Shaaa… Makocha hawa wamesepa ghafla!
Muktasari:
- Lakini, mara kadhaa imeshuhudiwa makocha wakitimka ghafla wakiwaacha mashabiki na viongozi wa klabu wakiwa na mshangao. Katika Ligi Kuu Bara na hata kwingineko Afrika matukio hayo yamekuwa ya kawaida.
KATIKA ulimwengu wa soka hujenga timu na kutoa mbinu za ushindi, kuamsha morali ya wachezaji na kuipa klabu dira ya mafanikio uwanjani.
Lakini, mara kadhaa imeshuhudiwa makocha wakitimka ghafla wakiwaacha mashabiki na viongozi wa klabu wakiwa na mshangao. Katika Ligi Kuu Bara na hata kwingineko Afrika matukio hayo yamekuwa ya kawaida.
Mfano wa karibuni ni kuondoka kwa Fadlu Davids kutoka Simba jambo lililoshangaza wengi. Lakini, tukio hilo sio la kwanza kwani kabla yake imewahi kushuhudiwa makocha wakiondoka ghafla na kujiunga na timu nyingine.
Wengi walionekana kama wasaliti kwa mashabiki, lakini wengine walitajwa kama watu waliotafuta changamoto na maisha bora zaidi.
Makala hii inamulika baadhi ya makocha waliotimka ghafla na kujiunga na timu zingine ikiweka kumbukumbu ya namna walivyoacha taswira tofauti ndani ya klabu walizozihudumia.
1. Fadlu Davids (Simba)
Kuondoka kwa Fadlu Davids Simba kuliacha pengo kubwa kwani alionekana kuanza kujenga mfumo mzuri wa uchezaji, lakini ghafla akatimka.
Simba baada ya kufikishwa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ndani ya msimu wake wa kwanza, iliamini msimu huu kocha huyo angeipeleka mbali zaidi ikimpa imani kubwa ya kujenga kikosi chake bila kuingiliwa.
Hata hivyo, Fadlu alitimka ghafla baada ya hatua ya awali kuanza msimu mpya, inaelezwa kocha huyo ambaye amerejea Raja Athletic ya Morocco hakutaka kupishana na ofa kubwa aliyowekewa na Waarabu na kuwaacha mashabiki, wanachama, wachezaji na viongozi wa klabu wakishtushwa na uamuzi wa kocha huyo raia wa Afrika Kusini.
2. Zoran MakI (Simba)
Simba ilipitia maisha hayo wakati Zoran Mack akitambulishwa Juni 29, 2022 kuchukua nafasi ya Mhispaniola Pablo Franco.
Zoran alianza hesabu za kuijenga kikosi akiingia kambini (pre season) Misri kisha baadaye kurejea nchini kuanza msimu.
Kabla ya kuanza msimu mpya ghafla Septemba 6,2022 kocha huyo akashtua baada ya kuwataka mabosi wa klabu hiyo kusitisha mkataba ili akajiunge na klabu nyingine iliyompa dau kubwa akiwauliza mabosi wa Simba iwapo wangeweza kulifikia.
Simba ilikubali yaishe na kuamua kuachanaa na raia huyo wa Serbia, kisha akatimka na kwenda Al Ittihad ya Libya ambayo ilikuwa inajenga timu ya ushindani
3. Denis Kitambi (Namungo)
Kocha Denis Kitambi ni mmoja wa makocha vijana wenye uwezo mkubwa wa kufundisha timu, lakini naye aliwahi kuachana klabu moja ghafla na kutimkia nyingine.
Kitambi alifanya uamuzi huo wakati anaifundisha Namungo kisha akiwa katikati ya msimu akaamua kuiacha Desemba 12,2023 na kwenda kujiunga na Geita Gold wakati huo ikiwa Ligi Kuu Bara.
Uongozi wa Namungo haukufurahishwa na uamuzi huo, lakini ukaamua kumuacha kisha kocha huyo akatangazwa Desemba 20, 2023 kuwa kocha mpya wa Geita Golda na siku moja baadaye akaiongoza kushinda bao 1-0 dhidi ya Fountain Gate. Hata hivyo, Kitambi ambaye anasifika kwa ubora wa kuwasoma wapinzani hakuwa na mafanikio ndani ya Geita Gold ambapo timu hiyo iliyumba ikikosa matokeo mpaka ikashuka daraja.
Wakati Geita ikishuka Namungo ilifanikiwa kubaki Ligi Kuu. Zipo taarifa pia kwamba Kitambi ameshaondoka Fountain Gate aliyoanza nayo msimu huu ambayo inasuasua uwanjani kutokana na kutokuwa na wachezaji wengi kikosini.
5. Juma Mgunda (Coastal Union)
Juma Mgunda yumo kwenye kundi hili baada ya kutua Simba ghafla akitokea Coastal Union wakati huo Wekundu wa Msimbazi walipoachana na kocha Zoran Maki.
Wakati Mgunda akitua Simba ilishtua wengi akiachana na nafasi yake Coastal Union kwenda kuungana na Wekundu hao akiwekewa dau zuri la mshahara ili akakaimu nafasi hiyo kwa muda ikizingatiwa timu hiyo ilikuwa inakabiliwa na mechi za kimataifa. Hata hivyo baadaye Simba iliachana naye baada ya kumpata Roberto Oliveira ‘Robertinho.
6. Sead Ramovic (Yanga)
Kocha huyo Mjerumani alitambulishwa na Yanga Novemba 16, 2024 akichukua nafasi ya Miguel Gamondi aliyesitishiwa mkataba baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam alipochapwa bao 1-0 na Tabora United (sasa TRA United) kwa mabao 3-1. Hata hivyo, baada ya kuingoza timu hiyo kwa muda wa miezi mitatu hivi ghafla kocha huyo alisepa Jangwani na kuibukia Algeria kuinoa CR Belouizdad.
Ramovic alitemana na Yanga Februari 4, 2025 wakati timu ikijiandaa kucheza mechi ya Ligi Kuu dhidi ya KenGold na kutoa nafasi kwa Miloud Hamdi ambaye naye aliondoka ghafla klabuni mara baada ya kumalizika kwa msimu wa 2024-2025 alioipa timu hiyo mataji matatu yakiwamo ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA), kisha akaibukia Al Ismailia ya Misri alipo hadi sasa.
WENGINE
Wapo makocha wengine ambao waliibukia katika Ligi Kuu Bara na wala hawakudumu muda mrefu kutokana na kusitishiwa au kusitisha wenyewe mikataba na hawakuwa na dili za kujiunga na timu nyingine akiwamo kocha Mfaransa wa Azam, Denis Lavagne aliyedumu Chamazi kwa mwezi mmoja.
Kocha huyo mwenye wasifu mkubwa alitambulishwa na Azam Septemba 22, 2022 na mechi yake ya kwanza ilikuwa dhidi ya Yanga kisha akatemeshwa kibarua Oktoba 22 baada ya kupoteza tena mbele ya KMC.
Pia kuna Zlatko Krmpotic aliyejiunga na Yanga msimu wa 2020-2021 akitua Jangwani Agosti 28, 20220 na kutemeshwa kibarua Oktoba 4, mwaka huohuo akiwa ameiongoza timu hiyo katika mechi tano ambazo ilishinda nne na kutoka sare moja kabla ya ‘thank you’ iliyotoka bila kutarajiwa akiwa amevuna pointi 13 ndani ya kipindi kifupi. Kocha huyo alitua kwenye kikosi hicho akichukua nafasi ya Luc Eymael ambaye naye aliondoka juu kwa juu mara baada ya msimu wa 2019-2020 kumalizika.