Jonas Adjetey; Fundi wa kupaka rangi aliyemzuia Harry Kane Kombe la Dunia
Muktasari:
- Miaka michache iliyopita, maisha ya Adjetey yalikuwa tofauti kabisa na yalivyo leo. Kama vijana wengi nchini Ghana wenye ndoto za kucheza soka la kulipwa, alikabiliwa na changamoto nyingi katika safari yake ya kufikia mafanikio. Fursa zilikuwa chache, ushindani ulikuwa mkubwa na kufika katika kiwango cha juu cha soka kulionekana kuwa ndoto ya mbali.
FAINALI za Kombe la Dunia 2026 zimeendelea kutoa simulizi nyingi za kusisimua, matokeo ya kushangaza na hadithi za kuvutia, lakini simulizi ya Jonas Adjetey ni miongoni mwa zile zinazogusa zaidi hisia za mashabiki wa soka duniani.
Miaka michache iliyopita, maisha ya Adjetey yalikuwa tofauti kabisa na yalivyo leo. Kama vijana wengi nchini Ghana wenye ndoto za kucheza soka la kulipwa, alikabiliwa na changamoto nyingi katika safari yake ya kufikia mafanikio. Fursa zilikuwa chache, ushindani ulikuwa mkubwa na kufika katika kiwango cha juu cha soka kulionekana kuwa ndoto ya mbali.
Ili kujikimu kimaisha, Adjetey alikuwa akifanya kazi ya upakaji rangi kwenye majengo huku akicheza soka alipopata nafasi. Wakati wengine wangeweza kukata tamaa kutokana na ugumu wa maisha, yeye aliendelea kuamini kuwa siku moja juhudi zake zingelipa. Aliendelea kufanya mazoezi, kuimarisha kiwango chake na kupambana kwa bidii ili kutimiza ndoto yake.
Leo hii, mambo yamebadilika kwa kiasi kikubwa.
Kutoka kuwa fundi wa kupaka rangi nchini Ghana, sasa Jonas Adjetey anaiwakilisha nchi yake katika Kombe la Dunia, mashindano makubwa zaidi ya soka duniani. Anacheza dhidi ya baadhi ya wachezaji bora kabisa duniani huku mamilioni ya mashabiki wakimtazama kutoka kila kona ya dunia.
Katika mchezo wa hatua ya makundi dhidi ya England, Adjetey alionyesha kwa nini safari yake ni ya kipekee. Ghana ilifanikiwa kupata sare ya bila kufungana dhidi ya moja ya timu zinazotajwa kuwania ubingwa wa dunia, matokeo ambayo yameiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua inayofuata.
Ingawa England ilitawala umiliki wa mpira na kujaribu mara kadhaa kuutoboa ukuta wa Ghana wakiongozwa na mshambuliaji, Harry Kane, lakini safu ya ulinzi ya timu hiyo ilisimama imara.
Adjetey alikuwa miongoni mwa nyota waliotoa mchango mkubwa katika kuhakikisha Ghana inatunza lango lake na kumzuia Kane na wenzake wasitikise nyavu licha ya mashuti 19 kupigiwa. Kane akipiga mashuti matatu.
Beki huyo wa kati alionyesha utulivu mkubwa, nidhamu ya hali ya juu na uwezo wa kusoma mchezo katika nyakati muhimu. Aliokoa mashambulizi kadhaa ya England, akashinda mapambano ya ana kwa ana na kuiongoza safu ya ulinzi kwa kujiamini dhidi ya baadhi ya washambuliaji hatari zaidi duniani.
Kwa mashabiki wengi, sare hiyo ilikuwa matokeo muhimu kwa Ghana. Lakini kwa Adjetey, ilikuwa zaidi ya matokeo ya mchezo. Ilikuwa ni ushahidi wa safari ndefu aliyopitia kutoka katika maisha ya kawaida hadi kufika kwenye jukwaa kubwa zaidi la soka duniani.
Adjetey aliyezaliwa Desemba 13, 2003 (umri miaka 22) huko Accra, Ghana, mbali na kucheza beki wa kati, pia ana uwezo wa kucheza beki wa kulia ambapo sasa anaitumikia VfL Wolfsburg ya Ujerumani aliyojiunga nayo Februari 2026 akitokea FC Basel ya Uswisi.
Nyota huyo kuanzia mwaka 2013 hadi 2019 alikuwa akicheza Teshie Football Academy, kisha 2019 hadi 2020 akawa pale Great Olympics, ndipo 2020 hadi 2022 akaitumikia Berekum Chelsea, hizi zote ni za Ghana, kabla ya mwaka 2022 kusajiliwa na FC Basel aliyoitumikia hadi Februari 2026 ndipo akatua Wolfsburg kwa uhamisho uliogharimu euro milioni 10 (Sh29.9 bilioni za Tanzania) akisaini mkataba hadi 2030.
Pia ameanza kuichezea Ghana ya wakubwa mwaka 2024, kabla ya hapo, kuanzia 2022 alikuwa akicheza Ghana U-20.
“Accra ni jiji kubwa sana lenye wilaya nyingi. Ni jiji ambalo halitulii kamwe,” anasema kuhusu nyumbani kwao.
“Kila mtu anafanya kazi, kuna nguvu nyingi na jasho la kutosha katika maisha ya kila siku.”
Anaendelea kwa kusema: “Hatukuwa na vitu vingi, lakini wazazi wangu walijitolea kwa kila kitu kwa ajili yangu na dada yangu.”
Kusimama bila kufanya chochote haikuwa chaguo. Hata alipokuwa mtoto, Adjetey alikuwa akifanya majukumu kadhaa kwa wakati mmoja.
“Unaenda shule, unacheza mpira wa miguu na unawasaidia wazazi wako. Mambo matatu, kila siku.
“Kila mtu hucheza mpira mitaani. Ni rahisi sana kuanza kucheza, lakini ni vigumu sana kupiga hatua na kufanikiwa katika mchezo huo,” anasema.
Anakumbuka kipindi ambacho hata kupata viatu vipya vya mpira haikuwa jambo la kawaida.
Anaendelea kusimulia: “Nilihitaji viatu vya mazoezi, lakini sikuwa na pesa. Hivyo ilinibidi kufanya kazi.”
Saa 11 alfajiri alikuwa akielekea kwenye eneo la ujenzi pamoja na marafiki zake ambapo anasema: “Nilikuwa nikisaidia kazi huko ili nipate fedha za kununua viatu.”
Kutoka kupaka rangi majengo nchini Ghana hadi kucheza kwa kiwango cha juu dhidi ya England katika Kombe la Dunia, Jonas Adjetey ameonyesha kuwa hakuna ndoto iliyo kubwa sana kwa mtu mwenye imani, juhudi na moyo wa kupambana.