Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kicheko, kilio siku 7 za Kombe la Mapinduzi 2026

MAPINDUZI Pict

Muktasari:

  • Timu hizo shiriki ni Mlandege, Azam, URA na Singida Black Stars zilizopangwa kundi A. Kundi B zipo Simba, Muembe Makumbi City na Fufuni, wakati kundi C ni Yanga, KVZ na TRA United.

JUZI Jumamosi zilitimia siku saba tangu kuanza kwa NMB Mapinduzi Cup 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja ambapo timu 10 zinashiriki.

Timu hizo shiriki ni Mlandege, Azam, URA na Singida Black Stars zilizopangwa kundi A. Kundi B zipo Simba, Muembe Makumbi City na Fufuni, wakati kundi C ni Yanga, KVZ na TRA United.

Tumeshuhudia katika kipindi hicho, bingwa mtetezi Mlandege ikiaga mashindano mapema baada ya kupoteza mechi zote tatu za hatua ya makundi, huku ikiruhusu mabao sita na yenyewe ikifunga moja tu.

Ilianza kuchapwa 3-1 na Singida Black Stars, kisha 1-0 na URA, ikamaliza kupasuliwa 2-0 na Azam.

Mlandege imeondoshwa mashindanoni hata kabla Simba na Yanga hazijashuka dimbani katika michuano hiyo.

Muembe Makumbi City ikafuatia kwa kuaga mashindanoni, huku Singida Black Stars ikiwa ya kwanza kufuzu nusu fainali.

Wakati leo Jumatatu na kesho Jumanne mechi za hatua ya makundi zikihitimishwa, hapa kuna mambo kadhaa yaliyojiri ndani ya wiki hiyo moja ambapo tamati ya michuano hii itakuwa Januari 13, 2026 kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba.

MAPI 03

TAIFA STARS YAPEWA HESHIMA

Wakati ratiba ya michuano ya NMB Mapinduzi Cup inapangwa, kamati ya maandalizi iliipa heshima timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inayoshiriki Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2025) zinazoendelea nchini Morocco.

NMB Mapinduzi Cup ilipoanza Desemba 28, 2025, Taifa Stars ilikuwa tayari imeshuka dimbani huko Morocco mara mbili, Desemba 23, 2025 dhidi ya Nigeria na Desemba 27, 2025 dhidi ya Uganda. Mechi iliyofuata ilikuwa Desemba 30, 2025 dhidi ya Tunisia.

Siku ambayo Taifa Stars inacheza dhidi ya Tunisia, hakukuwa na mechi ya NMB Mapinduzi Cup, badala yake siku hiyo ilitengwa maalum kwa ajili ya kuwapa fursa Watanzania kushuhudia mubashara kupitia runinga.

Hata hivyo, matarajio ya wengi ilikuwa Taifa Stars itaishia makundi, lakini imetoboa 16 bora na jana ilicheza dhidi ya mwenyeji, Morocco.

Kufuzu kwa Taifa Stars hatua ya 16 bora, kamati ya maandalizi ya NMB Mapinduzi Cup 2026 ilisema ratiba ya mechi ya jana kati ya Yanga na KVZ imebadilishwa muda kutoka saa 2:15 usiku hadi saa 11:00 jioni.

Uamuzi huo umekuja kufuatia Taifa Stars kucheza na Morocco saa 1:00 usiku, hivyo kamati hiyo imetoa nafasi kwa Watanzania kulishuhudia chama lao, lakini pia kushuhudia mechi ya Yanga dhidi ya KVZ kwa utulivu.

MAPI 01

KILIO CHA WAUZA JEZI

Kuanzia Jumapili ya Desemba 28, 2025 wakati NMB Mapinduzi Cup ilianza hadi kufikia Ijumaa Januari 2, 2026, hakukuwa na mzuka mkubwa, mitaani kulipoa sio siku ya mechi wala ya mapumziko.

Hii ilionyesha kama vile bado watu hawajapata kile wanachohitaji kwa maana ya kushuhudia timu zao pendwa kutoka Tanzania Bara, Yanga na Simba.

Licha ya Azam, Singida Black Stars na TRA United za Tanzania Bara kutangulia kufika Unguja, lakini haikuleta msisimko.

Hali hiyo imewaathiri kwa kiasi fulani wafanyabiashara ya jezi wanaofanya shughuli zao pembezoni mwa Uwanja wa New Amaan Complex.

Mmoja wa wafanyabiashara ya jezi aliyejitambulisha kwa jina la Makame Ali Haji, amesema bado biashara ni ngumu pengine kwa sababu Simba na Yanga zimechelewa kufika.

