Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Beki afichua ya Fiston Mayele, John Bocco

MASAI Pict

KATIKA toleo lililopita, tuliona historia ya nahodha wa Mtibwa Sugar, Oscar Masai jinsi alivyopata umaarufu alionao kupitia simu ya Aishi Manula, ambaye alimuita Dar es Salaam aje kufanya majaribio ya kucheza soka katika klabu ya Azam FC akibainisha hata nauli alitumiwa na kipa huyo wa zamani wa zamani wa Simba, huku akifunguka kwamba alitembea kwa miguu kutoka Mbagala hadi Chamazi kwani nauli aliyotumiwa na Manula iliishia hapo ambako alikuwa amebakiwa na Sh300 tu. Endelea naye...


AGGREY MORRIS KAMPA NGUVU

KATIKA sehemu iliyopita ya mahojiano na Oscae Masai, alisimulia namna alivyosaidiwa na Aishi Manula kujiunga na Azam FC akianzia timu ya vijana hadi ya wakubwa kabla ya maisha mengine kuendelea. Pia alizungumzia namna klabu hiyo tajiri nchini ilivyompa maisha na kumiliki baadhi ya mali na kukuza jina lake.

Leo anaendelea kusimulia ubora wa nyota Ligi Kuu Bara akiwataja baadhi Dickson Job na Ibrahim Hamad 'Bacca' lakini anamsifia Aggrey Morris kwa kuwa kama kioo chake na kudumu kucheza nafasi moja licha ya awali kucheza tofauti na anayocheza sasa. Endelea naye...

MASA 01

MORRIS KAMBADILISHA NAMBA

Anasema awali alikuwa akicheza kiungo mkabaji lakini alipofika Azam FC na kukutana na beki wa zamani wa klabu hiyo, Aggrey Morris mambo yalibadilika na kujikuta akicheza beki wa kati baada ya kuvutiwa na namna ya uchezaji wake.

“Nilikuwa timu B Azam FC, nilikuwa namtazama sana Agrey Morris na nilikuwa navutiwa sana na upambanaji wake na kutamani kufikia uwezo wake, hivyo nakiri ndiye mchezaji aliyekuwa akinipa nguvu ya kupambana,” anasema na kuongeza hata ubora alionao sasa ni kutokana na kujifunza mengi kutoka kwake.

MASA 02

JOB, BACCA UKUTA WA CHUMA

Hakuna asietambua ubora wa Dickson Job na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ mastaa wa Yanga na timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kutokana na wawili hao kujitengenezea utawala kwenye timu hizo na Masai analiona hilo.

“Kwenye beki wa kati hivi sasa huwezi kuacha kumtaja Job na Bacca. Hawa wametengeneza pacha nzuri na bora kuanzia klabu wanayocheza na Taifa Stars wamekuwa watulivu na wanafanya kazi nzuri,” anasema na kuongeza;

“Navutiwa pia na aina yao ya uchezaji, wamekuwa imara sana eneo hilo hakuna mpenda mpira ambaye anaweza kupingana na hilo.”

MASA 03

BOCCO, MAYELE HAIJAWAHI KUTOKEA

Anasema kazi yake inakuwa ngumu kutokana na aina ya washambuliaji anaokutana nao na kukiri kwa John Bocco na Fiston Mayele alivuja jasho kutokana na ubora wao na wazuri kukaa maeneo ya hatari.

“Ligi kuu ina washambuliaji wengi wazuri na wapambanaji, lakini tangu nimeanza kucheza soka la ushindani nimekutana na wawili wagumu ambao nilikuwa nikimaliza mechi najua nimetoka kuvuja jasho kutokana na mikikimikiki niliyokuwa nakutana nayo,” anasema na kuongeza:

“Kulikuwa na John Bocco na Fiston Mayele, ni aina ya washambuliaji ambao nilikuwa nikikutana nao walikuwa wananipa kazi ngumu ya kufanya na nikimaliza dakika 90 najua kazi imefanyika. Sina maana waliopo sio bora, ni bora ila nimewataja hao kwa sababu walikuwa wananipa mechi ngumu sana.”

“Pia kuna Anuary Jabir, Sinchimba na wengine wengi, nikisema nitaje wote hatuwezi kumaliza leo, mabeki pia tunapitia changamoto lakini umakini na kutumia akili nyingi ndiyo kitu pekee kinachotufanya tuzisaidie timu zetu zifanye vizuri kwa kuruhusu mabao machache.”

MASA 04

NYOTA WA KIGENI CHACHU YA USHINDANI

Shirikisho la soka Tanzania (TFF) kwenye mabadiliko ya kanuni msimu huu imepitisha klabu kutumia nyota wao wote wa kigeni 12 walio wasajili tofauti na awali walikuwa wanaruhusiwa kucheza wachache huku wengine wakisubiri, hilo wala halijamshtua Masai na anasema ndiyo kwanza wanaongezewa hasira ya kupambana.

“Wanatuongezea hasira ya kupambana na kushindania namba. Idadi iliyopo ya wachezaji 12 ni kubwa na inatosha kupata kikosi cha kwanza, naamini hii inatufanya wazawa tuongeze juhudi ili tuwe bora."

“Hakuna mchezaji ambaye anapenda kukaa benchi, hivyo tutapambana kuhakikisha tunapata nafasi na hata hao wa kigeni wasitarajie tutawaachia namba, kila mmoja atapambania namba kwa kumshawishi kocha mazoezini.”

