Uwanja mpya Man United usipime
Muktasari:
- Ardhi hiyo imenunuliwa kutoka kampuni ya Indurent na ipo takriban mita 350 kutoka Old Trafford.
LONDON, England: Manchester United wamepiga hatua muhimu katika mpango wao wa kujenga uwanja mpya wa kisasa wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 100,000 baada ya kupata ekari 25 za ardhi katika eneo la Trafford Park.
Ardhi hiyo imenunuliwa kutoka kampuni ya Indurent na ipo takriban mita 350 kutoka Old Trafford.
Vyanzo vya ndani ya klabu vimesema kuwa eneo la Freightliner, ambalo hapo awali lilitajwa kuwa muhimu kwa mradi huo, halihitajiki tena kwa ujenzi wa uwanja mpya.
Manchester United pia wanaendelea na mazungumzo ya kununua ardhi zaidi, huku viongozi wakuu wa klabu wakiamini hakutakuwa na changamoto yoyote katika kukamilisha mchakato huo.
Ardhi hiyo ipo upande wa kaskazini magharibi mwa Old Trafford, kati ya barabara za Wharfside, Europa na John Gilbert.
Mpango mkubwa wa kuifufua Old Trafford
Mpango kamili wa maendeleo ya eneo la Old Trafford unatarajiwa kutangazwa rasmi tarehe 9 Julai. Baada ya hapo, klabu itaingia katika hatua ya mwisho ya kubuni uwanja kwa kushirikiana na mashabiki.
Mmiliki mwenza wa klabu, Jim Ratcliffe, amesema hapo awali kuwa kujenga upya uwanja katika eneo lile lile la Old Trafford ni jambo la wazi na la busara baada ya uwekezaji wake ndani ya klabu mwaka 2024.
Mwezi Machi 2025, United walionyesha michoro ya awali ya uwanja huo mpya unaokadiriwa kugharimu pauni2 bilioni.
Awali klabu ilikuwa imelenga kuhamia katika uwanja huo mwaka 2030, lakini sasa ratiba hiyo inaonekana haitafikiwa.
Hata hivyo, viongozi wa klabu wanaamini uwanja huo utakuwa tayari kutumika kabla ya Kombe la Dunia la FIFA kwa wanawake 2035 na unaweza kuwa moja ya viwanja vitakavyotumika katika mashindano hayo.
Mwisho wa enzi ya Old Trafford?
Old Trafford imekuwa nyumbani kwa Manchester United kwa miaka 116, lakini katika miaka ya karibuni umekumbwa na matatizo mbalimbali.
Mashabiki wamekuwa wakilalamikia kuhusu matatizo ya uvujaji wa paa wakati wa mvua, miundombinu iliyochakaa pamoja na huduma na vifaa visivyoendana na hadhi ya klabu kubwa duniani.
Licha ya kuwa uwanja mkubwa zaidi wa klabu nchini Uingereza, Old Trafford haukuchaguliwa kuwa miongoni mwa viwanja vitakavyotumika katika fainali za Euro 2028.
Kupatikana kwa ardhi hii mpya kunaonekana kuwa hatua kubwa kuelekea kutimiza ndoto ya Manchester United ya kujenga moja ya viwanja vikubwa na vya kisasa zaidi duniani, kitakachokuwa alama mpya ya klabu katika zama zijazo.