Mourinho akaribia rekodi ya Arsene Wenger
Muktasari:
- Mourinho, mwenye umri wa miaka 63, anatakiwa kutopoteza mechi yoyote kati ya nne zilizobaki katika Ligi Kuu ya Ureno msimu huu, huku kikosi chake kikiwa kimecheza mechi 30 bila kuonja machungu ya kupoteza.
Jose Mourinho, anakaribia kufikia rekodi ya mpinzani wake wa zamani, Arsene Wenger, kwa kumaliza msimu wa ligi bila kupoteza mechi.
Lakini tofauti iliyopo ni kwamba, kocha huyo wa zamani wa Chelsea ambaye hivi sasa anainoa Benfica, anaweza asitwae taji la ligi kwa heshima hiyo kutokana na nafasi iliyopo timu hiyo kwa sasa.
Mourinho, mwenye umri wa miaka 63, anatakiwa kutopoteza mechi yoyote kati ya nne zilizobaki katika Ligi Kuu ya Ureno msimu huu, huku kikosi chake kikiwa kimecheza mechi 30 bila kuonja machungu ya kupoteza.
Hata hivyo, rekodi ya ushindi wa mechi 21 na sare tisa iliyoongezeka mwishoni mwa wiki baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Sporting Lisbon, imewawezesha kufika nafasi ya pili ikiwa na pointi 72.
Kwa sasa FC Porto inaoongoza ligi hiyo kwa kishindo ikiwa na pointi 79, baada ya kushinda mechi 25, sare nne na kufungwa mara moja ugenini dhidi ya Casa Pia, Februari 2 mwaka huu.
Wakati huo huo, Sporting ina kiporo cha mchezo mmoja na iko nyuma kwa alama moja tu dhidi ya Benfica baada ya kushinda mechi 22, sare tano na kupoteza mara mbili, jambo linalowaacha na pointi 71.
Kupoteza nafasi mbili za juu kwenye msimamo, kutamaanisha kuwa Benfica itakosa fursa ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Kocha huyo wa zamani wa Chelsea na Manchester United, bado hajajishindia taji lolote akiwa na Benfica tangu alipojiunga tena na klabu hiyo Septemba 2025 ikiwa imepita takribani miaka 25 tangu alipoondoka hapo.
Wakati hayo yote yakijiri, ripoti zinaashiria kuwa Mourinho anaweza kurejea kwa kishindo Real Madrid.
Kwa mujibu wa gazeti la Record, Mourinho anatazamwa kama mbadala wa Alvaro Arbeloa kufuatia timu hiyo ya Hispania kutolewa katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa ilipofungwa na Bayern Munich.
Inasemekana Mourinho amewekwa juu katika orodha ya makocha wanaoweza kuchukua nafasi hiyo, iwapo Arbeloa ambaye ni kocha wa zamani wa akademi ya Real Madrid ataondolewa kazini.
Hizi hapa ni mechi nne zilizosalia za Benfica katika Ligi ya Ureno (Primeira Liga) msimu huu:
Aprili 25, 2026: Benfica vs Moreirense (Nyumbani)
Mei 02, 2026: Famalicão vs Benfica (Ugenini)
Mei 09, 2026: Benfica vs SC Braga (Nyumbani)
Mei 16, 2026: Estoril vs Benfica (Ugenini)