“Kwa makadirio siku moja naweza kuuza jezi mbili hadi tatu, lakini sio kila siku inaweza kuwa hivyo, bado mwamko wa mashabiki ni mdogo, hivyo tunatarajia labda zikija Simba na Yanga mambo yatakuwa mazuri.

“Sisi hapa jezi zetu kwa asilimia kubwa ni za Simba na Yanga na bei zake ni Sh10,000, hivyo kwa kuwa timu hizo hazijafika basi ndio maana hali imekuwa hivi, tunaamini siku zinavyokwenda biashara itachangamka kwa sababu mashabiki wataongezeka baada ya Simba na Yanga kufika.”

MAPI 02

BODABODA WANAPIGA HELA BALAA

Wakati wauza jezi wakiwa na kilio, upande wa pili ni kicheko tu kwa waendesha bodaboda kwani wao wanapiga hela kama kawaida.

Bodaboda wanapiga sana hela kwa mechi za usiku kwani bei yake ya safari wakati huo na mchana inakuwa tofauti.

Bodaboda mmoja aitwaye Hassan Mohamed maarufu Kismart, anasema mchana wakimbeba mtu katika nauli ya Sh5,000, usiku inakuwa mara mbili yake.

“Kama mchana unambeba mtu kwa Sh5,000, basi usiku inakuwa mara mbili yake na hakuna anayekataa kwa sababu usiku vyombo ni vichache,” anasema.

Hali hiyo imejidhihirisha kwani mara tu mechi inapomalizika, bodaboda wanakaa geti kubwa kusubiri abiria, ni kama vile kijiwe chao kinahamia hapo kwa muda.

MAPI 04

MAJUKWAANI MH!

Kwenyea Uwanja wa New Amaan Complex, mechi zilipoanza kupigwa mashabiki walikuwa wachache sana hali ambayo ilidhihirisha bado mwamko ulikuwa mdogo.

Mechi za Mlandege kwa kiasi fulani zilikuwa na mashabiki wengi na hii imetokana na Mstahiki Meya wa Jiji la Zanzibar, Kamal Abdulsatar ambaye pia ni rais wa klabu hiyo mara kadhaa kununua tiketi kwa ajili ya makundi mbalimbali ya hamasa.

Kwa kiingilio cha Sh1,000, Sh2,000 na Sh5,000, mashabiki huingia uwanjani kushuhudia mechi za Kombe la Mapinduzi.

Mzuka ulikuja siku ambayo Simba ilicheza na Muembe Makumbi ambapo majukwaa kwa asilimia kubwa yalikuwa na watu wengi, lakini kabla ya hapo, siku hiyohiyo ilipigwa mechi kati ya Singida Black Stars dhidi ya URA, hali ikawa ileile, mashabiki wa kuhesabu sana.

MAPI 05

KAULI YA ZFF

Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) ambaye pia Msemaji wa NMB Mapinduzi Cup 2026, Mohamed Kabwanga, amesema wanaamini kadiri siku zinavyokwenda, msisimko utazidi kuongezeka.

Kabwanga amebainisha kuwa, kutokana na udhamini walioupata wa Benki ya NMB kama mdhamini mkuu na wadhamini wengine, anaamini mashindano ya mwaka huu yatakuwa na ushindani mkubwa kwani kila timu itataka kuwa ya kwanza kubeba ubingwa na kitita cha Sh150 milioni.

“Udhamini upo wa kutosha, zawadi pia zipo za kutosha, kwa hiyo timu zitacheza kwa nguvu zao zote ili kuweka historia baada ya kuja mwekezaji, mimi nakwenda kuwa bingwa wa kwanza.

“Tulivyoanza msimu huu tunaweza kutofautisha na msimu uliopita, kwanza kwa mechi za awali watu walioingia uwanjani sisi inatupa faraja kwa sababu bado kuna mechi kubwa zaidi zitachezwa, maana yake bado mashindano yako moto kwelikweli.

“Tunaamini mashindano haya na namna tunavyokwenda kuyamaliza kwake tutapata mrejesho mzuri tunaotarajia.”

“Tukumbuke fainali tutaenda kuuzindua Uwanja wa Gombani kule Pemba. Mwaka jana fainali ilifanyika kule watu wakidhani haitakuwa na mvuto kutokana na kushiriki timu za mataifa, lakini mwisho wa siku uwanja ulijaa na hakukuwa pa kukanyaga.

“Sasa safari hii ni ngazi ya klabu, watu wamezoea, halafu tunaanza Unguja tunaenda kumaliza Pemba, hiyo ni tofauti nyingine ambayo mwaka huu tumechezesha Mapinduzi kwa kushirikisha maeneo yote, Unguja imechezwa na Pemba pia imechezwa na kila mmoja amepata nafasi ya kushuhudia mashindano haya,” amesema Kabwanga.