Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga yaichakaza Azam yakomaa kileleni

Muktasari:

  • Yanga imepata ushindi huo kupitia mabao ya Ibrahim Hamad 'Bacca' dakika ya 41, Laurindo Aurelio 'Depu' dakika ya 72 kwa mkwaju wa penalti na Pacome Zouzoua dakika ya 80.

Safari ya Yanga kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu imebakisha vituo viwili baada ya kuifunga Azam mabao 3-0 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Yanga imepata ushindi huo kupitia mabao ya Ibrahim Hamad 'Bacca' dakika ya 41, Laurindo Aurelio 'Depu' dakika ya 72 kwa mkwaju wa penalti na Pacome Zouzoua dakika ya 80.

Mechi hiyo iliyokuwa yenye msisimko wa aina yake ndani ya uwanja ikinogeshwa na ushindani baina ya timu hizo, ilikuwa ya 36 katika Dabi ya Dar es Salaam ndani ya Ligi Kuu Bara.

Bacca aliyefunga bao la kwanza katika mchezo huo, lilikuwa la 90 tangu timu hizo zianze kukutana kwenye Ligi Kuu Bara mwaka 2008 ambapo sasa jumla yamefungwa mabao 92.

Dar es Salaam Dabi ya kwanza baina ya timu hizo ilichezwa Oktoba 15, 2008, ambapo Yanga ilishinda 3-1 dhidi ya Azam. Siku hiyo Mkenya, Boniface Ambani alianza kufungua ukurasa wa mabao akifunga mawili dakika ya 11 na 15, kabla ya John Bocco kuifungia Azam bao moja dakika ya 31. Mapumziko matokeo yakawa Azam 1-2 Yanga.

Kipindi cha pili cha mchezo huo wa raundi ya nane ambao Azam ilikuwa mwenyeji, Castory Mumbala akaifungia Yanga bao la tatu dakika ya 88 na kuihakikishia timu hiyo ushindi.

Wakati Ambani akifunga bao la kwanza la Dar es Salaam Dabi, Bacca amefunga la 90 katika dabi hiyo likiwa la 47 upande wa Yanga ambayo sasa imefikisha mabao 49, huku Azam ikifunga mabao 43 tangu zianze kukutana kwenye ligi mwaka 2008.

Katika Dar es Salaam Dabi, sasa Yanga imeshinda mechi 15 dhidi ya 11 za Azam, sare zikiwa 10.

Timu hizo zimekutana baada ya siku tatu kupita ambapo ilikuwa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB iliyochezwa Juni 21, 2026 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na Azam kushinda mabao 3-2.

Pia msimu huu ni mara ya tano timu hizo zinakutana baada ya kuanza kwa matokeo ya 0-0 Ligi Kuu Bara, kisha Yanga kushinda kwa penalti 5-4 kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026, pia Yanga ikashinda tena 2-1 katika nusu fainali ya Kombe la Muungano, Azam ikajibu mapigo nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB kwa mabao 3-2 na sasa Yanga imeshinda 3-0.


MCHEZO ULIVYOKUWA

Yanga ambayo ilianzisha mechi hiyo iliyochezeshwa na Ahmed Arajiga, ilikuwa makini kuhakikisha inashinda ili kuweka hesabu zao sawa za kutetea ubingwa ambapo tofauti yao na Simba inayoshika nafasi ya pili ni pointi mbili. Yanga inazo 69, Simba pointi 67.

Mchezo ulianza kwa Azam kujaribu kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga. Dakika ya 35, umakini wa Twalibu Nuru ulimzuia Prince Dube kufunga baada ya beki huyo kuokoa shambulizi hatari na kuifanya Yanga kupata kona isiyozaa matunda.

Dakika mbili baadaye, Lusajo Mwaikenda alipiga krosi iliyomkuta Jean-Jacques Ngita akiwa uso kwa uso na kipa Djigui Diarra, lakini kipa huyo wa Yanga aliokoa kwa ustadi na kuokoa hatari hiyo.

Yanga ilivunja ukimya dakika ya 41 kupitia mpira wa adhabu uliochezwa kwa ujanja na Allan Okello kwenda kwa Prince Dube, ambaye aliunyanyua mpira ndani ya eneo la hatari. Ibrahim Bacca aliruka juu na kuunganisha kwa kichwa, akiiandikia Yanga bao la kwanza. Mapumziko Yanga 1-0 Azam.

Kipindi cha pili kilianza kwa Azam kufanya mabadiliko ambapo Kocha Florent Ibenge alimtoa Pascal Msindo na kumuingiza Nathaniel Chilambo.

Dakika ya 51, Chilambo alitoa krosi nzuri iliyounganishwa kwa kichwa na Feisal Salum, lakini Djigui Diarra aliendelea kuwa mwiba kwa Azam kwa kuokoa mpira huo na kuutoa nje kuwa kona.

Azam iliendelea kukosa nafasi zake, huku dakika ya 58 Jean-Jacques Ngita akishindwa tena kuifungia timu yake baada ya kupokea krosi ya Idd Nado akiwa katika nafasi nzuri, lakini shuti lake lilikwenda nje.

Dakika ya 60, Azam ilifanya mabadiliko mengine kwa kuwatoa Zidane Sereri na Jean-Jacques Ngita, nafasi zao zikichukuliwa na Abdul Suleiman pamoja na Jephte Kitambala.

Dakika ya 61, Feisal Salum 'Fei Toto' alionyeshwa kadi ya njano baada ya kumvuta Maxi Nzengeli karibu na eneo la hatari.

Yanga ilifanya mabadiliko dakika ya 64 kwa kumtoa Allan Okello na kumuingiza Mohamed Damaro.

Dakika ya 70, Twalibu Nuru alimwangusha Laurindo Depu ndani ya eneo la hatari na mwamuzi akaamuru penalti. Depu alisimama mwenyewe kupiga na kufanikiwa kuifungia Yanga bao la pili.

Dakika ya 71, Azam ilifanya mabadiliko mengine kwa kuwatoa Sadio Kanoute na Himid Mao, huku Yahya Zayd na James Akaminko wakichukua nafasi zao.

Laurindo Depu alitolewa nje dakika ya 77 na nafasi yake kuchukuliwa na Mudathir Yahya.

Yanga iliendelea kutawala mchezo na dakika ya 81 ilipata bao la tatu kupitia Pacome Zouzoua, ambaye aliunganisha kwa kichwa mpira uliotokea katika shambulizi kali na kuutikisa nyavu za Azam.

Dakika ya 86,  Yao Kouassi alitolewa nje na nafasi yake kuchukuliwa na Kibwana Shomari.

Mpaka mwamuzi anapuliza filimbi ya mwisho, Yanga ilikuwa mbele kwa mabao 3-0, ushindi ulioonyesha ubora wao katika mchezo huo huku Azam ikijutia nafasi kadhaa ilizoshindwa kuzitumia.