Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dakika 270 za mnyukano Ligi Kuu

Muktasari:

  • Wakati macho ya wengi yakiwa kwenye mnyukano wa watani wa jadi, Yanga na Simba kule juu kuwania ubingwa, ukweli ni kwamba vita kali na ya kusisimua zaidi inapiganwa chini, ambapo timu nane zinapumulia mashine zikihofia kuungana na KMC ambayo tayari imeshakata tiketi ya kushuka daraja kwenda Ligi ya Championship, wakati huohuo Geita Gold na Kagera Sugar zikipanda daraja.

MSIMU wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2025-2026 unaelekea ukingoni huku zikibaki raundi tatu pekee, sawa na dakika 270 za uamuzi mgumu kwa kila timu, kabla ya pazia kufungwa rasmi.

Wakati macho ya wengi yakiwa kwenye mnyukano wa watani wa jadi, Yanga na Simba kule juu kuwania ubingwa, ukweli ni kwamba vita kali na ya kusisimua zaidi inapiganwa chini, ambapo timu nane zinapumulia mashine zikihofia kuungana na KMC ambayo tayari imeshakata tiketi ya kushuka daraja kwenda Ligi ya Championship, wakati huohuo Geita Gold na Kagera Sugar zikipanda daraja.

Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 66 baada ya michezo 27, ikiwa imepoteza mchezo mmoja pekee msimu mzima.

Vinara hao chini ya ulinzi thabiti wa kipa Djigui Diarra mwenye clean sheets 14, wanahitaji kushinda mechi zote tatu zilizobaki ili kutetea taji lake kwa kulibeba mara ya tano mfululizo. Ratiba yao inaonesha watacheza dhidi ya Azam (nyumbani), TRA United (nyumbani) na kuhitimisha dhidi ya JKT Tanzania (ugenini).

Kwa upande mwingine, Simba inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 64, tofauti ya pointi mbili tu nyuma ya Yanga. Simba, ikiwa na silaha kama Clatous Chama na Elie Mpanzu, inasubiri kwa hamu kuteleza kwa Yanga huku yenyewe ikijiandaa kuvaana na Mtibwa Sugar (ugenini), Singida Black Stars (nyumbani) na KMC (nyumbani) ili kubeba ubingwa wa ligi ilioukosa kwa misimu minne.

Hesabu hapa ni rahisi, Yanga ikishinda mechi zake zote, Simba hata ifanye nini, ubingwa unabaki mitaa ya Twiga na Jangwani.

Katika kundi la nne bora, Singida Black Stars imejichimbia katika nafasi ya nne ikiwa na pointi 47.

Ili kuwa na uhakika wa moja kwa moja kubaki hapo na kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi kimataifa, inahitaji kukusanya angalau pointi nne katika mechi tatu zilizobaki, kwa lugha nyepesi ishinde moja na sare.

Hata hivyo, kutokana na idadi yao nzuri ya mabao ya kufunga (42) ukilinganisha na walio chini yao, hata pointi tatu zinaweza kuwatosha kuwa salama.

Wanamtegemea sana mshambuliaji wao hatari, Mossi Nduwumwe, ambaye ameshapachika mabao 12 msimu huu ikiwemo hat trick moja ikiwa ya kwanza msimu huu katika ligi hiyo ambapo sasa zipo mbili, nyingine kutoka kwa Mathew Tegisi Momanyi wa Pamba Jiji.


NAFASI, FEDHA

Kutokana na udhamini uliopo, kila timu ina kiasi chake cha fedha inakipata kulingana na nafasi iliyomaliza. Udhamini huu unajumuisha ule wa NBC ambao ni wadhamini wakuu wa ligi na Azam Media ambao wanasimamia haki za matangazo wakionesha mechi zote, kumbuka zawadi hizo zilitangazwa tangu msimu wa 2021-2022.

