Simba yaichakaza Mtibwa, ila mhh...
Muktasari:
- Katika mchezo huo Simba ilikuwa ya kwanza kupata bao kwa mkwaju wa penalti iliyopigwa na Rushine de Reuck baada ya Shomari Kapombe kuangusha kwenye eneo la hatari.
Mashabiki wa Simba pamoja na kushuhudia timu yao ikitoa kipigo kizito mbele ya Mtibwa Sugar walitoka kwenye Uwanja wa Jamhuri wakiwa hawana furaha baada ya kupata taarifa ya kilichotokea Zanzibar.
Katika mchezo huo Simba ilikuwa ya kwanza kupata bao kwa mkwaju wa penalti iliyopigwa na Rushine de Reuck baada ya Shomari Kapombe kuangusha kwenye eneo la hatari.
Simba ilirudi kipindi cha pili kwa kasi zaidi na kupata bao la pili lililofungwa na Seleman Mwalimu aliyeingia akitokea benchi kabla ya Anicet Oura kupachika bao la tatu kwa shuti kali la mbali lililomshinda kipa wa Mtibwa na kujaa wavuni.
Shangwe la mashabiki hao lilipungua kutokana na wengi wao walikuwa wanasikiliza matokeo ya Yanga hasa watani wao walipokuwa wamepata bao la pili la penalti.
Simba ilianza mchezo huo kwa kasi na kufanya mashambulizi ya presha dakika nane za mwanzo, baadaye Mtibwa ikawa inajaribu kushambulia kwa kupiga mashuti ya mbali,jambo ambalo ni kama lilikuwa linapunguza nguvu kwa nyota wa Wanamsimbazi.
Simba mashambulizi yake mara nyingi yalikuwa yanaanzia kwa Kapombe, ambaye alikuwa anawalisha pasi za mwisho viungo na kama Clatous Chama aliye na mabao manane na asisti saba na kwa Elie Mpanzu mwenye mabao sita, asisti nane.
Kuanzia dakika ya 40 hadi ya 45 Mtibwa ilipeleka presha kwa mabeki wa Simba kwa kufika mara kwa mara golini kwao, huku Rushine mfungaji wa bao la kwanza aliweka umakini mkubwa wa kuondoa hatari.
Hata hivyo, kutokana na mechi kuwa tafu, wachezaji waliyopewa kadi za njano kipindi cha kwanza ni Kibabage na Said Mkopi ambaye ana mabao manne.
Kocha wa Simba, Steven Barker alifanya mabadiliko ya Alassane Kante ambaye ni mzuri zaidi kukaba akamuingiza Oura aliye na mabao matano.
Dakika ya 57 Oura aliwapunguza wachezaji wanne wa Mtibwa na kumpa krosi Libasse Gueye mwenye mabao manane aliyepiga shuti ambalo halikuwa na vipimo sahihi, akiwaacha mashabiki wakishangaa.
Katika mechi 28 Simba imeshinda 20, sare saba, imefungwa moja, imefunga mabao 52 imeruhusu mabao 17, ina pointi 67 na ipo nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu.
Kwa Mtibwa Sugar iliyopo nafasi ya 15 katika 28 imeshinda sita, sare tisa, imefungwa 13 imefunga mabao 23 imetikiswa nyavuni mara 44 ina pointi 27.