Messi, Mbappe, Haaland wanakabika hivi
Muktasari:
- Mshambuliaji Kylian Mbappe wa Real Madrid tayari ameweka rekodi ya kufunga mabao manne katika mechi mbili alizocheza hadi sasa.
MIAMI, MAREKANI: KOMBE la Dunia huwa la kuvutia zaidi pale mastaa wakubwa wanapoonyesha uwezo wao, washambuliaji wanne bora duniani walionyesho ubora wao katika mashindano hayo.
Mshambuliaji Kylian Mbappe wa Real Madrid tayari ameweka rekodi ya kufunga mabao manne katika mechi mbili alizocheza hadi sasa.
Naye Erling Haaland wa Manchester City ameiiga mafanikio hayo kwa kufunga mabao manne katika mechi mbili na kuiongoza Norway kufuzu kwa hatua ya 32 bora.
Hiyo yote tisa kumi mkongwe Lionel Messi, ameonyesha daraja lake kwa kufunga hat-trick kabla ya kufunga mabao mawili na kuandika rekodi ya kufikisha mabao 18 huku akiiongoza Argentina kusonga mbele.
Mwisho, Harry Kane wa Bayern Munich alifunga mabao mawili katika ushindi wa 4-2 wa England dhidi ya Croatia, sasa mashabiki wanataka kuona kama ataendeleza rekodi hiyo katika mechi ya pili dhidi ya Ghana.
Jinsi ya kuwazuia washambuliaji hawa?
Beki wa zamani wa Everton na Wales, Ashley Williams, alieleza namna ya kukabiliana na kila mmoja wao.
Lionel Messi: Mpeleke maeneo yasiyo hatari
Messi, ambaye atatimiza miaka 39 hivi karibuni, akiweka rekodi mpya ya mabao 18 katika Kombe la Dunia, na kuivunja rekodi ya Mjerumani Miroslav Klose ya mabao 16.
Williams alisema:"Kumzuia Messi ni kazi ya timu nzima. Unahitaji kumlazimisha kuelekea maeneo ambayo hayana madhara makubwa na kuhakikisha hapati nafasi ya kupiga shuti."
Aliongeza kuwa Messi ni mgumu sana kudhibiti kwa sababu ya uwezo wake wa kugeuza mwelekeo, usawa wa mwili na udhibiti bora wa mpira.
Kylian Mbappe: Lazima ubaki makini kila sekunde
Williams aliwahi kukutana na Mbappe akiwa na Wales mwaka 2017.
Alisema:"Mbappe ni wa moja kwa moja zaidi kuliko Messi. Anatumia kasi yake na anakulazimisha kucheza kwa mwendo wake."
Kwa mujibu wa Williams, beki anapaswa kubaki makini muda wote kwa sababu Mbappe anaweza kubadilisha mchezo kwa sekunde chache tu.
Aidha, Ufaransa ina nyota wengine wengi kama Michael Olise, Ousmane Dembele na Desire Doue, hivyo huwezi kumlenga Mbappe peke yake.
Erling Haaland: Kata huduma kabla haijamfikia
Kwa upande wa Haaland, Williams anaamini siri kubwa ni kuzuia pasi zinazomfikia.
"Haaland ni tofauti kabisa. Mara nyingi anakuumiza bila hata kuwa na mpira miguuni."
Alieleza kuwa: Usipe nafasi nyuma ya mabeki, zuia pasi za kupenyeza na punguza nafasi kati ya safu ya kiungo na ulinzi.
Haaland ana mabao 59 katika mechi 52 za kimataifa na anajulikana kwa kutumia nafasi chache sana kupata mabao.
Harry Kane: Usimpe nafasi ya kupiga shuti
Williams anasema nguvu kubwa ya Kane ni uwezo wake wa kumalizia nafasi.
"Upigaji wake wa mashuti unaweza kuwa bora zaidi kuliko wote hawa."
Tofauti na zamani, Kane wa sasa hushuka sana katikati ya uwanja kusaidia kujenga mashambulizi.
Hii huwapa nafasi wachezaji kama Jude Bellingham, Noni Madueke na Anthony Gordon kukimbilia nafasi zilizoachwa nyuma ya mabeki.
Williams anasema mabeki wanapaswa kuwasiliana vizuri na viungo ili kuhakikisha Kane hafanyi uamuzi kwa uhuru.
Nani ni hatari zaidi?
Kwa mujibu wa Williams:Messi ni mchezaji mgumu zaidi kusoma na kutabiri. Wakati Mbappe ni mchezaji mwenye kasi na nguvu za moja kwa moja.
Upande wa Haaland ni mfungaji hatari zaidi ndani ya eneo la penalti, huku Kane ni mshambuliaji mwenye upigaji bora wa mashuti na uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi kwa wenzake.
Kombe la Dunia la 2026 linaonekana kuwa jukwaa la washambuliaji wakubwa, na ikiwa wataendelea na kiwango hiki, mashabiki wanaweza kushuhudia mojawapo ya mashindano yenye mabao mengi na burudani kubwa zaidi katika historia ya soka.