Uholanzi yatinga 32 bora, Tunisia ikiaga kwa aibu
Muktasari:
- Mapema tu dakika ya tatuTunisia ndio imeanza kuutengeneza ushindi wa Uholanzi, baada ya kiungo wake Ellyes Skhiri kujifunga wakati akitaka kudhibiti shambulizi la wapinzani.
Uholanzi imemaliza kibabe mechi za makundi ikipata ushindi mzuri wa mabao 3-1 dhidi ya Tunisia ambayo imeacha rekodi mbaya ikiaga fainali hizo za Kombe la Dunia 2026.
Mapema tu dakika ya tatuTunisia ndio imeanza kuutengeneza ushindi wa Uholanzi, baada ya kiungo wake Ellyes Skhiri kujifunga wakati akitaka kudhibiti shambulizi la wapinzani.
Dakika nne baadaye Uholanzi imeandika bao la pili kupitia mshambuliaji Brian Brobbey akimalizia vizuri asisti ya beki Virgil van Dijk.
Bao hilo limemfanya Brobbey kufikisha mabao matatu kwenye mechi tatu za makundi akiongoza kwa ufungaji kwenye kikosi cha Uholanzi mpaka sasa, timu hizo zikienda mapumziko huku Wadachi wakiongoza kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili Tunisia imerudi na nguvu na kufanikiwa kupata bao kupitia shambulizi la kona mfungaji akiwa Hazem Mastouri kwa kichwa dakika ya 54.
Uholanzi imekamilisha ushindi wake dakika ya 62 kwa bao la Jan Paul van Hecke akimalizia asisti ya kiungo Tijjani Reijnders, mchezo ukimalizika kwa Wadachi kushinda mabao 3-1.
Ushindi huo umeifanya Uholanzi kufikisha pointi saba na kuongoza kundi F, Japan ikimaliza ya pili na alama tano wakati Sweden ikiwa ya tatu kufuatia kuvuna pointi nne.
Tunisia imemaliza mkiani mwa kundi hilo bila pointi ikiweka rekodi ya timu iliyoruhusu mabao mengi 12, huku ikifunga mawili na pia ikiwa ndio timu ya kwanza kufukuza kocha baada ya kucheza mchezo wake wa kwanza.