Kaseja awatuliza mastaa Kagera Sugar

Muktasari:
- Kagera ipo nafasi ya 15 katika msimamo baada ya kukusanya pointi 22 katika mechi 27 ilizocheza na endapo ikishinda zote itafikisha pointi 31, huku ikiziombea mabaya Pamba Jiji na Tanzania Prisons kuangusha pointi zinazochuana kuepuka kuungana na KenGold iliyoshuka mapema daraja.
KOCHA Mkuu wa Kagera Sugar, Juma Kaseja anajua wana mechi ngumu za kumaliza msimu salama, lakini amesema amefanya kikao na wachezaji wa timu hiyo kuwatuliza na kuwataka wacheze kiufundi na kuweka pembeni presha ya kushuka daraja ili wajiokoe.
Kagera ipo nafasi ya 15 katika msimamo baada ya kukusanya pointi 22 katika mechi 27 ilizocheza na endapo ikishinda zote itafikisha pointi 31, huku ikiziombea mabaya Pamba Jiji na Tanzania Prisons kuangusha pointi zinazochuana kuepuka kuungana na KenGold iliyoshuka mapema daraja.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kaseja alisema hakuna mechi rahisi kwa zilizobaki, kwani kila moja ni fainali na ili kuhakikisha hawadondoshi pointi amekaa na wachezaji wake akiwataka wacheze kimbinu na akili.
"Ligi inaelekea mwisho tuna mechi tatu muhimu tukianza na Mashujaa kwenye uwanja wetu wa nyumbani tunatakiwa kucheza kwa akili zaidi na sio presha kila kitu kinawezekana nafasi bado ipo kama tutapambana," alisema Kaseja na kuongeza;
"Kila mchezaji anatambua umuhimu wa mechi zilizobaki ukiangalia sisi ndio tuna presha kubwa ya matokeo hivyo kutokana na hilo nimekaa na wachezaji na kuwatoa hofu juu la hilo ili tuweze kucheza kwa kujiamini na kusaka pointi tatu muhimu."
Kaseja alisema kazi aliyonayo ni kubwa mbali na kuandaa timu kiufundi pia anatakiwa kuwajenga wachezaji wake kisaikolojia kwa kuwaambia bado wana nafasi waangalie matokeo zaidi ya kukimbizana na tatizo.
Akizungumzia mechi inayofuata dhidi ya Mashujaa alisema maandalizi yanaendelea vizuri na wachezaji wapo katika hali nzuri ya ushindani dakika 90 ndio zitatoa maamuzi na hatma yao.
"Hautakuwa mchezo rahisi Mashujaa pia wanahitaji pointi tatu lakini tunahitaji kutumia vizuri uwanja wetu wa nyumbani na kupambana kuondoka nafasi tuliyopo licha ya kwamba ushindi tutakaoupata hautatupeleka popote zaidi ya kuongeza namba."