SPOTI DOKTA: Ugumu wa mechi Simba SC ilistahili kufanya haya

Muktasari:
- Kutaka tiketi hiyo baada ya suluhu ya mechi ya marudiano ugenini haikuwa jambo rahisi, ila wachezaji walipambana kutoruhusu mabao zaidi. Ni kawaida wachezaji wanapotumia nguvu nyingi na kuchoka, kuwa wachovu na kupata majeraha.
KATIKA mchezo wa soka, kuna majeraha ya aina tano yanayowatesa zaidi wachezaji ambayo ni kifundo cha mguu, goti, nyama za paja, bega na kuvunjika mfupa.
Kwa mujibu wa madaktari wa timu za Ligi Kuu Bara msimu huu zipo changamoto nyingine za kiafya lakini kuna tatizo moja kubwa ambalo limeonekana kuzitesa karibu nusu ya timu shiriki.
Madaktari waliozungumza na Mwanaspoti kwa nyakati tofauti wameweka wazi kwamba tatizo la majeraha ya kifundo cha mguu maarufu kama enka ndiyo imekuwa shida kubwa msimu huu.
YANASABABISHWA NA NINI?
Sababu kubwa inayotajwa kujirudia kwa madaktari wote ni ugumu wa viwanja sehemu ya kuchezea. Kutua vibaya baada ya kuruka na aina ya viatu wanavyotumia wachezaji.
Majeraha ya enka au kifundo cha mguu, mara nyingi husababishwa pia na kujikunja ghafla kwa kifundo cha mguu, mara nyingi wakati wa michezo au wakati wa kutembea.
Kwa mujibu wa wataalam wa afya, majeraha haya yanahusisha kunyoosha au kupasuka kwa mishipa inayounga kifundo cha mguu. Sababu nyingine ni pamoja na kuanguka, kutua vibaya baada ya kuruka, au kupigwa kwa moja kwa moja kwenye kifundo cha mguu.
Katika ungio la enka linajumuisha mfupa wa kisigino na mifupa miwili iliyoungana ya mguu. Eneo hilo ni moja ya eneo ambalo wachezaji wa mpira wanapata majeraha kutokana na kulitumia kufanya mambo mengi wakati wanacheza.
Kutokana na maumbile ya ungio la enka kuwa na tishu laini kama vile ligamenti na tendoni, pale linapojeruhiwa husababisha kuchelewa kupona.
Kwa kawaida majeraha ya enka hujulikana kama ‘ankle strain na sprain’ ambayo yanakuwa sio katika hali mbaya na hayahusishi kuvunjika, bali ni kujeruhiwa kwa nyuzi za ligamenti, tendoni na misuli.

Nyuzi hizi zinaweza kupata majeraha baada ya kufinywa, kujipinda, kunepa, kuvutika kuliko pitiliza, kukwanyuka, kuchubuka na kuchanika kiasi au kukatika na kuachana pande mbili.
Wataalam wanaongeza kuwa eneo hilo likipatwa na shinikizo kubwa kama vile kugongwa na kitu kizito linaweza kusababisha nyufa katika mifupa, kututumka kwa mfupa na kuvunjika vifupa vidogo vya kilindo.
Mara zingine nyuzi hizi za kifundo zinaweza kuvutika sana na kubanwa katikati ya mifupa ya kifundo cha mguu endapo zitapata shinikizo kubwa.
Wataalam wanasema, nyuzi hizo ngumu zimejichimbia katika mifupa ya kifundo cha miguu ijulikanayo kama talus na tibia, na pale zinapopata majeraha husababisha maumivu, mlipuko wa kinga ya mwili na kuvimba.
Majeraha haya hulikumba zaidi eneo la mbele la mguu wa chini yaani funiko la mguu ni kujeruhiwa kwa mfupa wa enka (talus) au mfupa wa ugoko (tibia) katika eneo la mpaka wa kifundo na mguu wa juu.
Lakini wanaongeza kuwa uwepo wa majeraha katika mifupa ikiwamo nyufa au kupasuka vipande vidogovidogo huleta majeraha ya tishu laini zinazozunguka kuunda kifundo cha mguu na kuleta maumivu makali na kuvimba.
