Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SIO ZENGWE: Mkataba wa Diadora, Simba ni funguo nyingine

ZENGWE Pict

Muktasari:

  • Nimetanguliza hilo kwa kuwa wale watetezi wa uzawa wanaweza kusoma safu hii kwa jicho la kutaka kukosoa badala ya kuelewa kile ninachomaanisha.

SI kwamba hatutaki kampuni za ndani kupata mikataba minono ya udhamini, bali tunataka zijifunze kwa kampuni kubwa zilizoendelea na zenye uzoefu wa muda mrefu katika biashara.

Nimetanguliza hilo kwa kuwa wale watetezi wa uzawa wanaweza kusoma safu hii kwa jicho la kutaka kukosoa badala ya kuelewa kile ninachomaanisha.

Ni kuhusu mkataba mpya wa klabu ya Simba na Jayrutty ambao umewapeleka hadi Italia ambako wanakutana na kampuni ya Diadora, kampuni kubwa ya vifaa vya michezo iliyoanzia umaarufu wake katika mchezo wa tenisi.

Jayrutty na Simba zilisaini mkataba wa Sh38 bilioni wiki mbili zilizopita, mkataba ambao umehusisha manufaa mengi kwa mabingwa hao wa soka wa zamani wa Tanzania Bara, kubwa likiwa ni ujenzi wa uwanja wa michezo utakaokuwa na uwezo wa kuchukua watu kati ya 10,000 na 12,000.

ZEN 01

Kabla ya taarifa za mkataba huo kuingia vichwani vizuri, Jayrutty ikatangaza tena jambo kubwa.

Kwa mujibu wa taarifa za wiki hii, kampuni ya Jayrutty imeingia mkataba na Diadora kwa ajili ya kutengeneza vifaa vya michezo kwa klabu ya Simba na hivyo kuifanya klabu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi kuwa na uhusiano na moja ya chapa kubwa duniani.

Kwa kuingia mkataba huo, Simba sasa ina uhakika wa kupata vifaa vyenye ubora kutoka moja kwa moja kwa watengenezaji hao, tofauti na mikataba ya hivi karibuni ya klabu za Tanzania ambazo zimekuwa zikiingia mkataba na kampuni ambazo baadaye huenda kuchapisha jezi sehemu nyingine.

Mkataba huo unaifanya Simba kuwa klabu ya kwanza katika miaka ya hivi karibuni kuingia mkataba na moja ya chapa kubwa duniani ambazo hujali sana ubora wa vifaa na huangalia vitu vingi muhimu kwenye historia na utamaduni wa klabu kabla ya kutengeneza jezi.

ZEN 02

Mbali na kujali ubora, kampuni hizi kubwa kimataifa huheshimu mikataba na wateja wake, tofauti na mizozo tuliyoishuhudia katika siku za hivi karibuni baina ya klabu na wadhamini wa mavazi ya michezo.

Kutoingia mkataba moja kwa moja na kampuni hizo kubwa za utengenezaji vifaa vya michezo huondoa madalali katikati ambao kwa kawaida huongeza gharama za udhamini bila ya kuwepo umuhimu wa uwepo wao.

Labda tatizo ni kwamba ilikuwaje klabu ikashindwa kuona uwezekano wa kupata mkataba wa udhamini moja kwa moja kutoka Diadora na badala yake ikapitia njia ya Jayrutty?

ZEN 03

Nadhani hapo ndipo idara za masoko za klabu zetu zinapokosa maarifa ya kujenga chapa zao na kuwaasilisha maandiko kwa kampuni kubwa kwa ajili ya kusaka udhamini badala ya mtindo wa sasa wa kutangaza zabuni ambao huruhusu watu waliochungulia fursa kuwasilisha maombi mazuri ya zabuni kwa kujua ukubwa wa klabu sokoni na uwezekano wa kupata mikataba minono.

Hivi sasa kuna mjadala unaendelea wa kampuni moja kudhamini zaidi ya klabu mbili kwenye Ligi Kuu, lakini hauangalii suala hilo muhimu la kutokuwepo na idara imara na zenye maono za masoko.

ZEN 04

Ni kama vile kampuni zinazodhamini zaidi ya klabu moja hufanya hivyo kama msaada na si udhamini kwa kuwa zinajua wengi kwenye klabu wanadhani si kitu rahisi kupata udhamini mkubwa zaidi ya fedha wanazowekewa mezani.

Katikam dunia ya sasa ambayo mpira wa miguu unazidi kuwa biashara kubwa, idara ya masoko ni muhimu sana katika kuvutia kampuni kuwekeza kwenye klabu, la sivyo tutaendelea kupata udhamini wa huruma kama unaofanywa na kampuni nyingi kwa sasa Ligi Kuu.

Bravo Simba kwa japo kuthubutu kuona kampuni ya Jayrutty yenye maono kama hayo ya mbali.

Ukubwa ambao Simba inajinasibu nao, huambatana na mikataba kama hiyo ya uhusiano na wakubwa wengine duniani.

ZEN 05

Badala ya klabu nyingine kutafuta udhaifu au kasoro za mkataba huo wa Diadora, ni muhimu wakauchukulia kama ni funguo kwa kuzifikia kampuni nyingine kubwa, jambo ambalo litaweza hata kuzizindua kampuni za wazawa kuona zinatakiwa zijirekebishe wapi.