Utabiri Argentina, Ufaransa fainali, England mmh!
Muktasari:
- England imepewa nafasi ya tatu kwa uwezekano wa kutinga nusu fainali kwa asilimia 42. Mbele yake ni Ufaransa yenye asilimia 50 na mabingwa watetezi Argentina wenye asilimia 58.
NEW YORK, MAREKANI: KOMPYUTA maalumu ya kutabiri matokeo ya mashindano (supercomputer) imetabiri kuwa Argentina na Ufaransa zitakutana tena kwenye fainali ya Kombe la Dunia 2026, kama ilivyokuwa mwaka 2022.
Baada ya hatua ya makundi kumalizika, mfumo huo umehesabu uwezekano wa kila timu kufika katika kila hatua ya mashindano kwa asilimia.
England imepewa nafasi ya tatu kwa uwezekano wa kutinga nusu fainali kwa asilimia 42. Mbele yake ni Ufaransa yenye asilimia 50 na mabingwa watetezi Argentina wenye asilimia 58.
Ili England ifike hatua hiyo, italazimika kwanza kuifunga DR Congo katika hatua ya 32 bora. Baadaye itacheza na mshindi kati ya Mexico na Ecuador kabla ya robo fainali dhidi ya mojawapo ya Brazil, Japan, Norway au Ecuador.
Iwapo itafika nusu fainali, njia hiyo inaonyesha uwezekano mkubwa wa kukutana na Argentina. Hata hivyo, supercomputer inatabiri kuwa safari ya England itaishia hapo.
Kwa mujibu wa makadirio hayo, Argentina ina nafasi ya asilimia 34 kufika fainali, huku Ufaransa ikiwa na asilimia 31. England imepewa nafasi ya asilimia 27 ya kucheza fainali itakayofanyika mjini New York Uwanja wa New Jersey tarehe 19 Julai.
Argentina inaonekana kuwa na njia rahisi zaidi kuelekea fainali. Kwanza itakutana na Cape Verde katika hatua ya 32 bora, kisha mshindi kati ya Australia na Misri katika hatua inayofuata.
Baada ya hapo, robo fainali inaweza kuwakutanisha na mojawapo ya Ghana, Colombia, Algeria au Uswisi.
Kwa mujibu wa utabiri huo, huenda Argentina ikapata mtihani mkubwa wa kwanza nusu fainali dhidi ya England au Brazil, huku ikipewa nafasi kubwa zaidi ya kusonga mbele katika kila hatua hadi fainali.
Kwa upande wa Ufaransa, safari yake inaonekana kuwa ngumu zaidi. Itaanza kwa kucheza dhidi ya Sweden katika hatua ya 32 bora. Mshindi wa mechi hiyo atakutana na mshindi kati ya Ujerumani na Paraguay.
Katika robo fainali, wapinzani wanaoweza kujitokeza ni Afrka Kusini au Canada, hatua inayofuata atacheza na Uholanzi au Morocco.
Baada ya hapo, nusu fainali inaweza kuwapeleka dhidi ya timu kutoka upande wenye Hispania au Ureno.
Hatimaye, supercomputer inatabiri kuwa Ufaransa itaishinda Argentina kwenye fainali na kutwaa taji la Kombe la Dunia 2026, ikipewa nafasi ya asilimia 21 ya kuwa mabingwa.
Iwapo utabiri huo utatimia, itakuwa hitimisho la kihistoria kwa kocha Didier Deschamps, ambaye tayari aliiongoza Ufaransa kutwaa Kombe la Dunia mwaka 2018 katika kipindi chake cha miaka 14 akiwa kocha wa taifa hilo.