Benfica: Mourinho haendi kokote
Muktasari:
- Kwa sasa, Madrid inatafuta kocha mpya, huku aliyepo Alvaro Arbeloa akitarajiwa kufutwa kazi mwisho wa msimu baada ya klabu kushindwa kuonyesha matokeo ya kuridhisha.
LISBON,URENO: MABOSI wa Benfica wameendelea kuwa na imani kubwa kuwa kocha wao Jose Mourinho atasalia katika kikosi chao msimu ujao licha ya taarifa zinazodai anaweza kutimkia Real Madrid.
Kwa sasa, Madrid inatafuta kocha mpya, huku aliyepo Alvaro Arbeloa akitarajiwa kufutwa kazi mwisho wa msimu baada ya klabu kushindwa kuonyesha matokeo ya kuridhisha.
Arbeloa alichukua nafasi ya Xabi Alonso Januari mwaka huu, lakini hadi sasa ameshindwa kuirejesha Madrid kwenye ubora wake, ikiwa tayari imetolewa katika Ligi ya Mabingwa Ulaya na ina nafasi ndogo ya kuipiku Barcelona katika mbio za ubingwa wa La Liga.
Majina kadhaa yamehusishwa na kibarua cha kuinoa Madrid, ikiwemo Jurgen Klopp na Didier Deschamps, lakini Mourinho anaonekana kuwa chaguo kuu kutokana na ukaribu wake na rais wa klabu hiyo Florentino Perez.
Kwa sasa, Mourinho mwenye umri wa miaka 63 anaifundisha Benfica aliyojiunga nayo Septemba mwaka jana, kwa mkataba wa misimu muwili hadi Juni 2027.
Hata hivyo, ripoti zinaeleza katika mkataba wake kuna kipengele cha kuuvunja kinachohitaji Madrid kulipa Euro 3 milioni ili kufanikisha suala hilo.
Hata hivyo, Benfica wanadaiwa kuwa na uhakika mkubwa kocha huyo ataendelea kubaki kwa msimu ujao na tayari wanaendelea kupanga mipango ya msimu wa 2026/27 chini ya na Mourinho.
Ripoti nyingine zimefichua ikiwa Mourinho mwenyewe atalazimisha kuondoka, Benfica itamgeukia kocha Fulham, Marco Silva, ili awe mbadala wake.
Silva mwenye umri wa miaka 48 anatarajiwa kumaliza mkataba wake na Fulham dirisha lijalo la majira ya kiangazi.