Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fahamu BMI kikotozi cha kutathimini uzito

Muktasari:

  • Jumamosi, soka la Afrika lilinoga baada ya Mamelodi Sundowns kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika. Sundowns ilitwaa ubingwa huo baada ya kuifunga AS FAR ya Morocco kwa jumla ya mabao 2-1 katika michezo miwili ya fainali, ukiwamo mchezo wa marudiano uliochezwa nchini Morocco.

WAKATI ligi za soka katika nchi mbalimbali duniani zikifikia tamati mwishoni mwa wiki iliyopita, Ligi Kuu Bara iliendelea juzi kwa mechi mbili kabla ya kusimama kupisha kalenda ya Fifa kwa nchi wanachama. Wakati Yanga ikiendelea kuongoza msimamo Bara bado kinyang’anyiro cha ubingwa wa Ligi Kuu kinachoendelea kushika kasi, huku zikiwa zimesalia mechi nne kumpata bingwa wa msimu huu.

Jumamosi, soka la Afrika lilinoga baada ya Mamelodi Sundowns kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika. Sundowns ilitwaa ubingwa huo baada ya kuifunga AS FAR ya Morocco kwa jumla ya mabao 2-1 katika michezo miwili ya fainali, ukiwamo mchezo wa marudiano uliochezwa nchini Morocco.

Ikumbukwe kuwa Sundowns ilishinda mchezo wa kwanza nyumbani kwa mabao 1-0 mnamo Mei 17 kabla ya kulazimisha sare ya 1-1 katika mchezo wa marudiano.

Sasa macho ya mashabiki wa soka yanaelekezwa kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Arsenal na PSG inayotarajiwa kuchezwa  Jumamosi. Baada ya hapo, dunia ya soka itahamia kwenye Kombe la Dunia 2026 linalotarajiwa kuanza Juni 11, 2026 kwa ushirikiano wa nchi tatu ambazo ni Marekani, Canada na Mexico. Mashabiki wa soka ni miongoni mwa makundi yanayopata burudani mfululizo, ikiwamo kutazama kandanda moja kwa moja viwanjani au kupitia luninga na simu janja. Ndiyo maana ni jambo la kawaida kuwaona baadhi ya mashabiki wakiwa na uzito uliokithiri au unene, jambo ambalo mara nyingi huchangiwa na kukosa muda wa kufanya mazoezi.

Vilevile, hata baadhi ya wachezaji waliomaliza ligi katika nchi ambazo hazishiriki Kombe la Dunia huingia katika mapumziko ya kiangazi, hali inayoweza kuwafanya pia kuwa katika kundi la wanaojisitiri kwenye burudani.

Wachezaji walio kwenye mapumziko pamoja na mashabiki wanaopenda burudani bila kufanya mazoezi huku wakila vyakula kiholela wako katika hatari ya kuongezeka uzito au kupata unene. Kwa mashabiki wanaopenda burudani, hususan waliofikisha umri wa miaka 35 na kuendelea, ni muhimu kula mlo wa wastani.

Kadhalika, mchezaji anayekula vyakula kiholela huku akiwa kwenye mapumziko marefu bila mazoezi anaweza kuongezeka uzito. Leo, Jicho la kitabibu linaangazia njia rahisi ya kutathmini uzito wa mwili ijulikanayo kama BMI, kwa kirefu Body Mass Index au kwa Kiswahili “Kielelezo cha Uzito wa Mwili”. Hii ni njia rahisi inayowezesha kujua mwenendo wa uzito wa mwili. Mchezaji au shabiki anaweza kuitumia kutathmini uzito wake na kuchukua hatua mapema.

BMI hufafanuliwa kama kipimo kisicho cha moja kwa moja cha unene wa mwili, kinachohesabiwa kwa kugawanya uzito wa mtu katika kilogramu dhidi ya urefu wake katika mita za mraba. Kwa matokeo yake, BMI ya 30 au zaidi huashiria unene, huku BMI ya 25 au zaidi ikionesha uzito kupita kiasi na hatari ya kupata unene uliokithiri.


BMI IKO HIVI

Katika hali rahisi, maumbile ya mwanadamu kwa kuzingatia uzito yanaweza kuanishwa katika makundi ya uzito wa chini, uzito wa kawaida, uzito uliozidi, unene na unene uliokithiri. Uhamasishaji wa kufanya mazoezi mepesi unatokana na kutambua kuwa tatizo la unene si zuri kiafya, kwani huweka mwili katika hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza (Non-Communicable Diseases).