Bingwa (Sh600 milioni), nafasi ya pili (Sh300 milioni), nafasi ya tatu (Sh255 milioni), nafasi nne (Sh200 milioni), nafasi ya tano (Sh65 milioni), nafasi ya sita (Sh60 milioni), nafasi ya saba (Sh55 milioni), nafasi ya nane (Sh50 milioni), nafasi ya tisa (Sh45 milioni), nafasi ya kumi (Sh40 milioni), nafasi ya 11 (Sh35 milioni), nafasi ya 12 (Sh30 milioni), nafasi ya 13 (Sh25 milioni), nafasi ya 14 (Sh20 milioni) nafasi ya 15 (Sh10 milioni), nafasi ya 16 (Sh10 milioni). Timu yenye nidhamu Sh20 milioni.


TIMU NANE, HATARI MOJA

Huku KMC ikiwa tayari imeshuka daraja baada ya msimu mbaya uliowaacha na pointi tisa pekee katika michezo 27, nafasi mbili za kushuka moja kwa moja na mbili za mtoano (play-offs) bado zimekaa kimtego.

Kuna timu nane ambazo hesabu zinaiweka moja katika hatari ya kuungana na KMC endapo itashindwa kufurukuta katika hizi dakika 270 zilizobaki.

Ili kuwa salama kabisa, timu hizi zinapaswa kulenga kuvuka alama 36 ambazo kwa sasa zinashikiliwa na Pamba Jiji katika nafasi ya saba.

Kumbuka hata Mbeya City yenye pointi 25 katika nafasi ya 15, ikichanga vizuri karata zake kisha timu za juu zikateleza, inaweza kubaki salama kwani inaweza kufisha pointi 34 ambazo timu saba za juu yake hazijafikia zaidi ya Dodoma Jiji iliyo karibu zaidi ikikusanya pointi 33 na Coastal Union 32.

Harakati hizo zote tutaanza kuzishuhudia Jumatano hii Juni 24, 2026, kisha Juni 27, 2026 na hitimisho lake Juni 30, 2026 ambapo tarehe hizo ndipo zinachezwa raundi tatu zilizobaki.


DODOMA JIJI (Pointi 33, nafasi ya 8)

Ipo katika nafasi nzuri kidogo kuliko wengine, lakini haipo salama kwa asilimia mia moja. Inahitaji ushindi mmoja tu kufika alama 36 za usalama.

Mechi zilizobaki: vs JKT Tanzania (nyumbani), vs Mbeya City (nyumbani) na vs Azam (ugenini).

Changamoto kubwa kwao ni mechi ya mwisho dhidi ya Azam ambao wanapigania heshima ya nafasi ya tatu kwani mzunguko wa kwanza matokeo yalikuwa Dodoma 0-3 Azam, huku dhidi ya JKT Tanzania ambayo haina presha yoyote ya ubingwa wala kushuka daraja, zilipokutana raundi ya kwanza matokeo yalikuwa JKT Tanzania 0-1 Dodoma Jiji wakati dhidi ya Mbeya City iliyo kwenye hatari, mwanzo matokeo yalikuwa 1-1.


COASTAL UNION (Pointi 32, nafasi ya 9)

Wagosi wa Kaya wanahitaji pointi nne ili kufikia alama 36. Mshambuliaji wao Maabad Maulid mwenye mabao saba atakuwa tegemeo kubwa nyakati hizi.

Mechi zilizobaki: vs TRA United (ugenini), vs Azam (nyumbani) na vs Pamba Jiji (nyumbani).

Mechi dhidi ya Pamba Jiji inaweza kuwa ya kuamua nani anakaa sehemu salama zaidi.

Coastal ina bahati inamaliza mechi tatu dhidi ya timu zote ambazo zipo salama, huku mechi mbili za nyumbani zikionekana zinakwenda kuwabeba kwani ina rekodi nzuri hapo dhidi ya wapinzani wake ikishinda mechi tano, sare tano na kupoteza tatu kati ya 13 ilizocheza dimba la nyumbani.


