Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SIRI: Jeraha linalotesa mastaa msimu huu

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa madaktari wa timu za Ligi Kuu Bara waliozungumza na Mwanaspoti majeraha hayo yamekuwa sugu huku yakichukua muda mrefu kupona.

KATIKA mchezo wa soka, kuna majeraha ya aina tano yanayowatesa zaidi wachezaji ambayo ni kifundo cha mguu, goti, nyama za paja, bega na kuvunjika mfupa.

Kwa mujibu wa madaktari wa timu za Ligi Kuu Bara waliozungumza na Mwanaspoti majeraha hayo yamekuwa sugu huku yakichukua muda mrefu kupona.

Kati ya hayo, majeraha ya kifundo cha mguu ndiyo yametajwa zaidi kuwasumbua wachezaji huku sababu mbalimbali za kutokea kwake zikitajwa ambazo ni ugumu wa viwanja sehemu ya kuchezea, kutua vibaya baada ya kuruka na aina ya viatu wanavyotumia wachezaji.

Mbali na maumivu ya kifundo cha mguu, goti ni majeraha yanayofuatia katika kuwatesa wachezaji wa Ligi Kuu Bara kisha nyama za paja huku bega ikiwa sio sana.

Kwa mujibu wa madaktari hao, maumivu ya bega huwapata zaidi makipa kutokana na kazi yao mara nyingi ikiwa ni kujirusha.

Akizungumza na Mwanaspoti, Daktari wa Azam FC, Mbaruku Mlinga anasema kifundo cha mguu na goti ni miongoni mwa matatizo makubwa wanayokabiliana nayo, ingawa ukifuata utaratibu wake hupona kwa wakati husika.

New Content Item (2)
New Content Item (2)

“Kwa mfano katika kifundo cha mguu husababishwa na hali ya wachezaji kugusana sana kwa sababu mpira kama ambavyo tunajua ni mchezo wa aina hiyo, jeraha hili huchukua muda wa kuanzia wiki tatu hadi nane ili kupona,” anasema.

Mbaruku anaongeza kwamba jeraha la kifundo cha mguu mbali na kukaa kwa wiki tatu hadi nane, pia huweza kusababisha mchezaji akawa nje ya uwanja kwa takribani mwezi mmoja hadi mitatu, ikiwa atafanyiwa upasuaji kutokana na ukubwa wa tatizo.

“Majeraha ya kwenye goti huwa yanatokana na kano ‘Ligament’ ambayo inashikilia mifupa, hii inaweza isisababishwe na ile hali ya kugusana mara kwa mara kwa wachezaji kwa sababu inatokana na matumizi ya nguvu mchezaji anayoitumia,” anasema.

Daktari huyo, alisema mchezaji anapopata majeraha hayo ya goti, huweza kukaa nje ya uwanja kuanzia mwezi mmoja hadi mitatu, japo kama jeraha hilo ni kubwa na linahitaji upasuaji linaweza kumsababishia kutokuwa uwanjani zaidi kwa miezi sita au tisa.

Kutokana na majeraha hayo, Mbaruku alisema mchezaji anapokutana na hali hiyo hutakiwa asilazimishe kurudi uwanjani kama ambavyo wengi wao wamekuwa wakifanya kutokana na kuhofia kupoteza nafasi ya kucheza, kwani itasababisha matatizo zaidi.

“Mchezaji anapokumbwa na hali kama hiyo anatakiwa kuwa chini ya uangalizi wa madaktari muda wote, kwa sababu kuna vitu anatakiwa awe anashauriwa mara kwa mara, ikiwemo vyakula anavyopaswa kula ili mwili usiongezeke zaidi,” anasema Mbaruku.

Daktari wa Coastal Union, Hussein Ramadhan anasema: “Majeraha sumbufu zaidi ni goti, kifundo cha mguu na mabega, mara nyingi sehemu ambazo zinaunganisha viungo huwa zinakuwa na changamoto mara kwa mara kwa wachezaji.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

“Kwa upande wa kwetu hapa Tanzania mara nyingi inasababishwa na miundombinu mibovu ya michezo, hapa nazungumzia viwanja ambavyo havikidhi vigezo.

“Pili ni ukosefu wa wataalamu wa viungo, wachezaji wanatakiwa wapate watu wenye ujuzi ambao hawa kazi yao ni kuwapa mazoezi halisi ya viungo yatakayowafanya wawe sawa kabla ya mechi.

“Ndani ya msimu mmoja, binafsi naweza kupokea kesi za majeraha niliyoyataja takribani kila mwezi, lakini zile za kugongana wachezaji  wenyewe kwa wenyewe ni mara chache nayo inachangiwa na utimamu wa mwili wa mtu binafsi,” anasema.