MASA 05

DAUD KITAMBAA HADI JEZI NO

“Kipindi natua Mtibwa Sugar nikitokea Geita Gold nilikuta kitamba cha unahodha kipo kwa Dickson Daud na Issa Rashid na baada ya nahodha mkuu uamua kupumzika na kuingia kwenye uongozi, ndipo viongozi na benchi la ufundi walipofanya uamuzi wa kunipa kitambaa.”

“Pia ni kwa kuwa Daud aliamua kuachana na uchezaji na kuingia kwenye uongozi, niliamua kuchukua hadi jezi namba tatu aliyokuwa anaivaa kutoka 58 ambayo ndiyo nilikuwa navaa tangu nilipopandishwa Azam FC timu ya vijana hadi wakubwa,” anasema nahodha huyo ambaye mwaka 2019 alipelekwa kwa mkopo Namungo baada ya kupandishwa Ihefu chini ya Zuberi Katwila, akarudishwa Azam, akatolewa tena Geita Gold na kucheza miezi sita na sasa yuko Mtibwa Sugar.

Anasema hakuchagua kuwa kiongozi bali kocha na viongozi ndio waliompa nafasi ya kuvaa kitambaa cha unahodha na ni heshima kwake kwani ndiyo kwanza alikuwa mgeni kwenye kikosi huku akiweka wazi uongozi ni wito.


MICHORO MWILINI, MAMA ANAHUSIKA

Hakuna mtoto asiyejua thamani ya mama yake kama anavyothibitisha Masai kwa kuamua kuchora jina lake mwilini kwa mtindo wa 'Tattoo'.

Masai amechora 'tattoo' tatu na anafunguka maana zake.

“Moja ni majina ya wazazi wangu na wadogo zangu, hapa kuna jina la baba, mama na wanangu, dada zangu sijawaandika. Sisi tumezaliwa wanne kwetu. Nyingine ni mkono wa shukurani na nyingine hii ni  kuna jina la Mbui ambalo ndilo nimekuwa nikilitumia kwenye jezi yangu.”

“Mbui ni jina la utamaduni ambao upo nyumbani kwetu, pia ni mila za kwetu, watu wa huko wanaelewa namaanisha nini,” anasema beki huyo na kufichua kama asingecheza soka angekuwa mkulima wa mpunga.

MASA 06

ANATAMANI KUCHEZA NA MWAIKENDA

Ubora anaouonyesha akicheza beki ya kulia hadi kuwa kinara wa upachikaji mabao msimu uliopita kwa wachezaji wanaocheza nafasi ya beki, siyo bahati ni uwezo, lakini Masai anamtaja Lusajo Mwaikenda ni pacha yake bora wakicheza pamoja beki ya kati.

“Ni mabeki wengi wanafanya vizuri na natamani kucheza nao ila kwa Mwaikenda ni bora zaidi kwani tayari tumeshawahi kufanya hivyo tukiwa wote Azam FC, sina maana ninaocheza nao sasa ni wabaya hapana,” anasema na kuongeza;

“Nimecheza na mabeki wengi kwenye timu mbali mbali nilizocheza nakiri kuwa pacha yangu na Mwaikenda ni bora licha ya watu kuto kufahamu ni mzuri pia akicheza beki ya kati nimecheza naye tangu timu ya vijana anauwezo mkubwa.”


ANAVYOIONA LIGI AKIITAJA YANGA

Licha ya kuchezwa mechi mbili tu kabla ya kupisha kalenda ya CAF kwa timu za taifa, anasema ligi kuu msimu wa 2025-26 ni ngumu tofauti na misimu miwili nyuma kabla hawajashuka.

“Ligi ni ngumu sana msimu huu na mapema sana picha limeonekana, timu ambazo zilitarajiwa kupata matokeo zimewashangaza wadau, mfano mechi ya Mbeya City na Yanga hakuna mtu alitarajia itaisha kwa suluhu lakini mambo yalikuwa magumu na matokeo kila mmoja aliyaona,” anasema na kuongeza;

“Ukiondoa hilo, pia hata matokeo mzunguko wa kwanza hakuna iliyoshinda mabao mengi kama misimu ya nyuma na timu inafungwa mabao hadi matano, mechi zilichezwa idadi ndogo ya mabao imefungwa mapema tu, imeonekana ni msimu mgumu.”

Masai anasema timu nyingi zimefanya usajili bora na zimejipanga kuhakikisha zinafanya vizuri, hivyo wanatarajia ushindani wa kutosha na timu iliyojiandaa vizuri ndiyo itakayopata matokeo mazuri.


KIKOSI CHAKE BORA

Licha ya ligi kuchezwa mechi mbili haijamzuia Masai kutaja kikosi chake bora kwa kufanya mchanganyiko kutoka timu mbalimbali huku akiweka wazi wanastahili na namba zinawabeba siyo kwa msimu huu pekee ambao anasema ni mapema sana.

“Golini naanza na Djigui Diarra kwa sababu ni kipa ambaye tangu ametua Tanzania amekuwa na mwendelezo wa ubora hadi sasa, namba mbili Mwaikenda namba za msimu ulioisha zinambeba amekuwa bora sana eneo lake, tatu Mohammed Hussein Tshabalala;

“Nne na tano ni Job, Bacca hawa wana ufalme wao eneo hilo sio Yanga tu hadi Taifa Stars sita naenda na Khalid Aucho saba Maxi Nzengeli nane Duke Abuya, tisa Prince Dube, kumi Feisal Salum na kumi na moja Pacome Zouzoua.”