Dalili na viashiria vya majeraha ya kifundo cha mguu ni pamoja na maumivu na kuuma pale panapominywa eneo hilo la kifundo, kupata maumivu pale unapojaribu kukukunja au kunyoosha kifundo.
Inashauriwa wachezaji watoe ishara pale wanapohisi maumivu makali wanapofanyiwa faulu.

MADAKTARI LIGI KUU
Daktari wa Azam FC, Mbaruku Mlinga, anasema kifundo cha mguu ni tatizo kubwa ikifuatiwa na magoti. "Kwa mfano katika enka wakati mwingine husababishwa na hali ya wachezaji kugusana sana kwa sababu mpira kama ambavyo tunajua ni mchezo wa aina hiyo, jeraha hili huchukua muda wa kuanzia wiki tatu hadi nane ili kupona,"anasema.
Mbaruku aliongeza kwamba jeraha la enka mbali na kukaa kwa wiki tatu hadi nane, pia huweza kumsababishia mchezaji akawa nje ya uwanja kwa takribani mwezi mmoja hadi mitatu, ikiwa atafanyiwa upasuaji kutokana na ukubwa wa tatizo.
"Majeraha ya kwenye goti huwa yanatokana na kano 'Ligament' ambayo inashikilia mifupa, hii inaweza isisababishwe na ile hali ya kugusana mara kwa mara kwa wachezaji kwa sababu inatokana na matumizi ya nguvu mchezaji anayoitumia," anasema.
Daktari huyo, alisema mchezaji anapopata majeraha hayo ya goti, huweza kukaa nje ya uwanja kuanzia mwezi mmoja hadi mitatu, japo kama jeraha hilo ni kubwa na linahitaji upasuaji linaweza kumsababishia kutokuwa uwanjani zaidi kwa miezi sita au tisa.
"Mchezaji anapokumbwa na hali kama hiyo anatakiwa kuwa chini ya uangalizi wa madaktari muda wote, kwa sababu kuna vitu anatakiwa awe anashauriwa mara kwa mara, ikiwemo vyakula anavyopaswa kula ili mwili usiongezeke zaidi," anasema Mbaruku.
Daktari wa Coastal Union, Hussein Ramadhan, anasema: "Majeraha sumbufu zaidi ni goti,kifundo cha mguu na mabega, mara nyingi sehemu ambazo zinaunganisha viungo huwa zinakuwa na changamoto mara kwa mara kwa wachezaji.
"Kwa upande wa kwetu hapa Tanzania mara nyingi inasababishwa na miundombinu mibovu ya michezo, hapa nazungumzia viwanja ambavyo havikidhi vigezo.
"Pili ni ukosefu wa wataalamu wa viungo, wachezaji wanatakiwa wapate watu wenye ujuzi ambao hawa kazi yao ni kuwapa mazoezi halisi ya viungo yatakayowafanya wawe sawa kabla ya mechi.
"Ndani ya msimu mmoja, binafsi naweza kupokea kesi za majeraha niliyoyataja takribani kila mwezi, lakini zile za kugongana wachezaji wenyewe kwa wenyewe ni mara chache nayo inachangiwa na utimamu wa mwili wa mtu binafsi," anasema.
Dk Gilbert Kigadye ambaye ni daktari maarufu anayewatibia wanamichezo mbalimbali nchini, anasema majeraha yote yanayosumbua hakuna la zaidi ila yapo yanayojirudia mara kwa mara.
"Kama kifundo cha mguu au bega kesi zake ziko nyingi, huwa zinasababishwa na mgongano wa moja kwa moja au mazingira lakini kuna kitu wengi hawajui, ni maumbile ya mchezaji mwenyewe.
"Sababu ya kimazingira ndio tunavigusa viwanja lakini waandaaji wa michezo pia, namanisha wataalamu wa viungo wana uwezo kiwango gani.
"Kila jeraha lina muda wake wa kupona inategemea na aina yake tu, ila kama ukizidi, ndipo tunatafuta sababu za kuchelewa kurejea kwa kiungo katika hali yake," anasema daktari huyo.
Daktari Amina Salum wa KenGold, anasema majeraha yanayosumbua zaidi kwake ni enka. "Enka inasababishwa na viwanja vigumu lakini pia soka ni mchezo wa kugongana kwa hiyo kuna nyakati hali hiyo inatokana na wachezaji kupambana."
