Mayele, Wissa waibeba DR Congo ikitinga 32 bora
Muktasari:
- Mapema tu DR Congo imeruhusu bao likifungwa dakika ya 10, mfungaji akiwa Eldor Shomuridov akimalizia asisti ya kiungo Akmal Mozgovoy.
DR Congo imefanya kweli ikitoka nyuma na kushinda mchezo dhidi ya Uzbekistan, ikikata tiketi ya hatua ya 32 bora kwenye fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea.
Mapema tu DR Congo imeruhusu bao likifungwa dakika ya 10, mfungaji akiwa Eldor Shomuridov akimalizia asisti ya kiungo Akmal Mozgovoy.
DR Congo ilikaribia kusawazisha dakika ya 17 kupitia mshambuliaji Nathanael Mbuku, lakini VAR ikalikataa na matokeo kubaki hivyo mpaka timu hizo zikaenda mapumziko.
Kipindi cha pili kocha Sebastian Desabre wa DR Congo amefanya mabadiliko akimtoa mshambuliaji Cedric Bakambu dakika ya 51 na nafasi yake ikichukuliwa na Mayele.
Mabadiliko hayo yameiongezea kasi DR Congo ambapo imefanikiwa kusawazisha bao kupitia Wissa dakika ya 68 kwa mkwaju wa penalti baada ya mchezaji wa Uzbekistan kucheza vibaya ndani ya eneo lao la hatari.
Mayele ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa Yanga, ameiweka DR Congo mbele dakika ya 78
akifunga bao la kiufundi akiwazidi akili mabeki na kipa wa Uzbekistan akitumia krosi ya Meshack Elia.
Wissa tena akaipa DR Congo bao la tatu akifunga kwa shuti kali dakika ya 90+1 akitumia asisti ya Elia.
Mpaka mwisho wa mchezo DR Congo imefanikiwa kupata ushindi wake wa kwanza ikiichapa Uzbekistan mabao 3-1 na kukata tiketi ya kwenda kucheza hatua ya mtoano.
Kwenye msimamo wa Kundi E Colombia imemaliza kinara kwa kufikisha pointi saba, Ureno ikiwa nafasi ya pili na pointi tano, huku DR Congo ikiwa ya tatu na pointi nne ilhali Uzbekistan ipo mkiani bila pointi.