Kufanya mazoezi na kuushughulisha mwili mara kwa mara ni moja ya njia rahisi za kuufanya mwili kuwa imara kiafya. Mazoezi hutusaidia kuwa na afya bora na kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza, yakiwamo magonjwa ya moyo, kisukari na unene uliokithiri. Watu wengi wazima wanaofanya mazoezi huwa na lengo la kupambana na uzito mkubwa au unene uliokithiri, ambao ni sehemu ya changamoto za kiafya zinazohusishwa na utapiamlo.

Ni kawaida kwa watu wengi kufanya mazoezi bila kufahamu wana uzito wa kiwango gani au unene wao uko katika kundi lipi. Ni muhimu kwa kila mtu, hata asiye mzoefu wa mazoezi, kufuatilia mwenendo wa uzito wa mwili ili pale unapozidi kiwango cha kawaida hatua za mapema ziweze kuchukuliwa.

Kitaalamu, zipo njia mbalimbali zinazotumika kubaini unene uliokithiri au kutambua mtawanyiko wa mafuta yaliyorundikana mwilini.

Miongoni mwa njia hizo ni upimaji wa mzunguko wa tumbo ukilinganishwa na urefu wa mwili, unaojulikana kama waist circumference ratio. Njia nyingine ni waist-hip ratio, yaani uwiano wa mzunguko wa tumbo na mzunguko wa nyonga. Njia ya tatu ni Body Mass Index (BMI), ambayo ni uwiano wa uzito dhidi ya urefu wa mwili.

Njia ya BMI ndiyo inayotumika zaidi kutathmini uzito wa mwili kwa watu wazima, na leo nitaelekeza zaidi mjadala kwenye njia hii kwa kuwa ndiyo inayotoa taswira ya kiwango cha unene mwilini.

Kwa kawaida, BMI huhesabiwa kwa kutumia fomula ya kugawanya uzito katika kilogramu kwa urefu katika mita za mraba. Kwa mfano, mtu mwenye uzito wa kilo 65 na urefu wa mita 1.5, BMI yake hupatikana kwa kugawa uzito huo kwa urefu mara urefu. Matokeo yanayopatikana ndiyo hujulikana kama BMI na hutusaidia kubaini kama mtu ana uzito mdogo, wa kawaida au unene uliokithiri.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), BMI hutumika kuanisha uzito wa mtu katika makundi matano. Jibu linalopatikana baada ya kukokotoa ndilo hutoa ainisho la uzito.

Kwa watu wazima, BMI ya 18.5 hadi 24.9 huchukuliwa kuwa uzito salama kiafya; 25.0 hadi 29.9 ni uzito mkubwa; 30.0 hadi 39.9 huashiria unene; huku 40.0 kuendelea ni unene uliokithiri. Endapo BMI itakuwa chini ya 18.5, maana yake ni kuwa mtu huyo ana uzito mdogo kupita kiasi.

Kupitia BMI, tunaweza kutofautisha uzito mkubwa, unene na unene uliokithiri. Hivyo, wataalamu wa afya hutumia njia hii kutathmini hatari za kiafya zinazoweza kujitokeza kulingana na matokeo ya BMI. Njia hii ya BMI ni rahisi na haina gharama. Pia husaidia kubaini mrundikano wa mafuta mwilini pamoja na uzito uliokithiri kwa urahisi.

Simu janja nyingi zina mfumo wenye kikokotozi cha BMI, ambapo mtumiaji hujaza uzito wake kwa kilogramu pamoja na urefu wake kwa mita. Ingawa BMI haipimi moja kwa moja kiwango cha mafuta mwilini, bado ni kiashiria muhimu kinachosaidia kubaini hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza. Ni vyema kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mepesi na kula vyakula visivyonenepesha mapema kabla umri haujasonga mbele.


CHUKUA HII

Ukokotozi wa BMI hukupa mwanga wa kuchukua hatua mapema. Dhibiti uzito wako katika maisha ya kila siku ili usiharibu uzito unaofaa kiafya, kwani uzito uliokithiri huwa vigumu kuupunguza.

Uzito uliokithiri ni moja ya changamoto zinazoweza kushusha kiwango cha mchezaji wa soka, hivyo ni muhimu kujiongeza kwa kutumia BMI kama njia ya kujitathmini na kujihami mapema.