"Nyama za paja zinasababishwa kama mchezaji hajafanya mazoezi vizuri ya kupasha mwili kama ambavyo makocha wa mazoezi ya viungo wanataka yafanyike.
"Kuna uwezekano mchezaji alikuwa anategea, sasa akifanya kazi kubwa nyama zitapata shida, hapa anaweza akachana nyama, maumivu hayo yanategemea kwa mfano misuli anaweza kutibiwa kwa siku moja au mbili akaanza mazoezi," anasema.
Daktari wa Kagera Sugar, Abel Shindika, anasema majeraha sugu yanayomsumbua kwenye timu yake pia ni enka ikifuatiwa na goti. Kisababishi kimojawapo akitaja kuwa ni kuruka ama kugongana.
"Majeraha hayo yamekuwa yakijirudia kwa wachezaji wengi na kuchukua muda mrefu kupona kwa sababu maeneo wanayoumia ni nyeti, yanakuwa hayana mifupa, hivyo maumivu yanakuwa katika viungo, kuyaepuka ni ngumu, kuna wachezaji wanaopenda kucheza rafu na majeraha mengine yanatokea kwa bahati mbaya," anasema.
Daktari wa Singida Black Stars, Shima Shonde, amesema majeraha ya enka (ankle sprain) nayo ni ya kawaida mno kwa wachezaji, hasa baada ya mabadiliko ya kasi au kuanguka vibaya.
"Wengi hupata majeraha haya kutokana na kubadili mwelekeo kwa ghafla au kuangukia kifundo cha mguu. Tiba yake ni barafu, mapumziko na bandeji, lakini baada ya hapo lazima mchezaji afanye mazoezi maalum ya tiba ya viungo ili kurejesha nguvu ya mguu,” anasema.
Aliongeza kuwa majeraha ya kuchanika kwa misuli, hasa ile ya nyuma ya paja (hamstring), huchangiwa zaidi na ukosefu wa mazoezi ya kunyoosha kabla ya mechi.
"Hamstring ni misuli inayovutika kirahisi sana, hasa kama mchezaji hajafanya mazoezi ya kutosha ya kunyoosha. Tiba yake inahusisha baridi au joto, mapumziko na mazoezi ya taratibu ya kurejesha hali ya kawaida," anasema.
Majeraha mengine ni goti na kuvunjika kwa mifupa (fractures), ambayo mara nyingi hutokana na migongano mikali uwanjani au kuanguka vibaya.
"Majeraha ya goti, hasa ya mishipa ya mbele ya goti (ACL), ni ya hatari sana kwa wachezaji. Mchezaji anaweza kuwa nje ya uwanja kwa miezi sita hadi tisa. Ni jeraha linalohitaji upasuaji na mazoezi ya kurejesha nguvu kwa makini sana," anasema Dk Shonde na kuongeza.
"Fractures ni mabaya zaidi kwa kuwa huweza kumweka mchezaji nje ya uwanja kwa miezi kadhaa. Wengine hulazimika kufanyiwa upasuaji, hasa pale ambapo mfupa umevunjika vibaya sana.”
Pia alizungumzia majeraha ya bega (shoulder injuries) ambayo ingawa si ya kawaida kama mengine, hujitokeza sana kwa wachezaji wanaoshindana kwa mipira ya juu au wanaoanguka vibaya.
Akitolea ufafanuzi wa kinga dhidi ya majeraha hayo, Dk Shonde amesisitiza umuhimu wa uchunguzi wa awali (diagnosis) kwa kutumia vifaa vya kisasa kama MRI na X-ray, pamoja na ufuatiliaji wa karibu wa hali ya kiafya ya mchezaji. Pia ameshauri lishe bora na mapumziko ya kutosha kama nguzo muhimu kwa wachezaji.
Dk Shonde ametoa wito kwa uongozi wa klabu kuhakikisha kuna wataalamu wa kutosha na vifaa vya kisasa vya tiba na mazoezi.

WACHEZAJI
Winga wa Namungo FC, Issa Abushehe 'Messi', anasema aliwahi kuumia enka wakati akiwa mazoezini baada ya kutaka kuupiga mpira na ndipo mchezaji mwenzake akamkanyaga, japo haikumsumbua kutokana na kufuata utaratibu vizuri.