FOUNTAIN GATE (Pointi 29, nafasi ya 10)

Hapa ndipo presha inapoanza kupanda. Fountain Gate inahitaji kushinda mechi mbili na kupata sare moja ili kufika alama pointi 36.

Mechi zilizobaki: vs Mashujaa (nyumbani), vs Namungo (ugenini) na vs Singida Black Stars (nyumbani).

Hizi ni mechi ngumu kwani Mashujaa na Namungo nazo zinapigania uhai wao.


MASHUJAA (Pointi 27, nafasi ya 11)

Mashujaa ipo katika hali tete. Imekusanya pointi 27 na inahitaji miujiza katika dakika hizi 270.

Mechi zilizobaki: vs Fountain Gate (ugenini), vs KMC (nyumbani) na vs Tanzania Prisons (nyumbani).

Mechi dhidi ya KMC iliyoshuka daraja ni inaweza kushinda kirahisi, lakini Prisons na Fountain Gate watakuwa vikwazo vikubwa kwa sababu nao wana kitu wanakitafuta.


NAMUNGO (Pointi 27, nafasi ya 12)

Kinara wa mabao kikosini hapa, Fabrice Ngoy (mabao 8), anapaswa kutumia uzoefu wake kufunga mabao ya ushindi ili kubaki ligi kuu.

Mechi zilizobaki: vs KMC (ugenini), vs Fountain Gate (nyumbani) na vs Mtibwa Sugar (nyumbani).

Ratiba yao inaonekana kuwa na unafuu kidogo kwani mechi mbili za mwisho itamalizia nyumbani baada ya kutoka ugenini kuikanili KMC, lakini mechi dhidi ya Mtibwa Sugar itakuwa ya kufa au kupona.


MTIBWA SUGAR (Pointi 27, nafasi ya 13 - eneo la mtoano)

Mtibwa ikiwa imerejea Ligi Kuu msimu huu, sasa inajikuta pabaya katika hatari ya kurudi ilipotoka Ligi ya Championship. Nafasi ya 13 iliyopo sasa, inaiingiza kwenye mtoano wa kuepuka kushuka daraja, hivyo inahitaji kupambana kutoka eneo hilo ili kuwa salama zaidi.

Mechi zilizobaki: vs Simba (nyumbani), vs Tanzania Prisons (ugenini) na vs Namungo (ugenini).

Kuanza na Simba ni mtihani mzito, huku Prisons na Namungo wakiwa ni wapinzani wa moja kwa moja katika vita hii kwani zote hazipo salama.


TANZANIA PRISONS (Pointi 26, nafasi ya 14 - eneo la mtoano)

Maafande wa Prisons wanahitaji kushinda mechi zao zote ili kuwa na uhakika wa kubaki. George Mpole mwenye mabao saba ndiye tumaini lao la ufungaji.

Mechi zilizobaki: vs Singida Black Stars (nyumbani), vs Mtibwa Sugar (nyumbani) na vs Mashujaa (ugenini).

Mechi mbili za mwisho dhidi ya Mtibwa na Mashujaa ni 'fainali' halisi za nani anabaki na nani anaondoka.


MBEYA CITY (Pointi 25, nafasi ya 15 - eneo la kushuka daraja moja kwa moja)

Mbeya City ipo katika hali mbaya zaidi. Inashika nafasi ya 15, ambayo inamaanisha kushuka daraja moja kwa moja endapo itasalia hapo. Inahitaji ushindi katika mechi zote na kuziombea njaa zilizo juu yake ili kuepuka kurudi Ligi ya Champioship ilipopanda sambamba na Mtibwa Sugar.

Mechi zilizobaki: vs Pamba Jiji (ugenini), vs Dodoma Jiji (ugenini) na vs TRA United (nyumbani).

Mechi dhidi ya Dodoma Jiji itakuwa ngumu sana kwani wote wanahitaji pointi kwa gharama yoyote ili kujiweka salama.