VAR yainyima bao DR Congo
Muktasari:
- Mshambuliaji Nathanael Mbuku aliisawazishia timu yake kwa bao zuri katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi. Hata hivyo, mwamuzi Felix Zwayer alilikataa baada ya kwenda kuangalia tukio hilo kwenye skrini kufuatia ushauri wa VAR.
DALLAS, MAREKANI: VAR kwa mara nyingine imeendelea kuzionea timu za Afrika baada ya Ghana sasa ni DR Congo walinyimwa bao la kuvutia dhidi ya Uzbekistan, uamuzi ambao uliibua hasira kubwa kutoka kwa mashabiki na wachambuzi wa soka.
Mshambuliaji Nathanael Mbuku aliisawazishia timu yake kwa bao zuri katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi. Hata hivyo, mwamuzi Felix Zwayer alilikataa baada ya kwenda kuangalia tukio hilo kwenye skrini kufuatia ushauri wa VAR.
Baada ya mapitio ya video, Zwayer aliamua kuwa Mbuku alimgonga usoni mchezaji wa Uzbekistan, Sherzod Nasrullaev, kwa mkono wake alipokuwa akikimbia mwanzoni mwa shambulio lililozaa bao.
Uamuzi huo uliwaudhi mashabiki wengi pamoja na mchambuzi wa BBC, Chris Sutton.
Sutton amesema: "Siamini kabisa uamuzi huu. Ni kweli mkono wake ulitingishika, lakini je, ilikuwa kwa makusudi?
"Alikuwa anajaribu tu kujilinda dhidi ya mpinzani. Huu ni uamuzi dhaifu sana. Ni uamuzi mwepesi kupita kiasi.
"Hasa katika Kombe la Dunia ambalo waamuzi wamekuwa wakiruhusu mchezo uwe na mawasiliano ya kimwili zaidi."
Mashabiki wengi pia walionyesha kutoridhishwa kwao kwenye mitandao ya kijamii.
Mmoja aliandika kwenye X:"Bao la DR Congo kukataliwa ni kituko kabisa."
Mwingine aliandika kwenye Reddit:
"Ni uamuzi wa kusikitisha. Hii ndiyo aina ya uamuzi wa waamuzi unaoua kabisa ladha ya mchezo."
Shabiki mwingine amesema:
"Huenda huu ukawa uamuzi wa kipuuzi zaidi kuwahi kufanywa na VAR."
Wakati mwingine aliandika:
"Sijawahi kuona matumizi mabaya ya teknolojia kama haya katika mchezo wowote."
Wengine waliuita uamuzi huo kuwa "wa aibu", huku wakimtaka mwamuzi Zwayer kutokubali kushinikizwa na VAR kubatilisha bao hilo.
Katika mchezo huo, Uzbekistan ilianza vizuri baada ya Eldor Shomurodov kufunga bao la mapema kwa mpira wa juu uliompita kipa.
Bao hilo liliifanya Uzbekistan kupanda hadi nafasi ya tatu katika Kundi K, lakini tofauti yao ya mabao iliyochangiwa na kipigo kikubwa walichopata kutoka kwa Ureno, ilimaanisha hawakuwa na nafasi ya kufuzu hatua ya 32 bora.
DR Congo ilisawazisha kupitia mkwaju wa penalti uliopigwa na Yoane Wissa.
Baadaye, Fiston Mayele aliifungia timu yake bao la pili kwa umaliziaji mzuri.
Wissa ameongeza bao lake la pili mwishoni mwa mchezo na kuifanya DR Congo ishinde kwa mabao 3-1.
Ushindi huo uliifanya DR Congo kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye kundi na kufuzu hatua ya 32 bora, ambako itakutana na England mjini Atlanta siku ya Jumatano.