"Nakumbuka nilikaa kwa wiki mbili hadi tatu kisha nikarudi katika hali ya kawaida, mambo niliyoambiwa niyazingatie ni kutotumia kiatu chenye meno na nisikimbie kwenye lami, kwani ingeweza kunisababishia majeraha zaidi," anasema Abushehe.
Kwa upande wa beki wa Kagera Sugar, Datius Peter anasema moja ya majeraha ambayo amekuwa yakimsumbua ni ya goti; "Majeraha hayo ni ya kawaida kwa mchezaji yeyote,nakumbuka nilipata jeraha la goti wakati naenda kuokoa mpira uliokuwa unaenda langoni mwetu mechi na Mashujaa, kuanzia hapo sikuweza kuendelea na ilinichukua miezi mitatu kupona."
Datius anasema kilichomsaidia kurejea haraka ni kufuata ushauri wa madaktari, ikiwemo kupunguza kabisa kufanya mapenzi, asiwe mtu wa kutembea mara kwa mara hasa umbali mrefu, kisha kuzingatia kula mlo sahihi ili kulinda zaidi afya yake.
Kiungo wa KenGold, Abdallah Masoud ‘Cabaye’ ameeleza kwamba aliwahi kupata majeraha enka mazoezini wakati akikabiliana na mchezaji mwenzake.
Tukio hilo alisema lilitokea wakati akijaribu kuzuia mpira akiwa kwenye harakati za kulinda lakini aliteleza vibaya na mguu ukapata maumivu.
Baada ya vipimo vya awali, madaktari wa Kengold walithibitisha kuwa Cabaye alipata mtikisiko kwenye enka.
"Nimepata enka mara nyingi, ujue hii kazi yetu ni rahisi kukumbana na majeraha kwa sababu inahusisha migongano,nilikaa nje ya uwanja kwa wiki mbili na nilirejea na kuendelea na majukumu yangu, " alisema.
Beki wa Yanga, Shomary Kibwana alisema aliumia kwenye mchezo dhidi ya Simba hakumbuki ilikuwaje ila mara baada ya vipimo akiwa hospitali baada ya kuambiwa jeraha lake ni la kufanyiwa upasuaji alianza kusikia joto ghafla.
"Mimi ni mchezaji ambaye nina malengo kukaa nje miezi mingi nje ya uwanja ilikuwa inanipa shida nashukuru kocha Nasreddine Nabi na daktari walinipa moyo na kuamua kufanya maamuzi ya kufanyiwa upasuaji," alisema na kyuongeza;
"Hofu yangu kubwa ilikuwa kwenye upasuaji maana nilikuwa sijawahi kufanyiwa upasuaji na kama kijana mdogo bado nina malengo na ndoto kubwa kwenye mpira"
Alisema alipimwa vipimo vitatu tofauti Hospitali ya Taifa Muhimbili, hospitali binafsi na Tunisia ambapo alipelekwa kwaajili ya matibabu haikuwa rahisi kwake lakini Mungu alimpa ujasiri na kukamilisha zoezi la upasuaji ambao ulikuwa ni mdogo.
Kibwana alisema ili wachezaji waweze kuamini na kufanyiwa upasuaji kuepusha majeraha ya mara kwa mara wanatakiwa kujengwa sana kisaikolojia na sio kukimbilia kutumia dawa ambazo zitapunguza maumivu na kusababisha jeraha kurudi mara kwa mara.
Beki wa zamani wa Biashara United, Singida Black Stars, Abdulmajid Mangalo alisema majeraha yanarudisha nyuma ndoto za wachezaji hasa kukiwa hakuna usimamizi mzuri anajutia shida hiyo ambayo anaipitia sasa.
"Hakuna jeraha ambalo lenye afadhali kila kitu ambacho kinapunguza kasi ya kucheza kwa mchezaji kinamtoa mchezoni napitia wakati mgumu kwani kazi yangu ni mpira ni msumu sasa unakatika bila ya kucheza shida ikiwa ni goti," alisema na kuongeza:
"Mpira ndio ajira yangu ya kudumu nipo nje ya uwanja napambania kujiimarisha nafikiri kitu muhimu ambacho kinaweza kutusaidia wachezaji ni kuhakikisha mikataba yetu inazingatia majeraha kwani tunaachwa kipindi ambacho tunahitaji misaada wa kusimamiwa ili turudi kujipambania."