Azam FC ilivyowarejesha mastaa bongo
Muktasari:
- Wakati dirisha hili la usajili likifunguliwa, wapo wachezaji mbalimbali walioichezea Ligi Kuu kwa miaka ya hivi karibuni na kupata nafasi ya kucheza hadi nje ya nchi, japo Azam iliwarejesha tena Bongo kama ambavyo Mwanaspoti linavyowaelezea.
DIRISHA dogo la usajili limefunguliwa rasmi tangu Januari 1, 2026 na linatarajiwa kufungwa Januari 30, 2026, likiwa na lengo la kutoa nafasi kwa timu kujiimarisha kutokana na mashindano mbalimbali na kuwafungulia nyota wengine mlango wa kutokea.
Wakati dirisha hili la usajili likifunguliwa, wapo wachezaji mbalimbali walioichezea Ligi Kuu kwa miaka ya hivi karibuni na kupata nafasi ya kucheza hadi nje ya nchi, japo Azam iliwarejesha tena Bongo kama ambavyo Mwanaspoti linavyowaelezea.
SHAABAN IDD CHILUNDA
Nyota huyu anayeichezea msimu huu TRA United, alianzia soka lake katika timu ya vijana ya Azam (U-19) mwaka 2016 na alipandishwa hadi ya wakubwa kutokana na kiwango bora alichokuwa anakionyesha kiasi cha kupata dili la kwenda Hispania.
Kiwango bora alichokionyesha Chilunda kilimfanya kujiunga na timu za CD Tenerife na Club Deportivo Izarra za Hispania, ingawa mwaka 2019 alirejea Azam, kisha kutimkia Moghreb Athletic de Tetouan ya Morocco aliyoitumikia kuanzia 2020 hadi 2021.
Hata hivyo, maisha ya Morocco kwa mshambuliaji huyo hayakuwa mazuri sana na kujikuta akirejea tena Azam mwaka 2022, japo aliondoka 2023, kisha akajiunga na Simba na baadaye akatua KMC aliyoachana nayo na kujiunga na kikosi cha TRA United.
ADOLF MTASINGWA
Adolf Mtasingwa Bitegeko, ni miongoni mwa viungo wazuri wa kikosi cha Azam kutokana na umaridadi wake katika eneo hilo na baada ya nyota huyo kucheza soka nje ya nchi kwa muda mrefu, matajiri wa Jiji la Dar es Salaam wakamrejesha tena.
Bitegeko aliyewahi kuzichezea timu mbalimbali za KR Reykjavik, Keflavik na Volsungur IF zote za Iceland, alirejea Azam dirisha dogo la Januari 2024, baada ya kiungo huyo awali kukitumikia pia kikosi hicho akiwa katika akademia.
Baada ya Mtasingwa kukaa nje ya uwanja kwa takribani miezi minane akiuguza majeraha yake ya kifundo cha mguu, nyota huyo kwa sasa amerejea mazoezini na kuungana na wachezaji wenzake, ikiwa ni ishara nzuri kwa kikosi hicho kwa mechi zijazo.
Nyota huyo mara ya mwisho kuonekana uwanjani ni katika mechi ya Ligi Kuu Bara ambayo Azam ilishinda mabao 2-0, dhidi ya maafande wa Mashujaa Februari 15, 2025, hivyo, urejeo wake unaongeza upana wa timu hiyo kwenye eneo la kiungo.
Hata hivyo, licha ya urejeo wa nyota huyo ila, timu hiyo inayonolewa na Mkongomani Florent Ibenge imekuwa na wigo mpana wa viungo bora wa kati wenye ushindani, wakiongozwa na, Himid Mao Mkami, Sadio Kanoute, Yahya Zayd na James Akaminko.
HIMID MAO MKAMI
Nyota huyo anayejulikana kwa jina la ‘Ninja’, alianzia maisha yake ya soka Azam mwaka 2009, baada ya kupandishwa kikosi cha wakubwa akitokea cha vijana kilichotwaa ubingwa wa Ligi chini ya miaka 20, maarufu (Uhai Cup) mara mbili mfululizo.
Pia, Himid mwenye umri wa miaka 33, alikuwa miongoni mwa wachezaji wa Azam waliotwaa taji la kwanza la Ligi Kuu msimu wa 2013-2014, ingawa aliondoka kwa matajiri hao wa Chamazi mwaka 2018, kisha kwenda Misri kujiunga na Klabu ya Petrojet.
Baada ya kujiunga na Petrojet, aliitumikia kwa msimu mmoja kisha akajiunga na Enppi SC ya huko huko ambayo nayo alihudumu kwa mwaka mmoja, ingawa aliondoka tena na kujiunga na Entag El Harby na baadaye akatua Ghazl El Mahalla zote za Misri.
Kiungo huyo amerejea Azam msimu huu akiwa mchezaji huru baada ya mkataba wake kumalizika katika Klabu ya Talaea El Gaish ambayo ilikuwa ni timu yake ya mwisho kuichezea huko Misri, huku akiendelea kuonyesha uwezo mkubwa kwenye kikosi hicho.
Himid ambaye ni mtoto wa nyota wa zamani wa Pamba, Mtibwa Sugar na Moro United, Mao Mkami ‘Ball Dancer’, aliibuliwa na aliyekuwa Kocha wa Taifa Stars, Mbrazil Marcio Maximo katika kituo cha kulea vipaji cha TFF cha Tanzania Soccer Academy (TSA).
Maximo aliyeifundisha pia Yanga na msimu huu KMC kabla ya kuachana nayo Desemba 6, 2025, alimuita Himid timu ya taifa ya Tanzania ili kuongeza ushindani enzi hizo na mastaa wengine, Henry Joseph Shindika, Shaban Nditi na Athuman Idd ‘Chuji’.
SHOMARI KAPOMBE
Beki huyo wa kulia asiyechuja kuanzia ngazi ya klabu hadi timu ya taifa ya Tanzania, aliondoka Simba Agosti 21, 2013, kisha kwenda kujiunga na AS Cannes iliyokuwa inashiriki Ligi Daraja la nne Ufaransa, japo aliitumikia hadi mwaka 2014.
Mwaka 2014, nyota huyo alirejea tena nchini ingawa safari hii alijiunga na kikosi cha Azam kwa mkataba wa miaka mitatu na baada ya kuisha mwaka 2017, alijiunga na Simba anayoendelea pia kuitumikia hadi sasa akiwa katika kiwango bora.
MUHSINI MALIMA
Muhsini Malima Makame ni nyota mwingine aliyejea nchini baada ya kucheza soka nje ya nchi na amejiunga na kikosi cha Azam Agosti 7, 2025, baada ya kuachana na ZED FC ya Misri, aliyojiunga nayo Agosti 13, 2023, akitokea Dodoma Jiji.
Kiungo huyo mshambuliaji amechezea klabu mbalimbali za Coastal Union ya Tanzania, huku akichezea timu za vijana chini ya miaka 19 ya Red Star Belgrade (U19) au Crvena Zvezda (U19) ya Serbia, huku akitazamiwa kuongezea nguvu kikosi cha Azam.
Malima aliyesaini mkataba wa mwaka mmoja na Azam wenye kipengele cha kuongeza mwingine, bado hajapata nafasi ya kutosha ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Kocha Florent Ibenge kutokana na ushindani wa namba uliopo ndani ya timu hiyo.