MZEE WA FACT: Harufu ya 1992 kwenye dabi ya 2025

Muktasari:
- Hivi karibuni mjadala wa mechi ya watani wa jadi, Yanga na Simba, ulirudi tena na kuilazimu bodi ya ligi kuweka tena wazi msimamo wao kwamba mechi ipo.
Hivi karibuni mjadala wa mechi ya watani wa jadi, Yanga na Simba, ulirudi tena na kuilazimu bodi ya ligi kuweka tena wazi msimamo wao kwamba mechi ipo.
Lakini hata hivyo hadi sasa hakuna uhakika wa kuwepo kwa mechi hiyo iliyokwama kufanyika Machi 8, 2025.
Yanga wanaendelea kusisitiza kwamba hawatocheza tena mechi hiyo kwa tarehe nyingine, na wasimamizi wa mpira, bodi ya ligi na TFF, wanaendelea kusisitiza kwamba mechi itapangiwa tarehe nyingine na itafanyika.
Hali hii imeturudisha hadi mwaka 1992 kwenye mkasa wa mechi kama hii.
Wakati huo chama cha soka kilikuwa kikiitwa FAT na kilikuwa chini ya uongozi wa mwenyekiti wa muda Muhidini Ndolanga, marehemu, na katibu mkuu Geras Lubega.
Mechi ilipangwa kufanyika Agosti 8, 1992 kwenye uwanja wa taifa, sasa Uhuru.
Lakini FAT iliahirisha kwa kuwa Simba ilikuwa na wachezaji watano kwenye timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.
Stars ilikuwa kambini kujiandaa na mechi mbili za kufuzu AFCON 1994, dhidi ya Ghana Agosti 15, na dhidi ya Liberia Agosti 30.
Pambano likapangwa lichezwe Agosti 22, lakini likaahirishwa tena kufuatia maombi ya Simba.

Yanga hawakufurahishwa na hilo kwa sababu walishajiandaa.
Wakasema hawatocheza tena mechi hiyo hadi walipwe fidia ya shilingi milioni moja na laki tano kwa hasara ya maandalizi.
Wakati mgogoro unaendelea, na ligi ilikuwa inaendelea hatimaye Yanga wakapata alama za kutosha kuwahakikishia ubingwa.
FAT ikapanga mechi ichezwe Septemba 26 lakini hadi hapo tayari Yanga walishakuwa mabingwa wakagoma kucheza.
Sakata hili liliusumbua sana uongozi wa muda wa FAT ulioingia madarakani Disemba 1991.
ULIINGIAJE?
Novemba 30, 1991, timu ya taifa ya Tanzania Bara (jina la Kilimanjaro Stars lilikuwa halijaanza) ilifungwa 5-0 na Uganda Cranes, na kutolewa kwenye mashindano ya CECAFA Challenge Cup.
Wakati huo mashindano haya yalikuwa na heshima kubwa sana.
Zambia ambao baadaye wakawa mabingwa, walimleta Kalusha Bwalya aliyekuwa akicheza PSV ya Uholanzi.
Bwalya na Majjid Musisi wa Uganda, wakawa wafungaji bora wa mashindano.
Baada ya kipigo hiki, Halmashauri Kuu ya FAT ilikutana Mwanza, mwezi Disemba na kuuondoa uongozi wa FAT chini ya mwenyekiti Mohamed Mussa.
Halmashauri Kuu ya FAT kilikuwa chombo kilichoundwa na wenyeviti wa mikoa wa FAT, na ndicho kilichokuwa na nguvu, nyuma ya mkutano mkuu ambao ulihusisha pia makatibu.
Mussa aliingia madarakani 1986 kuchukua nafasi ya Said El Maamry, aliyeondolewa madarakani kwa shinikizo la serikali!
Kuondoka kwa Mohamed Mussa na katibu mkuu wake Meshack Maganga, kukampa nafasi Muhidin Ndolanga, ambaye alikuwa mwenyekiti wa chama cha soka mkoa wa Arusha, kuchukua nafasi kwa muda, akiwa na katibu wake Geras Lubega, ambaye alikuwa katibu wa chama cha makocha, TAFCA.
Watu hawa wakaanza kazi Januari 1992, walitakiwa kuongoza kwa muda hadi 1993, kwenye uchaguzi mkuu.
Mtihani wao wa kwanza ukawa mgogoro wa mechi ya watani kwa kweli uliwaendesha sana.

Baada ya mivutano mikali, Simba wakapewa ushindi wa mezani wa mabao mawili na alama mbili.
Kanuni za wakati huo hazikuwa na adhahu kubwa zaidi ya hiyo.
Ushindi huu wa mezani ulikuwa nafuu kubwa kwa Simba kwani wakitoka kuteseka sana kwa Yanga.
Huu ulikuwa ushindi wa kwanza kwa Simba dhidi ya Yanga tangu Mei 26. 1990 waliposhinda 1-0 kwa bao la mkwaju wa adhabu ndogo wa Mavumbi Onaru dakika ya 6.
Baada ya hapo Simba ilipoteza mechi sita mfululizo, ikiwemo moja ya kipigo cha mezani baada ya kugoma kucheza na Yanga.
OKTOBA 20, 1990 - ligi ya muungano
Yanga 3-1 Simba
WAFUNGAJI:
Yanga: Makumbi Juma dk 33, Thomas Kipese dk. 82, Sanifu Lazaro dk. 89
Simba: Edward Chumila dk. 58.
MEI 18, 1991 - ligi ya bara
Yanga 1-0 Simba
MFUNGAJI: Said Sued ‘Scud’ dk. 7.
AGOSTI 31, 1991 - ligi ya bara
Simba 0 - 1 Yanga
MFUNGAJI: Said Sued Scud.

OKTOBA 9, 1991 - ligi ya muungano
Yanga 2-0 Simba
WAFUNGAJI: Athumani China dk. 3, Abubakar Salum ‘Sure Boy’ dk. 54.
NOVEMBA 13, 1991 - ligi ya muungano
Simba 0 - 2 Yanga
Ushindi wa mezani baada ya Simba kugoma.
APRILI 12, 1992 - ligi ya bara
Yanga 1-0 Simba
MFUNGAJI: Kenneth Mkapa dk. 10.
SEPTEMBA 26, 1992 - ligi ya bara
Simba 2-0 Yanga
Ushindi wa mezani baada ya Yanga kugoma.
Ukiuangalia mkasa huu unaelekea kufanana kwa hali na wa mwaka huu.
Mechi imeshindwa kufanyika Yanga wamesema hawachezi mechi hiyo tena na ligi inaendelea.

Yawezekana ikaja kupangwa katika tarehe ambayo tayari Yanga washakuwa mabingwa huenda wakagoma kama 1992.
Pia mfululizo wa matokeo katika mechi zilizopita ni mbaya kwa Simba huenda wakajipatia ushindi wa kwanza baada ya muda mrefu kwa matokeo ya mezani kama 1992.
Hebu tusubiri tuone.