Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bruno awafunika nyota Arsenal

Muktasari:

  • Bruno ameshinda tuzo hiyo baada ya kuwa na msimu bora akiwa nahodha wa Manchester United akiweka rekodi ya kutoa pasi za mabao (asisti) 20 katika msimu mmoja wa ligi.

LONDON, ENGLAND: KIUNGO wa Manchester United, Bruno Fernandes, amewabwaga nyota watatu wa Arsenal na kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa msimu wa Ligi Kuu England 2025-2026.

Bruno ameshinda tuzo hiyo baada ya kuwa na msimu bora akiwa nahodha wa Manchester United akiweka rekodi ya kutoa pasi za mabao (asisti) 20 katika msimu mmoja wa ligi.

Rekodi hiyo inamfanya Bruno kuwa sawa na gwiji wa zamani wa Arsenal, Thierry Henry aliyefanya hivyo katika msimu wa 2002-03, pamoja na kiungo wa zamani wa Manchester City, Kevin De Bruyne (msimu wa 2019-20)

Bruno bado ana nafasi moja ya kuvunja rekodi hiyo katika mchezo wa mwisho leo wakati Manchester United watakapocheza dhidi ya Brighton & Hove Albion.

Katika kuwania tuzo hiyo, Bruno aliwashinda nyota watatu wa Arsenal, Gabriel Magalhaes, Declan Rice na David Raya waliokuwa nguzo muhimu ya timu hiyo kutwaa ubingwa wake wa kwanza wa Ligi Kuu England baada ya miaka 22.

Wengine waliowania tuzo hiyo ni pamoja na nyota wa Manchester City, Erling Haaland na Antoine Semenyo, wengine ni nyota wa Nottingham Forest, Morgan Gibbs-White na yule wa Brentford, Igor Thiago.

Bruno mwenye miaka 31, amecheza mechi 34 za ligi msimu huu, akifunga mabao manane na kutoa asisti 20. Huku akifikia rekodi yake ya mabao ya msimu uliopita, akiongeza mara mbili idadi ya asisti alizotoa msimu huu.

Kiungo huyo wa Ureno msimu huu amefikisha idadi ya mechi 229 alizocheza Ligi Kuu England tangu atue hapo Januari 2020, huku akifunga mabao 70 na kutoa asisti 71.

Nahodha huyo ameiongoza Manchester United kumaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi, mafanikio ambayo wengi hawakuyatarajia baada ya kuondoka kwa kocha Ruben Amorim, Januari 2026.

Baada ya hapo, Michael Carrick alichukua nafasi ya muda na kufanikiwa kuiongoza United hadi kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Manchester United, Ijumaa ilitangazwa kuwa kocha Carrick amesaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kuwa kocha mkuu wa kudumu ndani ya Old Trafford, baada ya kufanya vizuri katika kipindi chake cha pili cha ukocha wa muda.

Tangu Carrick achukue timu hiyo, Bruno amefunga mabao matatu na kutoa asisti 11, baada ya kurudishwa katika nafasi yake anayopendelea ya namba 10 nyuma ya mshambuliaji mmoja katika mfumo wa 4-2-3-1.