Dk Gilbert Kigadye ambaye ni daktari maarufu anayewatibia wanamichezo mbalimbali hapa nchini, anasema majeraha yote yanasumbua hakuna la zaidi ila yapo yanayojirudia mara kwa mara.

“Kama kifundo cha mguu au bega kesi zake ziko nyingi, huwa zinasababishwa na mgongano wa moja kwa moja au mazingira lakini kuna kitu wengi hawajui, ni maumbile ya mchezaji mwenyewe.

“Sababu ya kimazingira ndio tunavigusa viwanja lakini waandaaji wa michezo pia, namanisha wataalamu wa viungo wana uwezo kiwango gani.

“Kila jeraha lina muda wake wa kupona inategemea na aina yake tu, ila kama ukizidi ndipo tunatafuta sababu za kuchelewa kurejea kwa kiungo katika hali yake,” anasema daktari huyo.

Daktari Amina Salum wa KenGold, anasema majeraha yanayosumbua zaidi kwake ni kifundo cha mguu, nyama za paja na misuli.

“Enka inasababishwa na viwanja vigumu lakini pia soka ni mchezo wa kugongana kwa hiyo kuna nyakati hali hiyo inatokana na wachezaji kupambana.

“Nyama za paja zinasababishwa kama mchezaji hajafanya mazoezi vizuri ya kupasha mwili kama ambavyo makocha wa mazoezi ya viungo wanataka yafanyike.

“Kuna uwezekano mchezaji alikuwa anategea, sasa akifanya kazi kubwa nyama zitapata shida, hapa anaweza akachana nyama, maumivu hayo yanategemea kwa mfano misuli anaweza kutibiwa kwa siku moja au mbili akaanza mazoezi,” anasema.

Daktari wa Kagera Sugar, Abel Shindika, anasema majeraha sugu ya wachezaji wengi ni goti na kifundo cha mguu ambayo mara nyingi yanatokana na mazoezi ya kuruka ama kugongana.

“Majeraha hayo yamekuwa yakijirudia kwa wachezaji wengi na kuchukua muda mrefu kupona kwa sababu maeneo wanayoumia ni nyeti, yanakuwa hayana mifupa, hivyo maumivu yanakuwa katika viungo, kuyaepuka ni ngumu, kuna wachezaji wanaopenda kucheza rafu na majeraha mengine yanatokea kwa bahati mbaya,” anasema.

Daktari wa Singida Black Stars, Shima Shonde, amesema majeraha ya kifundo cha mguu (ankle sprain) nayo ni ya kawaida mno kwa wachezaji, hasa baada ya mabadiliko ya kasi au kuanguka vibaya.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

“Wengi hupata majeraha haya kutokana na kubadili mwelekeo kwa ghafla au kuangukia kifundo cha mguu. Tiba yake ni barafu, mapumziko na bandeji, lakini baada ya hapo lazima mchezaji afanye mazoezi maalum ya tiba ya viungo ili kurejesha nguvu ya mguu,” anasema.

Aliongeza kuwa majeraha ya kuchanika kwa misuli, hasa ile ya nyuma ya paja (hamstring), huchangiwa zaidi na ukosefu wa mazoezi ya kujinyoosha kabla ya mechi.

“Hamstring ni misuli inayovutika kirahisi sana, hasa kama mchezaji hajafanya mazoezi ya kutosha ya kujinyoosha. Tiba yake inahusisha baridi au joto, mapumziko na mazoezi ya taratibu ya kurejesha hali ya kawaida,” anasema.

Katika majeraha mengine aliyoeleza, ni goti na kuvunjika kwa mifupa (fractures), ambayo mara nyingi hutokana na migongano mikali uwanjani au kuanguka vibaya.

“Majeraha ya goti, hasa ya mishipa ya mbele ya goti (ACL), ni ya hatari sana kwa wachezaji. Mchezaji anaweza kuwa nje ya uwanja kwa miezi sita hadi tisa. Ni jeraha linalohitaji upasuaji na mazoezi ya kurejesha nguvu kwa makini sana,” anasema Dk Shonde na kuongeza:

“Fractures ni mbaya zaidi kwa kuwa huweza kumweka mchezaji nje ya uwanja kwa miezi kadhaa. Wengine hulazimika kufanyiwa upasuaji, hasa pale ambapo mfupa umevunjika vibaya sana.”

Pia alizungumzia majeraha ya bega (shoulder injuries) ambayo ingawa si ya kawaida kama mengine, hujitokeza sana kwa wachezaji wanaoshindana kwa mipira ya juu au wanaoanguka vibaya.

