Utamu wa Ligi Kuu Bara sasa umebaki hapa

Muktasari:
- KenGold ilitangulia kushuka daraja ikiwa imecheza ligi hiyo kwa msimu mmoja tu, huku Kagera Sugar ikidumu miaka 20 tangu ilipopanda daraja 2005 na kuwa timu pekee iliyocheza ligi hiyo Kanda ya Ziwa kwa muda mrefu.
WAKATI Kagera Sugar ikiungana na KenGold kwenda kucheza Ligi ya Championship, kwa sasa Ligi Kuu Bara presha imebaki kwa timu tisa kujitetea kukwepa hatua ya mchujo (play- offs) ya kushuka daraja, huku makocha wakichora ramani namna ya kumaliza dakika 180.
KenGold ilitangulia kushuka daraja ikiwa imecheza ligi hiyo kwa msimu mmoja tu, huku Kagera Sugar ikidumu miaka 20 tangu ilipopanda daraja 2005 na kuwa timu pekee iliyocheza ligi hiyo Kanda ya Ziwa kwa muda mrefu.
Kagera Sugar yenye makazi wilayani Misenyi, mkoani Kagera, imeshuka daraja baada ya kuvuna pointi 22 ikiwa bado na michezo miwili kumaliza msimu, ambapo kwa sasa itacheza Championship msimu ujao, kwani hata ikishinda zote itafikisha pointi 28 ambazo zimeshapitwa na timu zilizopo juu yake.
Wakati timu hizo mbili zikienda na maji, kibarua kimebaki kwa timu tisa ambazo bado yoyote inaweza kuangukia kwenye hatua ya ‘play offs’ kutegemeana na matokeo ya michezo miwili iliyobaki kumaliza Ligi hiyo.
Kiujumla, timu inayoshika kuanzia nafasi ya sita hadi ya 14, hakuna yenye uhakika wa kuepuka kuingia katika mechi za play-offs’ ambazo zinakutanisha timu inayoshika nafasi ya 13 na 14 na anayepigwa anaenda kukutana na timu inayopigania kupanda daraja kutoka Ligi ya Championship.
yoyote
JKT Tanzania iliyopo katika nafasi ya sita ikiwa na pointi 35, iwapo itapoteza mechi mbili ilizobakiza, huku Pamba na Tanzania Prisons zenye pointi 30 katika nafasi ya 12 na 13 zikishinda mechi zake mbili zake zinaweza kuwashusha wanajeshi hao.
Dodoma Jiji iliyo katika nafasi ya saba kwa pointi 34, Mashujaa iliyopo nafasi ya nane kwa pointi 33, Coastal Union nafasi ya tisa kwa pointi 31 sawa na Namungo, huku Pamba Jiji na Tanzania Prisons zikiwa zimevuna pointi 30 kila moja na kufanya vita kuwa nzito.
Kocha Mkuu wa TZ Prisons, Aman Josiah alisema vita ni kubwa japo hadi sasa wana uhakika wa kucheza play off, lakini hesabu zao ni kuondoa presha hiyo ili kumaliza salama ligi.
“Hatutaki kusubiri hadi Agosti ishu ya play offs, tunataka tumalize mapema ligi tujiandae na msimu ujao, tunaenda kujipanga kwa mechi zijazo tukianza na Yanga nyumbani kisha Singida BS ugenini tukitafuta pointi sita,” alisema Josiah.
Kocha wa Pamba Jiji, Mathias Wandiba alisema mechi zilizobaki dhidi ya JKT Tanzania na KMC ni kufa au kupona akieleza kuwa wanaenda kusuka kikosi kwa muda huu ligi imesimama ili kuwa bora.
“Hatutaki hata sare kwenye mechi hizo na bahati nzuri tutakuwa nyumbani CCM Kirumba Mwanza kuhakikisha hatuachi mtu, pointi sita ni muhimu sana kwetu ili kubaki salama Ligi Kuu,” alisema Wandiba, huku kocha wa Coastal Union, Joseph Lazaro akisema dk180 zilizobaki ni za utulivu na ushindi.
“Hatuko salama sana japokuwa vita si kwetu tu, timu nyingi presha ni kubwa hivyo tunaenda kutumia mapumziko haya kusahihisha makosa hasa eneo la ushambuliaji ili kushinda michezo iliyobaki,” alisema Lazaro.