Prime
SIO ZENGWE: Siasa isiunganishe ligi za Bara, Zanzibar
Muktasari:
- Mpango huo uliwekwa bayana bungeni wiki iliyopita na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma wakati akijibu moja ya maswali ya wabunge kuhusu Muungano na michezo.
SERIKALI ina mpango wa kuunganisha ligi za soka za Tanzania Bara na Zanzibar ili kuwa na ligi moja itakayoweka tafsiri halisi ya Muungano wa pande hizo mbili ulioanza mwaka 1964.
Mpango huo uliwekwa bayana bungeni wiki iliyopita na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma wakati akijibu moja ya maswali ya wabunge kuhusu Muungano na michezo.
Kikatiba, michezo si suala la Muungano na kila pande ina wizara yake inayojishughulisha na michezo, na kuna baadhi ya michezo kama mpira wa miguu ambayo uwakilishi wa kimataifa hauhusishi Muungano, yaani wawakilishi wa Tanzania Bara n I tofauti na wa Visiwani.
Lakini michezo mingine, mwakilishi huwa mmoja tu na hupatikana baada ya kushindanisha timu kutoka kila upande wa Muungano.
Imewezekana katika mpira wa miguu wakati Zanzibar ilipopewa uanachama wa muda wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) wakati ikifanya jitihada za kupata uanachama wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa).
Hata hivyo, mpango huo wa kwenda Fifa ulikufa kutokana na shirikisho hilo la kimataifa kutambua utaifa wan chi ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa.
Hata hivyo, nchi nne zinazounda Dola la Umoja wa Kiingereza (UK), yaani England, Wales, Scotland na Ireland, zimepewa uanachama maalum wa Fifa kutokana na historia, yaani zilihusika katika kuutengeneza mpira wa miguu unaochezwa sasa duniani.
Kwa hiyo, Zanzibar haiwezi kupewa uanachama kwa hoja hiyo au hoja nyingine yoyote ikiwa ndani ya Muungano kwa kuwa Fifa inaitambua Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ndiyo nchi yenye sifa zote zinazotakiwa na Umoja wa Mataifa.
Hoja ya kuunganisha ligi si mpya. Ilishakuwepo miaka ya themanini wakati kulipokuwa na ligi moja. Lakini matatizo ya kifedha na maendeleo tofauti ya soka kwa pande zote mbili yalisababisha ligi hiyo kufutwa na baadaye kila upande kutakiwa kutafuta wawakilishi wake ili washindane kupata wawakilishi wan chi kwenye mashindano ya kimataifa.
Kuna timu zilikuwa zinapata vipigo hadi vya mabao 9-0 huku baadhi ya timu zikitakiwa kusafiri hadi Arusha au Mwanza na hivyo kujikuta katika wakati mgumu kiuchumi.
Hata wakati kulipoanzishwa Ligi ya Muungano iliyoshirikisha wawakilishi wa Zanzibar na Bara, bado kuliibuka changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni ya udhamini wa kampuni za bidha za pombe.
Zanzibar hairuhusu matangazo ya bidhaa za vilevi na wakati huo Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ilikuwa ndio mdhamini wa Ligi ya Muungano. Kwa hiyo, timu za Zanzibar hazikukubali kudhaminiwa na TBL kwa kuwa udhamini ulimaanisha zivae jezi zenye chapa ya Safari Lager. Hata viwanjani, matangazo ya Safari Lager yalitakiwa yawepo.
Kwa hiyo, timu za Zanzibar zikalazimika kucheza bila ya kunufaika na fedha za TBL na bila kuvaa au kupachika matangazo ya bia hiyo uwanjani.
Udhamini haukuwa na maana tena kwa kuwa mdhamini wa jumla hakuwa ananufaika kikamilifu na udhamini huo.
Haya mazingira, yaani udhamini na gharama za ushiriki ikizingatiwa kuwa ligi ziko kwenye muundo wa kucheza nyumbani na ugenini, na maana yake ni kwamba yanaweza kuwa kikwazo kikubwa kwa mpango huo wa serikali na iwapo utalazimishwa ligi inaweza kuendeshwa kwa matatizo makubwa.
Udhamini mkubwa wa sasa ni kampuni za ubashiri ambazo zimetapakaa dunia nzima, huku mamlaka za Zanzibar zikiwa haziruhusu biashara hiyo kutangazwa hadharani.
Hata kabla ya kuanza utekelezaji wa mpango huo, mchakato tu unaweza kuvutia kampuni nyingi za vileo na za ubashiri ambazo huweka fedha nyingi, lakini zitarudi nyuma pale zitakapoona msimamo wa mamlaka bado ni uleule.
Hata hivyo, Ligi ya Muungano inatakiwa iendelee kuwa ya kudumisha Muungano na si kutafuta uwakilishi kwa kuwa kwa sasa kila upande wa Muungano una nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa ya klabu, ingawa idadi ya wawakilishi hutegemea jinsi ligi za nchi wanachama wa CAF zinavyovuna pointi nyingi katika mashindano hayo. Ndio maana Bara ina nafasi nne na Zanzibar bado ni mbili.
Ili kupanua uwakilishi Afrika, kuna haja ya kuwekeza nguvu kwenye Ligi Kuu ya Zanzibar ili timu zake zifike hatua za juu za mashindano ya CAF na kufikia kiwangom cha kuongezewa idadi ya timu. Na juhudi hizo ni pamoja na kutengeneza mikakati ya kuvutia mashabiki zaidi viwanjani au unazi, kuvutia au kushawishi kampuni kuongeza udhamini na kuziwezesha klabu kuimarika kiuchumi na hivyo kuwa na nguvu katika spoko la wachezaji na ajira za makocha na hivyo kujenga timu imara.
Zanzibar ikiongeza idadi ya uwakilishi, Tanzania itakuwa na uwakilishi mkubwa zaidi badala ya kutaka kugombea hizo nafasi chache zilizopo.
Juhudi pia zinatakiwa zifanyike ili uanachama wa Zanzibar usiwe wa kuandikwa kwa penseli na hivyo kuwa rahisi kufutika. Juhudi hizo zitaimarika iwapo timu za Zanzibar itaongeza ushindani na kufikia hatua za juu za mashindano ya CAF.
Kwa hiyo, hatuna budi kupima ni kitu gani tunatyakiwa tukiwekee nguvu kwa sasa. Kuunganisha ligi za Zanzibar na Bara bila ya kulazimishwa na sheria na kanuni au kufanya jitihada za kuimarisha ligi za Zanzibar na nafasi yake CAF?
Ni muhimu kushughulikia michezo kwa utamaduni wake badala ya kuingiza siasa sehemu ambayo haihitajiki. Kuunganisha ligi za Bara na Visiwani ni siasa zaidi kuliko mahitaji ya kimpira.