Akitolea ufafanuzi wa kinga dhidi ya majeraha hayo, Dk Shonde amesisitiza umuhimu wa uchunguzi wa awali (diagnosis) kwa kutumia vifaa vya kisasa kama MRI na X-ray, pamoja na ufuatiliaji wa karibu wa hali ya kiafya ya mchezaji. Pia ameshauri lishe bora na mapumziko ya kutosha kama nguzo muhimu kwa wachezaji.

Akihitimisha, Dk Shonde ametoa wito kwa uongozi wa klabu kuhakikisha kuna wataalamu wa kutosha na vifaa vya kisasa vya tiba na mazoezi.


INAVYOKUWA

Majeraha ya kifundo cha mguu, mara nyingi husababishwa na kujikunja ghafla kwa kifundo cha mguu, mara nyingi wakati wa michezo au wakati wa kutembea.

Majeraha haya yanahusisha kunyoosha au kupasuka kwa mishipa inayounga kifundo cha mguu. Sababu nyingine ni pamoja na kuanguka, kutua vibaya baada ya kuruka, au kupigwa moja kwa moja kwenye kifundo cha mguu.

Ungio la kifundo linajumuisha mfupa wa kisigino na mifupa miwili iliyoungana ya mguu. Eneo hilo ni moja ya maeneo ambayo wachezaji wa mpira wanapata majeraha kutokana na kuyatumia kufanya mambo mengi wakati wanacheza.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Kutokana na maumbile ya ungio la kifundo cha mguu kuwa na tishu laini kama vile ligamenti na tendoni, pale linapojeruhiwa husababisha kuchelewa kupona.

Kwa kawaida majeraha ya kifundo cha mguu hujulikana kama ‘ankle strain na sprain’ ambayo yanakuwa sio katika hali mbaya na hayahusishi kuvunjika, bali ni kujeruhiwa kwa nyuzi za ligamenti, tendoni na misuli.

Nyuzi hizi zinaweza kupata majeraha baada ya kufinywa, kujipinda, kunepa, kuvutika kuliko pitiliza, kukwanyuka, kuchubuka na kuchanika kiasi au kukatika na kuachana pande mbili.

Vilevile eneo hilo likipatwa na shinikizo kubwa kama vile kugongwa na kitu kizito linaweza kusababisha nyufa katika mifupa, kututumka kwa mfupa na kuvunjika vifupa vidogo vya kilindo.

Mara zingine nyuzi hizi za kifundo zinaweza kuvutika sana na kubanwa katikati ya mifupa ya kifundo cha mguu endapo zitapata shinikizo kubwa.

Nyuzi hizo ngumu zimejichimbia katika mifupa ya kifundo cha miguu ijulikanayo kama talus na tibia, na pale zinapopata majeraha husababisha maumivu, mlipuko wa kinga ya mwili na kuvimba.

Majeraha haya hulikumba zaidi eneo la mbele la mguu wa chini yaani funiko la mguu ni kujeruhiwa kwa mfupa wa kifundo cha mguu (talus) au mfupa wa ugoko (tibia) katika eneo la mpaka wa kifundo na mguu wa juu.

Uwepo wa majeraha katika mifupa ikiwamo nyufa au kupasuka vipande vidogovidogo huleta majeraha ya tishu laini zinazozunguka kuunda kifundo cha mguu na kuleta maumivu makali na kuvimba.

Dalili na viashiria vya majeraha ya kifundo cha mguu ni pamoja na maumivu na kuuma pale panapominywa eneo hilo la kifundo, kupata maumivu pale unapojaribu kukunja au kunyoosha kifundo.

Inashauriwa wachezaji watoe ishara pale wanapohisi maumivu makali wanapofanyiwa faulo.


WASIKIE WACHEZAJI

Winga wa Namungo FC, Issa Abushehe ‘Messi’, anasema aliwahi kuumia kifundo cha mguu (ankle) wakati akiwa mazoezini baada ya kutaka kuupiga mpira na ndipo mchezaji mwenzake akamganyaga, japo haikumsumbua kutokana na kufuata utaratibu vizuri.

“Nakumbuka nilikaa kwa wiki mbili hadi tatu kisha nikarudi katika hali ya kawaida, mambo niliyoambiwa niyazingatie ni kutotumia kiatu chenye meno na nisikimbie kwenye lami, kwani ingeweza kunisababishia majeraha zaidi,” anasema Abushehe.

Kwa upande wa beki wa Kagera Sugar, Datius Peter anasema moja ya majeraha ambayo amekuwa yakimsumbua ni ya goti, ingawa kifundo cha mguu, misuli ni miongoni mwao, ingawa sio kwa kiwango kikubwa japo anachozingatia ni ushauri wa madaktari.

