehemu ya sababu ilikuwa ratiba ngumu pamoja na ukweli kwamba kocha Mikel Arteta hakufanya mzunguko mkubwa wa kikosi. Licha ya kutumia fedha nyingi msimu uliopita kuongeza kina cha kikosi, kulikuwa na baadhi ya wachezaji ambao Arteta hakutaka kabisa kuwapumzisha.
David Raya alicheza kila dakika ya Ligi Kuu England hadi Arsenal walipotwaa ubingwa, huku pia akianza mechi 13 kati ya 14 za Ligi ya Mabingwa Ulaya. Declan Rice na MartÃn Zubimendi walikuwa karibu kutogusika kabisa katikati ya uwanja.
Rice alikosa mechi mbili huku Zubimendi akicheza zote. Kwenye safu ya ulinzi, Gabriel Magalhaes na William Saliba walikosekana tu pale walipokuwa na matatizo.
Wachezaji hao watano wa Arsenal wote walianza angalau mechi 30 za Ligi Kuu England msimu huu, huku hakuna mchezaji wa PSG aliyeanza zaidi ya mechi 27 za Ligue 1.
Katika mashindano yote, kundi hilo la Arsenal limecheza zaidi ya dakika 4,000 kila mmoja msimu huu. Kwa PSG, mchezaji pekee aliyefikisha kiwango hicho ni Warren Zaïre-Emery.
Ukijumlisha vikosi vyote viwili, kuna wachezaji 12 waliofikisha angalau dakika 3,000 za mechi za ushindani msimu huu, na tisa kati yao wanatoka Arsenal.
Kama Jurrien Timber atakuwa fiti, wote wanaweza kuanza fainali mjini Budapest, leo Jumamosi na bila shaka, wachezaji hao wenye viwango vikubwa vya utimamu wa mwili wana uwezo wa kucheza mechi moja zaidi.
Lakini, mzigo mkubwa wa msimu unaweza kuwa na athari kuhusu ni timu gani itaweza kumudu hadi mwisho na kuendelea kucheza kwa kasi na nguvu ambazo makocha wao wanahitaji kwa dakika zote 90. Na hapo ndipo PSG inaweza kuwa na faida kubwa ya kuamua mchezo.
Fainali hiyo itakuwa mchezo wa 63 wa msimu wa 2025-26 kwa Arsenal, na wa 56 kwa PSG. Hata hivyo, PSG pia walicheza mechi saba kwenye Kombe la Dunia la Klabu majira ya kiangazi yaliyopita, maana yake ni kwamba ukijumuisha mashindano hayo timu zote mbili zimecheza mechi 62 tangu Juni, mwaka jana. Lakini ukiangalia kwa undani zaidi, kuna tofauti kubwa nyuma ya takwimu hizo.