“Majeraha hayo ni ya kawaida kwa mchezaji yeyote, nakumbuka nilipata jeraha la goti wakati naenda kuokoa mpira uliokuwa unaenda langoni mwetu mechi na Mashujaa, kuanzia hapo sikuweza kuendelea na ilinichukua miezi mitatu kupona,” anasema.

Datius anasema kilichomsaidia kurejea haraka ni kufuata ushauri wa madaktari, ikiwemo kupunguza kabisa kufanya mapenzi, asiwe mtu wa kutembea mara kwa mara hasa umbali mrefu, kisha kuzingatia kula mlo sahihi ili kulinda zaidi afya yake.

Kiungo wa KenGold, Abdallah Masoud ‘Cabaye’ambaye kwa sasa amesimamishwa kwa utovu wa nidhamu, ameeleza kwamba aliwahi kupata majeraha ya enka mazoezini  wakati akikabiliana na mchezaji mwenzake.

Tukio hilo alisema lilitokea wakati akijaribu kuzuia mpira akiwa kwenye harakati za kulinda lakini aliteleza vibaya na mguu ukapata maumivu.

Anasema mara baada ya tukio hilo, alishindwa kuendelea na mazoezi na benchi la ufundi lililazimika kumtoa uwanjani huku akisaidiwa na timu ya tiba. Baada ya vipimo vya awali, madaktari wa KenGold walithibitisha kuwa Cabaye alipata mtikisiko kwenye enka (ankle sprain).

“Nimepata enka mara nyingi, ujue hii kazi yetu ni rahisi kukumbana na majeraha kwa sababu inahusisha migongano, nilikaa nje ya uwanja kwa wiki mbili na nilirejea na kuendelea na majukumua yangu,” alisema.

Beki wa Yanga, Kibwana Shomary alisema aliumia kwenye mchezo dhidi ya Simba hakumbuki ilikuwaje ila mara baada ya vipimo akiwa hospitalini baada ya kuambiwa jeraha lake ni la kufanyiwa upasuaji alianza kusikia joto ghafla.

“Mimi ni mchezaji ambaye nina malengo. Kukaa nje ya uwanja miezi mingi ilikuwa inanipa shida, nashukuru kocha Nasreddine Nabi na daktari walinipa moyo na kuamua kufanya uamuzi wa kufanyiwa upasuaji,” alisema na kuongeza;

“Hofu yangu kubwa ilikuwa kwenye upasuaji maana nilikuwa sijawahi kufanyiwa upasuaji na kama kijana mdogo bado nina malengo na ndoto kubwa kwenye mpira.”

Alisema alipimwa vipimo vitatu tofauti Hospitali ya Taifa Muhimbili, hospitali binafsi na Tunisia ambako alipelekwa kwaajili ya matibabu. Haikuwa rahisi kwake lakini Mungu alimpa ujasiri na kukamilisha zoezi la upasuaji ambao ulikuwa ni mdogo.

Kibwana alisema ili wachezaji waweze kuamini na kufanyiwa upasuaji kuepusha majeraha ya mara kwa mara wanatakiwa kujengwa sana kisaikolojia na sio kukimbilia kutumia dawa ambazo zitapunguza maumivu na kusababisha jeraha kurudi mara kwa mara.

Beki wa zamani wa Biashara United, Singida Black Stars, Abdulmajid Mangalo alisema majeraha yanarudisha nyuma ndoto za wachezaji hasa kukiwa hakuna usimamizi mzuri anajutia shida hiyo ambayo anaipitia sasa.

“Hakuna jeraha ambalo lina uafadhali, kila kitu ambacho kinapunguza kasi ya kucheza kwa mchezaji kinamtoa mchezoni. Napitia wakati mgumu kwani kazi yangu ni mpira, ni msimu sasa unakatika bila ya kucheza shida ikiwa ni goti,” alisema na kuongeza:

“Mpira ndio ajira yangu ya kudumu nipo nje ya uwanja napambania kujiimarisha, nafikiri kitu muhimu ambacho kinaweza kutusaidia wachezaji ni kuhakikisha mikataba yetu inazingatia majeraha kwani tunaachwa kipindi ambacho tunahitaji misaada wa kusimamiwa ili turudi kujipambania.”

Alisema jeraha la goti ni baya kwa mchezaji kwasababu ni eneo ambalo ndio mhimili wa kupambana. Mchezaji akiumia goti ili aweze kurudi haraka uwanjani hatakiwi kufanya mambo mengi lakini pia kwenye kutulia hatakiwi kupata uzito mkubwa kwani hilo pia bado litamtesa.